Fusw-Swilat: 41

  فُصِّلَت
Fusw-Swilat: 41

(Imeteremka Makka)


Sura hii imeanzia kwa harufi mbili katika harufi za alifbete kama inavyo fanya Qur'ani katika Sura nyingi. Sura hii imeeleza katika nyingi ya Aya zake shani ya Qur'ani na mambo iliyo kusanya yaliyo khusu bishara na maonyo. Na imeeleza msimamo wa washirikina kukhusu Qur'ani, katika kuipuuza na kuupiga vita wito wake, na msimamo wa Mtume kwa mnasaba wa makafiri, kwa kusimama imara juu ya wito wake kwao na kuwaambia: "Hakika mimi ni mtu kama nyinyi; inafunuliwa kwangu ya kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Basi tengeneeni kumwendea Yeye, na mumtake msamaha." Na Sura inaingilia kuwakumbusha washirikina uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kuziumba mbingu na ardhi, kisha inawahadharisha na yaliyo watokelea watu wa mataifa walio karibu mno na makwao, nao ni kina A'adi na Thamudi. Na inawakumbusha Siku ya Akhera, siku yatakapo washuhudia masikio yao, na macho yao, na ngozi zao, kwa waliyo kuwa wakiyatenda; na mijadiliano itakayo kuwa baina yao na viungo vyao siku hiyo; na watayo  yaomba wafwasi kwa Mola wao Mlezi Siku ya Kiyama: "Mola wetu Mlezi! Tuonyeshe wale walio tupoteza miongoni mwa majini na watu ili tuwaweke chini ya miguu yetu, wapate kuwa miongoni mwa walio chini kabisa." Na kama ilivyo kuwa mwendo wa Mwenyezi Mungu katika Kitabu hichi akisimulia khabari ya makafiri, husimulia pia khabari za Waumini. Basi Sura hii  imesimulia khabari za walio sema: "Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu", kisha wakasimama sawa sawa, neema za daima alizo waneemesha, na akalinganisha baina ya kheri na shari: "Wema haulingani na uovu".
Kisha Sura inataka watu waangalie Ishara za uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu zinazo onyesha kumkinika kufufuliwa maiti, kisha inarejea tena kuzidi kuwakemea wanao zigeuza Aya za Mwenyezi Mungu, na kwamba hao hawamkhofu Mwenyezi Mungu. Na kwamba hakika Kitabu hichi hakiingiliwi na upotovu kutoka mbele yake wala nyuma yake. Huu ni mteremsho ulio tokana na Mwenye hikima, Msifika. Na hakika Ujumbe wa Muhammad si ujumbe ulio zuliwa tu.
Na Sura inathibitisha khulka moja katika khulka za binaadammu, nayo ni kuwa Mwenyezi Mungu akimneemesha mtu huipuuza Haki, na ikimgusa tu shari anakuwa na madua marefu marefu.
Na Sura imekhitimisha kwa kuthibitisha mambo mawili muhimu kabisa, nayo ni la kwanza: kutaja kwa Qur'ani Tukufu yenyewe Haki iliyomo ndani yake isiyo na shaka yoyote: "Tutawaonyesha Aya zetu katika upeo wa macho na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli."  Na la pili lake kuwa hilo wanalo litegemea makafiri si lolote  ila ni shaka tu ya kufufuliwa iliyo wapelekea kuwa nayo ukafiri na upotovu. "Ama hakika wao bado wamo katika shaka ya kukutana na Mola wao Mlezi. Hakika Yeye amekizunguka kila kitu."



بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
حم﴿١﴾
1. Haa Miym.


تَنزِيلٌ مِّنَ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ﴿٢﴾
2. Ni uteremsho kutoka kwa Ar-Rahmaanir-Rahiym (Mwingi wa Rahmah - Mwenye kurehemu).


كِتَابٌ فُصِّلَتْ آيَاتُهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا لِّقَوْمٍ يَعْلَمُونَ﴿٣﴾
3. Kitabu zimefasiliwa (waziwazi) Aayaat zake, (ni) Qur-aan ya Kiarabu kwa watu wanaoelewa.


بَشِيرًا وَنَذِيرًا فَأَعْرَضَ أَكْثَرُهُمْ فَهُمْ لَا يَسْمَعُونَ﴿٤﴾
4. Kinachobashiria (mazuri) na kinachoonya; lakini wamekengeuka wengi wao, basi wao hawasikii.


وَقَالُوا قُلُوبُنَا فِي أَكِنَّةٍ مِّمَّا تَدْعُونَا إِلَيْهِ وَفِي آذَانِنَا وَقْرٌ وَمِن بَيْنِنَا وَبَيْنِكَ حِجَابٌ فَاعْمَلْ إِنَّنَا عَامِلُونَ﴿٥﴾
5. Na wakasema: “Nyoyo zetu zimo katika vifuniko kwa yale unayotuitia, na masikioni mwetu mna uziwi na baina yetu na baina yako (kuna) kizuizi, basi tenda nasi tunatenda (tutakavyo).”


قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُوحَىٰ إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ فَاسْتَقِيمُوا إِلَيْهِ وَاسْتَغْفِرُوهُ ۗ وَوَيْلٌ لِّلْمُشْرِكِينَ﴿٦﴾
6. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika mimi ni mtu kama nyinyi; hufunuliwa Wahy kwamba: Ilaah (Muabudiwa wa haki) wenu ni Ilaah Mmoja, basi thibitikeni imara Kwake, na mwombeni maghfirah. Na ole kwa washirikina.


الَّذِينَ لَا يُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُم بِالْآخِرَةِ هُمْ كَافِرُونَ﴿٧﴾
7. Ambao hawajitakasi kutokana na shirki na wao kwa Aakhirah wenye kuikanusha.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُمْ أَجْرٌ غَيْرُ مَمْنُونٍ﴿٨﴾
8. Hakika wale walioamini na wakatenda mema watapata ujira usiokatika.


قُلْ أَئِنَّكُمْ لَتَكْفُرُونَ بِالَّذِي خَلَقَ الْأَرْضَ فِي يَوْمَيْنِ وَتَجْعَلُونَ لَهُ أَندَادًا ۚ ذَٰلِكَ رَبُّ الْعَالَمِينَ﴿٩﴾
9. Sema: “Je, hivi nyinyi mnamkufuru Yule Aliyeumba ardhi kwa siku mbili, na mnamfanyia waliolingana Naye? Huyo Ndiye Rabb (Mola) wa walimwengu.”


وَجَعَلَ فِيهَا رَوَاسِيَ مِن فَوْقِهَا وَبَارَكَ فِيهَا وَقَدَّرَ فِيهَا أَقْوَاتَهَا فِي أَرْبَعَةِ أَيَّامٍ سَوَاءً لِّلسَّائِلِينَ﴿١٠﴾
10. Na Akaweka humo milima juu yake, na Akabariki humo, na Akakadiria humo (kwa viumbe) rizki yake katika siku nne zilizo sawasawa kwa (taarifa ya) wanaouliza.


ثُمَّ اسْتَوَىٰ إِلَى السَّمَاءِ وَهِيَ دُخَانٌ فَقَالَ لَهَا وَلِلْأَرْضِ ائْتِيَا طَوْعًا أَوْ كَرْهًا قَالَتَا أَتَيْنَا طَائِعِينَ﴿١١﴾
11. Kisha Istawaa (Yuko juu kwa namna inayolingana na Utukufu Wake Yeye Mwenyewe Allaah) kuzielekea mbingu nazo ni moshi; Akaiambia (mbingu) na ardhi: “Njooni kwa khiari au bila khiari.”  Zikasema: “Tumekuja hali ya kuwa wenye utiifu.”


فَقَضَاهُنَّ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ فِي يَوْمَيْنِ وَأَوْحَىٰ فِي كُلِّ سَمَاءٍ أَمْرَهَا ۚ وَزَيَّنَّا السَّمَاءَ الدُّنْيَا بِمَصَابِيحَ وَحِفْظًا ۚ ذَٰلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ﴿١٢﴾
12. Akamaliza kuziumba mbingu saba katika siku mbili, na Akatia ilhamu katika kila mbingu jambo lake; na Tukaipamba mbingu ya dunia kwa taa (nyota) na hifadhi. Hayo ni takdiri ya Al-‘Aziyzil-‘Aliym (Mwenye nguvu zote Asiyeshindika - Mjuzi wa yote).


