Soraqa Ibn Malik - Mfuatiliaji wa nyayo

Soraqa Ibn Malik - Mfuatiliaji wa nyayo


Waliamka Makureshi asubuhi moja wakiwa na hofu na shaka baada ya habari kufika kwenye vikao vyao kwamba Muhammad amekimbia Makka akijificha kwenye kiza cha usiku.
Viongozi wa Makureshi hawakuweza kusadiki habari hiyo. Wakavamia nyumba baada ya nyumba za Banu Hashim kumtafuta na kumuulizia kila nyumba ambayo alikuwa na masahaba wake, mpaka wakafika nyumbani kwa Abubakr. Akatoka mwanawe Asmaa. Abujahal akamuuliza; “Yuko wapi baba yako?” Akasema; “Sijui yuko wapi sasa hivi” Abujahal akanyanyua mkono wake na kumpiga kibao usoni kilichomfanya aanguke chini.

Wazimu uliwapanda viongozi wa Makureshi walipotambua yakini kwamba Muhammad amekwishaihama Makka. Wakakusanya kila wajuzi wa alama za nyayo ili kutambua ni njia gani amepita na kuanza kumtafuta.  Walipofika ghaar thawr[i] , mmoja wa wajuzi wa alama za nyayo aliwaambia;  “ Wallahi haiwezekani mtu wenu kupindukia pango hili”.

Na hawakuwa wamefanya kosa kwa waliyosema kuwaambia makureshi kwani Muhammad na Sahiba wake walikuwemo ndani ya pango lile na makureshi wamesimama juu yake.

Abubakar Siddiyq aliweza kuiona miguu yao ikipita juu yao na machozi yalimtoka. Mtume alimtazama kwa jicho la huruma na mapenzi.  Abubakar Siddiyq alimwambia kwa kumnon'goneza; “Wallahi silii kwa ajili ya nafsi yangu, lakini ni hofu ya kuona unasibiwa na jambo baya. Ewe Mtume wa Allah”. Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) akamwambia kwa kumtulizia; “Usihuzunike ewe Abubakar hakika Allah yuko pamoja nasi".

Allah akateremsha utulivu ndani ya moyo wa Abubakar na akawa anaitazama miguu ya makureshi huku akisema; “Ewe Mtume wa Allah, laiti mmoja wao angelitazama chini ya miguu yake basi angelituona” Mtume akamwambia;“Unadhani nini ewe Abubakar kwa wawili na Allah ni watatu wao? Hapo wakamsikia kijana wa kikuraish akiwaambia wenzake; “Njooni hapa pangoni tutazame ndani yake” Ummaiya bin Khalaf akamwambia kwa istihizai (utani), “Humuoni huyo buibui alietanda hapo mbele ya mlango? Wallahi huyo hapo ni mkongwe kuliko uhai wa Muhammad". Ama Abujahal yeye akasema; “Naapa kwa laata na ‘uzzah (miungu ya kikafiri) mimi nadhani yupo karibu nasi anatusikia na kuona tunayoyafanya lakini uchawi wake umeziba macho yetu.”

Lakini licha ya hivyo, makureshi hawakupangusa mikono na kuacha kumtafuta Muhammad wala hawakusita kufanya hivyo na kumsaka. Wakayatangazia makabila yao yaliyokuwa yakiishi baina ya njia ya Makka na Madina kwamba atakaefanikiwa kumleta Muhammad akiwa hai au amekufa atapata zawadi ya ngamia mia walio bora.

Soraqa bin Malik Al-Madlaj alikuwa katika majlis ya watu wake katika kijiji cha Qudeydi karibu na Makka mara mjumbe katika wajumbe wa kikuraish akaingia na kuwatangazia habari ya zawadi nono ambayo makureshi wamedhamini kwa atakaefanikiwa kuja na Muhammad akiwa hai au amekufa. Soraqa kusikia habari ya zawadi nono ya ngamia mia , tamaa ikamchukua. Lakini aliidhibiti nafsi yake na hakutamka lolote isije watu wengine wakajawa pia na tamaa. Kabla hajaondoka katika majlisi ile mtu mwengine aliingia akasema; “Wallahi kuna watu watatu wamenipita njiani nadhani hao ni Muhammad na Abubakar na muongozaji njia". Soraqa akasema; “Nadhani hao ni kina fulani wametoka kutafuta ngamia wao aliyepotea", Yule mtu akasema; “Pengine inawezekana” Na akanyamaza.

Soraqa akakaa kitambo akichelea watu wasitambue nini kinatokea  na watu walipoingia kwenye mazungumzo mengine akaondoka pole pole, haraka akaelekea nyumbani kwake na kumuelekeza mfanyakazi wake kisiri amtolee farasi wake bila watu kujua na akamfunge bondeni.

