017 - Hadiyth Ya 17: Kuondosha Munkari Kwa Mkono Au Ulimi Au Kuchukia Moyoni


عن أبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيُّ (رضي الله عنه) قال: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم):  ((مَنْ رَأَى مِنْكُمْ مُنْكَرًا فَلْيُغَيِّرْهُ بِيَدِهِ فَإِنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَبِلِسَانِهِ فَإِنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَبِقَلْبِهِ وَذَلِكَ أَضْعَفُ الإيمَانِ)) رواه مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه) amesema: Nilimsikia Mtume wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) anasema: ((Atakayeona munkari [uovu] basi aubadilishe kwa mkono wake, na asipoweza basi kwa ulimi wake, na asipoweza basi kwa moyo wake [achukizwe] na huo ni udhaifu wa Iymaan)).[1]
 
Mafunzo Na Hidaaya:
 
  1. Wajibu wa Muislamu kuamrisha mema na kukataza munkari kwa hali yoyote ile. [Aal-‘Imraan 3: 110, At-Tawbah 9: 71, 112, Al-Hajj 22: 41].
 
 وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ
Na uweko (watokeze) kutoka kwenu Ummah unaolingania kheri na unaoamrisha ma’aruwf (mema) na unaokataza munkari. Na hao ndio waliofaulu[2]
 
  1. Kuamrisha mema na kukataza munkari ni jukumu la kila Muislamu na jamii, kwani ni fardhi kifaayah (ya kutosheleza). Walilaaniwa Ahlul-Kitaab wasiotimiza amri hii. [Al-Maaidah 5: 78-79].
 
  1. Imesemwa na Ma’ulamaa kuwa Hadiyth hii ni thuluthi ya Dini. Na imesemwa pia kuwa Uislamu wote umo humo, kwani vitendo katika Shari’ah ama ni vyema vinavyowajibika kutendwa au munkari vinavyowajibika kujiepusha navyo.

  1. Muislamu hatakiwi kuchangia katika maovu, bali kusaidia katika mema na uchaji Allaah. [Al-Maaidah 5: 2].
 
  1. Waislamu wako tofauti katika uwezo wa kukataza maovu.
 
  1. Iymaan ziko katika daraja tofauti. Inaongezeka katika kumtii Allaah (سبحانه وتعالى) na inapunguka katika kumuasi Allaah (سبحانه وتعالى).
 
  1. Muumin ni yule anayekataza maovu na asipoweza achukie kwa moyo wake au sivyo atakuwa katika hatari ya kupokutoka, kupata adhabu na kutokukubaliwa du’aa yake. [Hadiyth: ((Naapa kwa Ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake, hakika mtaamrishana ma’aruwf [wema] na mtakatazana munkari [maovu], au Allaah Atakuleteeni adhabu, kisha mtamuomba wala Hatokuitikieni)).[3]

  1. Baadhi ya Ma’ulamaa wameona kwamba lau ingelikuwa fardhi za Kiislamu ni sita, basi ya sita yake ingelikuwa ni kuamrishana mema na kukatazana maovu.
 




[1]  Muslim.
[2]  Aal-‘Imraan (3: 104).
[3]  At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan.