MAISHA YA
MASAHABA
صور من حياة الصحابة
Kimefasiriwa na Ustaadh Talib Juma
Huu ni Mji wa Madina, bado unatuliza huzuni zake
kwa kifo cha kipenzi - Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam). Na pia
unasikitishwa na kifo cha Khalifa Abubakr Assiddiyq, Alla amuwie radhi
Na hawa ni
wawakilishi mbali mbali wanakuja toka miji mbali mbali kumfanyia
bay-‘ah Khalifa ‘Umar ibn Al Khattaab juu ya utiifu kwa kila hali.
Asubuhi moja
ulimjia Amirul Muuminina ‘Umar, ujumbe wa Bahrain na kundi la wajumbe
wengine. Alikuwa ‘Umar Al Farouq ni mwenye hima ya kusikiliza ujumbe wa
wajumbe wote wanaomjia pengine, apate katika mazungumzo yao mawaidha na fikra
zenye manufaa au nasaha kwa ajili ya Allah na kitabu chake na kwa waislamu
wote. Lakini licha ya fursa waliyopewa hapakuwa na mazungumzo yenye kuingia
akilini mno.
Akamtazama mmoja
wa watu, alietarajia kwake kheri na akamwambia; "Sema ulichonacho".
Yule mtu akamshukuru Allah Subhaanahu Wata’ala na akasema; "Hakika wewe
ni Amirul Muuminina hujatawalishwa masuala ya umma huu ila ni mtihani wa
Allah Subhaanahu Wataa’ala amekuletea kwako. Mche Allah kwa yale
uliyotawalishwa na tambua akipotea kondoo mmoja pembezoni mwa mto Euphrate
(Alfurat) utaulizwa siku ya kiyama"
Amirul Muuminiina
alilia kwa sauti kubwa akasema; "Hakika hajapata mtu kuniambia maneno ya
ukweli tangu nilipopata ukhalifa kama ulivyoniambia wewe".
Akauliza; “Wewe
ni nani hasa?"
Akasema; “Al
Rabiy ibn Zayad Al Haarithy"
Akasema;“Ndugu
yake Al Muhajir ibn Zayad?"
Akasema; "Ndiyo."
Baada ya wageni
kuondoka, Amirul Muuminiina alimwita Abu Mussa
Al Ash’ary na akamwambia; “Hebu mfuatilie Al Rabiy ibn Zayad akiwa
ni mkweli, basi atakuwa ni mtu wa kheri nyingi na atatusaidia katika kazi
yetu. Hivyo mpe majukumu na uniandike habari zake".
Hazikupita siku
nyingi mpaka Abu Mussa Al Ash’ary alipotayarisha jeshi kufungua mji wa Manadhir
katika ardhi ya Al-Ahwazi. Kwa amri ya Khalifa akawachagulia
katika kikosi Al Rabiy ibn Zayad na ndugu yake Al Muhajir. Abu Mussa
Al-ash’ary aliuzunguka mji wa Manadhir na akaingia nao vitani, vita
ambavyo vilikuwa vikali havikuwa na mfano wake.
Washirikina
waliingia vitani kwa nguvu zao zote na subira ambavyo haikutarajiwa na
waislamu walikufa wengi bila ya matarajio. Waislamu walipigana siku hiyo
wakiwa wamefunga ndani ya Ramadhaan.
Alipoona Al
Muhajir vifo vimekuwa vingi ndani ya safu za waislamu, akaazimia kuiuza nafsi
yake kupata radhi za Allah Subhaanahu Wata’ala na akajitayarisha kwa mauti na
kumuusia ndugu yake.
Alitoka Al Rabiy
kwenda kwa Abu Mussa akamwambia; “Hakika Al Muhajir ameazimia leo kuiuza
nafsi yake kwa ajili ya Allah nae amefunga. Na waislamu wamo kwenye vita na
wamefunga jambo lenye kupunguza azma na nguvu zao na hawataki kufungua, hebu
fanya unaloliona (la kheri).”
Abu Mussa Al
Ash’ary akasimama na kulihutubia jeshi: “Enyi waislamu, naapa kwa kila
aliefunga kwamba afungue au aache kupigana”
Akachukua birika
la maji akanywa ili watu wamfuate. Aliposikia Al Muhajir maneno hayo akapiga
funda la maji na kusema; “ Wallahi sijapiga funda hili kwa sababu ya kiu
lakini ni kuitikia kiapo cha Amiri wangu.”