Akamuamrisha kijana wake amtayarishie silaha yake na atoke nayo nyuma ya nyumba siri siri bila ya kuonekana na aiweke mahala karibu na alipo farasi. Soraqa akavaa nguo zake za dirai (chuma) na kufunga upanga wake na kuchupia farasi wake. Haraka akaondoka kumtafuta Muhammad kabla ya mtu mwengine zaidi yake kufanikiwa kupata tuzo kubwa kwa Makureshi.

Soraqa bin Malik alikuwa ni mpandaji farasi shujaa baina ya watu wake  na alikuwa ni mrefu wa kimo mwenye hima kubwa ya mambo hodari wa kufuata alama za nyayo. Ni mwenye subira juu ya shida za safari. Pia alikuwa hodari, mweledi na mshairi. Na farasi wake alikuwa katika farasi wa aina bora.

Soraqa akatoka na kuanza kuikunja ardhi akiharakiza kumfikia Muhammad lakini njiani farasi wake alijikwaa na akumuangusha chini. Akaanza kuvunjika moyo na kusema; “Nini hichi? Farasi gani wewe?” Akampanda tena akajikwaa tena na kuanguka na akazidi kuvunjika moyo na akatamani arudi kwao kama sio tamaa ya kufuzu na ngamia mia moja.

Soraqa hakuwa mbali na pale alipoanguka Farasi ila akamuona Muhammad na wenzake wawili. Akanyanyuka  na  kutia mkono kiotani (kutoa mshale) lakini mkono wake ulishindwa kuuvuta kwani aliiona miguu ya farasi wake ikididimia ardhini na moshi unatoka baina ya miguu ya mbele ya farasi na kuyagubika macho ya farasi na yake yeye mwenyewe.

Akamuhimiza farasi kwenda lakini kazama ardhini kama kwamba amegongomelewa misumari. Akageuka upande wa Mtume na wenzake na akaita kwa sauti; “Enyi wawili niombeeni kwa Mola wenu amkomboe farasi wangu nami nakupeni ahadi ya kuacha kukufuateni” Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) akamuombea na Allah Subhaanahu Wata’ala akamtoa farasi wake ardhini. Lakini tamaa alizonazo zilimwandama tena  na akaanza tena kumfuata Mtume na mwenzake. Na mara hii farasi alizama zaidi michangani na akawaomba tena wamuombee kwa Allah Subhaanahu Wata’ala na akasema; “Chukueni kila kilicho changu, chakula, bidhaa na silaha  na nakuahidini kwamba nitamzuia kila anaejaribu kukufuateni” Wakamjibu; “Sisi hatuna haja ya vitu vyako, lakini mzuie kila anaejaribu kutufuata”.

Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) akamuombea na farasi akakomboka. Alipokuwa anataka kuondoka aliwaita na kuwaambia; “Subirini nizungumze nanyi, Wallahi hamtopata kutoka kwangu tendo lolote lile ambalo msingelipenda. Wakasema ; “Unataka nini kwetu?” Akasema; “Wallahi ewe Muhammad hakika mimi najua wazi kwamba dini itakuwa juu basi nipe ahadi nikija kwako kwenye mamlaka yako utanikirimu, na niandikie hayo”

Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) akamuamuru Abubakar kuandika (Mkataba) huo na akamuandika kwenye kipande cha mfupa na kumkabidhi. Wakati anaondoka Mtume  (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) alimwambia Soraqa; “Nawe utakuwaje siku ile utakapovaa mapambo ya Mfalme Kisra?” Soraqa akauliza kwa mshangao;“Kisra bin Hurmuz !?”

Akarudi nyumbani kwake akawakuta watu wake wamehamanika kumtafuta Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) nae akawaambia; “Rejeeni nishapekua kila pembe ya ardhi kumtafuta nanyi mnajua umahiri wangu wa kufuata nyayo basi rejeeni”. Halafu akaficha habari zake na Muhammad na sahaba wake mpaka akahakikisha kwamba wameshafika Madina na wako salama na maadui wa kikuraish.

Baada ya hapo akatangaza hadharani na alipozisikia Abu Jahal habari za Soraqa na Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) na msimamo wake alimlaumu kwa kumuwacha na kufanya woga na kuiacha fursa ya (tunzo). Akasema Soraqa kumjibu juu ya lawama zake; “Ewe Abul Hakam, laiti ungelikuwa shahidi wa yaliyomtokea farasi wangu na kuzama miguu yake basi ungelijua na usingelitia shaka kwamba Muhammad ni Mtume mwenye dalili, na nani atasimama mbele yeke?”

 Siku zikawa zenye kupita na Muhammad ametoka Makka huku akijificha kwenye kiza na huyu anarejea (baada ya kuikomboa) akiwa ni Bwana mfunguzi, akiungwa mkono na jeshi kubwa la watu wenye panga na mikuki yenye kumeremeta. Na hawa hapa viongozi wa makureshi ambao punde hivi waliijaza ardhi kiburi na ujabari, sasa wanamuelekea kwa hofu na wanatetemeka, wakimtaka awafanyie huruma na wakasema; “Nini unatarajia kutufanyia?" Akawaambia kwa huruma za kinabii; “Nendeni na mko huru” .

