004 - Hadiyth Ya 4: Ukweli Unapelekea Peponi, Uongo Unapelekea Motoni

004 - Hadiyth Ya 4: Ukweli Unapelekea Peponi, Uongo Unapelekea Motoni


عَنْ عَبْدُ الله إبنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم قَالَ: ((إِنَّ الصِّدْقَ يَهْدِي إِلَى الْبِرِّ وَإِنَّ الْبِرَّ يَهْدِي إِلَى الْجَنَّةِ, وَإِنَّ الرَّجُلَ لَيَصْدُقُ حَتَّى يَكُونَ صِدِّيقًا, وَإِنَّ الْكَذِبَ يَهْدِي إِلَى الْفُجُورِ وَإِنَّ الْفُجُورَ يَهْدِي إِلَى النَّارِ وَإِنَّ الرَّجُلَ لَيَكْذِبُ حَتَّى يُكْتَبَ عِنْدَ اللَّهِ كَذَّابًا)) متفق عليه
 
Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’uwd(رضي الله عنه)  kwamba Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hakika ukweli unaongoza katika wema, na hakika wema unaongoza Peponi, na mtu ataendelea kusema ukweli mpaka aandikiwe mbele ya Allaah kuwa ni mkweli. Na hakika uongo unaongoza katika uovu, na hakika uovu unapeleka motoni, na mtu ataendelea kusema uongo mpaka aandikiwe mbele ya Allaah kuwa ni muongo)).[1]
 
Mafunzo Na Hidaaya 
 
  1. Umuhimu wa kuwa na sifa ya ‘ukweli’ na iwe sifa kuu ya Muumin. [Al-Hujuraat 49: 15].
 
  1. Kuhimizwa na pendekezo katika kusema ukweli, kwani ni sababu ya kutenda mema. Na tahadharisho la uongo kwani ni sababu ya kutenda maovu.
 
  1. Hatari ya kufuata nyayo za shaytwaan za kuanza kusema uongo hadi unampeleka mtu motoni.
 
  1. Mkweli atajulikana kwa kupewa sifa ya ‘mkweli’, na muongo atajulikana kwa kupewa sifa ya ‘muongo’.
 
  1. Ukweli utamfaa mtu mwenyewe Aakhirah na matokeo na thawabu zake   ni kupata Pepo, na matokeo na malipo ya muongo ni adhabu kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى). [Al-Ahzaab 33: 24].
 
 قَالَ اللَّـهُ هَـٰذَا يَوْمُ يَنفَعُ الصَّادِقِينَ صِدْقُهُمْ ۚ لَهُمْ جَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ
Akasema Allaah: “Hii ndiyo Siku itakayowafaa as-Swaadiqiyna ukweli wao; watapata mabustani zipitazo chini yake mito; watadumu humo milele.  Allaah Amewawia Radhi, nao wawe radhi Naye. Huko ni kufuzu kukubwa.”[2]
 
 
  1. Ukweli uwe kwa niyyah, kauli na ‘amali njema ili alipwe mtu malipo mema.
 
  1. Muislamu atangamane na wakweli, nayo ni amri ya Allaah (سبحانه وتعالى) [At-Tawbah 9: 119] ili naye apate tabia ya ukweli.
 
  1. Allaah (سبحانه وتعالى) Amewasifu wakweli na Atawapa malipo mema kabisa. [Al-Ahzaab 33: 35, Al-Hadiyd 57: 18].
 
  1. Kusema uongo ni katika maovu yatendwayo na ulimi. [Rejea Hadiyth namba 37, 87, 93, 94, 126].
 



[1]  Al-Bukhaariy na Muslim.
[2]  Al-Maaidah (5: 119).