Akachukua upanga
wake akaanza kukata safu na kupambana bila ya khofu wala woga. Alipoingia
ndani ya jeshi la maadui wakamzingira kila pembe na panga zikamzingira mbele
na nyuma mpaka kufariki.
Wakakikata kichwa
chake na kukitundika juu ya nguzo refu katikati ya uwanja wa vita. Al Rabiy
akamtazama na kusema; “Umefanikiwa na marejeo mazuri. Wallahi nitalipiza
kisasi kwa ajili yako na kwa ajili ya waislamu waliouawa..” Abu Mussa
alipoona hali ile ya huzuni ya Al Rabiy juu ya ndugu yake na alidiriki
kinachompitikia kifuani mwake dhidi ya adui, aliamua kumpa uongozi wa kikosi
na akaelekea kufungua mji wa Al Suusi.
Al Rabiy na
askari wake waliwashambulia washirikina mfano wa kimbunga na kuzivamia ngome
zao mfano wa majabali yanayovamiwa na mafuriko. Wakavunjavunja safu zao na
kuvunja nguvu zao na Allah akajaalia ufunguzi wa Manadhir katika mikono
ya Al Rabiy ibn Zayad kwa kujisalimisha watu wake. Wakauawa waliojaribu
kupigana na wengine wakatekwa na waislamu kupata ngawira nyingi.
Nyota ya Al Rabiy
ibn Zayad iling'ara baada ya vita vya Manadhir na jina lake kutajwa na kila
ulimi. Akawa ni mmoja ya viongozi wakubwa wenye kupendwa na wanaotarajiwa
amali bora. Waislamu walipoazimia kufungua mji wa Sajistani alikabidhiwa
uongozi wa kikosi na kutarajiwa nusra.
Aliendelea Al
Rabiy ibn Zayad na jeshi lake la ufunguzi katika njia ya Allah kuelekea
Sajistan akikata pori lenye urefu meli sabini na tano zisizo rahisi hata
kukatwa na wanyama.
Ikawa mji wa
mwanzo kumkabili njiani ni Rostokzalik kwenye mipaka ya Sajistan. Hii
ni ngome kuu iliyokuwa na majengo na makasri ya fakhari yaliyo ndani ya ngome
kubwa na ndani yake mna aina mbali mbali za miti.
Al Rabiy alituma
wapelelezi kabla ya kuingia Rostokzalik. Wakapata habari ya kwamba maadui
walikuwa wanajitayarisha kwa moja ya sherehe zao. Akangoja awashtukizie usiku
wa sikukuu hiyo na aweze kuwateka na kuufungua mji bila ya vita.
Akawateka mateka
wasiopungua ishirini elfu na kiongozi wa mji ule akawa ni jumla ya mateka wa
vita. Mmoja ya waliotekwa alikuwa amekusanya mali ya kiongozi wake ifikayo
elfu thelathini[i] amekusanya kumpelekea kiongozi
wake. Al Rabiy akamuuliza;
“Umepata wapi
mali zote hizi?”
Akasema; “Kijiji
cha karibu cha bwana wangu.”
Akasema “ Je watu
wa kijiji kimoja wamemkusanyia na kumpa mali yote hii?”
Akasema; “Ndiyo”
Akasema; “Vipi?”
Akasema; “kwa
majembe yetu, masururu yetu na jasho letu.
Vita
viliposimama, mkubwa wa mji Adahqaan akaja kwa Al Rabiy kwa ajili ya
kutaka kutoa fidya ili aachiwe yeye na jamaa zake.
Akamwambia Al
Rabiy; “Nitakuachia huru ikiwa utatoa fidya ya kutosha kwa waislamu".
Akasema;
"Unataka kiasi gani?"
Akasema; "Chomeka
mkuki huu ardhini halafu ujaze dhahabu na fedha".
Akasema;
“Nimekubali”
Akaanza kutoa
fedha na dhahabu katika hazina zake na kuanza kujaza mkuki hadi ukazama.
Liliingia jeshi
la Al Rabiy ibn Zayad lenye kushinda ardhi ya Sajistan na zikawa ngome zake
ni zenye kuanguka moja baada ya nyengine kama majani ya miti yanavyopukutika
kwenye msimu wa baridi[ii].