Wakati huo Soraqa akageuza mnyama wake na kuelekea kwa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) na kutangaza kusilimu kwake, huku mikononi mwake akiwa na ameshika mkataba alioandikiwa na Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) kabla ya miaka kumi nyuma.

Akasema Soraqa; “Nimekuja kwa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) kutokea Al-Jirana na nikajiunga na kikosi cha Ansaar wakawa wananipiga kwa mipini ya mikuki huku wakisema: "Kaa mbali, kaa mbali nini unataka?”
Nikawa najipitishapitisha mpaka nikawa karibu na Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) nae yupo juu ya ngamia wake. Nikanyanyua juu yale maandishi nikamwambia;

‘Ewe Mtume  wa Allah, mimi ni Soraqa bin Malik. Na haya ni maandiko yako kwangu”. Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) akasema; “Sogea Leo ni siku ya ahadi na wema.” Nikamsogelea na kutamka uislam mbele yake, na nikapata kheri na wema wake.

Haukupita muda baada ya Soraqa kukutana na Mtume  (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) ila ni miezi michache Allah akamukhitari Mtume wake (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam).

Soraqa alimhuzunikia sana Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam), na akawa anaikumbuka ile siku aliyokuwa akiwinda kumuuwa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) kwa ajili ya vijingamia na vipi leo ngamia wote wamekuwa hawana thamani hata ya ukucha wa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam).

Akawa daima anaikariri kauli ya Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam); “ Vipi siku ambayo utavaa mapambo ya Mfalme Kisra.?”Na hakuwa na shaka hata kidogo kwamba atayavaa.

Siku zikawa ni zenye kupita, na kuzunguka na masuala ya waislam yakawa ni yenye kusimamiwa na Amiirul Muuminiina Alfarouq-‘Umar ibnul Khattaab (Radhiyallahu ‘anhu).

Majeshi ya waislam kwenye kipindi hichi chenye baraka yakawa ni sawa na kimbunga dhidi ya mamlaka ya kifursi.Yakawa yenye kuvunja ngome na kuyashinda majeshi na kuteka ngawira mpaka Allah Subhaanahu Wata’ala akaangusha dola za Kisra mikononi mwa waislam.

Siku moja mwishoni mwishoni mwa ukhalifa wa Sayyidna ‘Umar, ulikuja Madina ujumbe wa Sa’ad bin Abi Waqaas na kumpa ishara ya ushindi wa waislam. Wakaja wamebeba mali kwa ajili ya Beit-al-mali ambayo ni khumsi (moja ya tano) ya mali ya ngawira za vita waliyoiteka wapiganiaji katika  njia ya Allah. Zilipowekwa mali hizo mbele ya Amirul Muuminiina alizitazama kwa mshangao.

Ndani ya mali hizo mlikuwa na taji la mfalme Kisra lililopambwa kwa kila aina ya vito vya thamani. Pia mlikuwa na nguo zake zilizoshonewa kwa nyuzi za dhahabu na kidani kilichotiwa johari. Na mabangili mawili ambayo macho hayajapatapo kuyaona na mali nyingi isiyo na mipaka ya vitu vyenye thamani.

‘Umar akawa anageuza huku na huko kwa fimbo aliyokuwa nayo mkononi na kusema:
 “Hakika watu wameleta mali hizi kwa wenye uaminifu”.


Akasema Sayyidna Ali bin Abi Talib ambae alikuwepo hapo wakati ule; “Laiti ungelichukuwa basi na wao wangelichukuwa”.

Hapo Al-Farouq alimwita Soraqa bin Malik na kumvalisha kanzu, suruali, kofia, viatu na kumvalisha ukanda na upanga na akaliweka taji juu ya kichwa. Waislam walisema kwa sauti:  “Allahu Akbar! Allahu Akbar! Allahu Akbar!.”

Kisha akageuka ‘Umar kwa Soraqa na kumwambia; “Hongera kwa mtu wa Bani Madlaji juu ya kichwa chake taji la Kisra.”  Soraqa akanyanyua uso juu mbinguni na kusema;
“Ewe Mola!  Hakika umemzuilia mali hii Mtume wako nae ni kipenzi chako zaidi yangu na mtukufu kwako zaidi. Na umemzuilia Abubakar umpendae zaidi yangu na mtukufu kwako zaidi. Na umenipa mimi najilindikiza kwako. Ikiwa umenipa kwa ajili ya kunitia mtihani.”

Hakusimama kwenye majlis ila baada ya kuigawa mali ile yote aliyokabidhiwa baina ya waislam.




 


[i] Mlima Thawr  uko nje kidogo ya mji wa Makkah