Watu wa mji huo
wakawa ni wenye kujisalimisha na kutafuta amani kabla ya panga usoni mwao
mpaka Al Rabiy akafika mji wa Zaranji (mji Mkuu wa Sajistani)
Hapo walimkuta
adui amejidhatiti vya kutosha na katayarisha vikosi vya kupambana. Na
akatangulizia wasaidizi wa kumsaidia mapambano akiwa na azma ya kurejesha
nyuma kikosi cha waislamu kutoka mji mkuu na kusimamisha usongaji mbele wa
waislamu kutoka Sajistan kwa thamani yoyote ile.
Vita vikali
vilitokea baina Al Rabiy na maadui wake ambavyo uzito wa mhanga wake
ulielemea pande zote mbili. Alama za ushindi zilipoonekana kwa waislamu
aliona Mirzabani[iii] aliyejulikana kwa jina la Perwaz
aje kwa Al Rabiy kutafuta suluhu akiwa bado ana nguvu labda pengine
atafanikiwa yeye na watu kwa jambo zuri.
Akatuma mjumbe
wake kwa Al Rabiy kupeana miadi kwa ajili ya mazungumzo ya suluhu. Al Rabiy
aliwaamrisha watu wake wapange kwenye majlis mabaki ya askari wa kifursi na
njiani ambamo atapita Perwaz mtawanywe miili ya askari wake waliouawa.
Al Rabiy alikuwa
ni mtu mrefu wa kimo mwenye hima kubwa sana. Pia ni mwenye rangi
iliyokoza wekundu, mpana wa maumbo mwenye, kuogopesha kwa anaemtazama. Perwaz
alipoingia kwa Al Rabiy, mwili ulimsisimka na hofu kumjaa kwa miili ya maiti
njiani akashindwa kumkaribia Al Rabiy na hata kumpa mkono kumsalimia.
Akasema nae kwa
kigugumizi na kitetemeshi cha ulimi na akataka suluhu na kwamba atamletea
vijana elfu kila mmoja amebeba sinia yenye dhahabu na Al Rabiy alikubali
suluhu hiyo. Siku ya pili yake Al Rabiy aliingia mjini akiwa na vijana hao
huku waislamu wakileta tahlili[iv] na takbir[v] ilikuwa ni siku kubwa katika siku
za Allah.
Alibakia Al Rabiy
ibn Zayad akiwa kama upanga ndani ya mikono ya waislamu ukipambana na
maadui. Na Allah akawafungulia miji na majimbo hadi pale uongozi ulipokuwa
mikononi mwa Banu Umayyah na Mu’awiya ibn Abu Sufiyan. Al Rabiy akapewa
uliwali wa Khurasan lakini hakupendezwa na uongozi wa Banu Umayyah.
Akabaki na
kutoridhika kwake hadi pale Zayad ibn Abeyh mmoja wa viongozi wakuu wa Banu
Umayyah alipomwandikia na kumwambia:
“Amirul Muuminina
Mu’awiyah ibn Abi Sufiyan anakutaka ubakishe fedha na dhahabu katika Baytul Maal
na nyenginezo uzigawe kwa mujahidina.” Akamwandikia kumjibu; “Mimi
nimekipitia kitabu cha Allah kinaamrisha kinyume na unavyoniamrisha wewe
kupitia Amirul Muuminina.” Akawaita watu wake na kuwaambia chukueni ngawira
zenu.Na khumsu (moja ya tano) iliyobaki akaipeleka makao makuu ya ukhalifa
Damascus.
Ilipofika siku ya
Ijumaa akisoma barua ile, alitoka Al Rabiy ibn Zayad kwa ajili ya sala
ya Ijumaa akiwa amevaa nguo nyeupe akawahutubia watu (hotuba ya Ijumaa) na
akasema; “Enyi watu mimi nimeshachoshwa na uhai hivyo naomba du’aa na
itikieni Amin.”
Akasema; “Ewe
mola ikiwa ni mwenye kunitakia kheri basi nifishe haraka au kidogo kidogo”.
Watu wakaitikia; “Amin" Jua halikumaliza kuzama siku ile, Al Rabiy
akatangulia kwa Mola wake.
|
Al Rabiy Ibn Zayad Al Haarithy Upanga Unaopambana na Maadui
Subscribe to:
Posts (Atom)