فَإِنْ أَعْرَضُوا فَقُلْ أَنذَرْتُكُمْ صَاعِقَةً مِّثْلَ صَاعِقَةِ عَادٍ وَثَمُودَ﴿١٣﴾
13. Wakikengeuka, basi sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Nakuhadharisheni radi na umeme angamizi mfano wa radi na umeme angamizi wa kina ‘Aad na Thamuwd.”


إِذْ جَاءَتْهُمُ الرُّسُلُ مِن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا اللَّـهَ ۖ قَالُوا لَوْ شَاءَ رَبُّنَا لَأَنزَلَ مَلَائِكَةً فَإِنَّا بِمَا أُرْسِلْتُم بِهِ كَافِرُونَ﴿١٤﴾
14. Walipowajia Rasuli mbele yao na nyuma yao (kuwalingania) kwamba: “Msimuabudu isipokuwa Allaah.” Wakasema: “Angelitaka Rabb (Mola) wetu, bila shaka Angeliteremsha Malaika; na hakika sisi ni wenye kuyakanusha yale mliyotumwa nayo”.


فَأَمَّا عَادٌ فَاسْتَكْبَرُوا فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَقَالُوا مَنْ أَشَدُّ مِنَّا قُوَّةً ۖ أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّـهَ الَّذِي خَلَقَهُمْ هُوَ أَشَدُّ مِنْهُمْ قُوَّةً ۖ وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يَجْحَدُونَ﴿١٥﴾
15. Ama kina ‘Aad, walitakabari katika ardhi bila ya haki, na wakasema: “Nani mwenye nguvu kuliko sisi?” Je, hawakuona kwamba Allaah Ambaye Amewaumba Ndiye Mwenye nguvu zaidi kuliko wao? Na walikuwa wanazikanusha Aayaat (ishara, dalili) Zetu.


فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا صَرْصَرًا فِي أَيَّامٍ نَّحِسَاتٍ لِّنُذِيقَهُمْ عَذَابَ الْخِزْيِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَخْزَىٰ ۖ وَهُمْ لَا يُنصَرُونَ﴿١٦﴾
16. Basi Tukawapelekea upepo wa dhoruba na mngurumo katika siku za mikosi ili Tuwaonjeshe adhabu ya hizaya katika uhai wa dunia; na bila shaka adhabu ya Aakhirah ni ya hizaya zaidi, nao hawatonusuriwa.


وَأَمَّا ثَمُودُ فَهَدَيْنَاهُمْ فَاسْتَحَبُّوا الْعَمَىٰ عَلَى الْهُدَىٰ فَأَخَذَتْهُمْ صَاعِقَةُ الْعَذَابِ الْهُونِ بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ﴿١٧﴾
17. Na ama kina Thamuwd, Tuliwaongoza, lakini walifadhilisha upofu kuliko Uongofu basi ikawachukuwa radi na umeme angamizi wa adhabu idhalilishayo kwa yale waliyokuwa wakichuma.


وَنَجَّيْنَا الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ﴿١٨﴾
18. Na Tukawaoka wale walioamini na walikuwa wenye taqwa.


وَيَوْمَ يُحْشَرُ أَعْدَاءُ اللَّـهِ إِلَى النَّارِ فَهُمْ يُوزَعُونَ﴿١٩﴾
19. Na Siku watakayokusanya maadui wa Allaah kwenye Moto, nao wanapangwa safusafu.


حَتَّىٰ إِذَا مَا جَاءُوهَا شَهِدَ عَلَيْهِمْ سَمْعُهُمْ وَأَبْصَارُهُمْ وَجُلُودُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٢٠﴾
20. Mpaka watakapoufikia yatashuhudia dhidi yao, masikio yao, na macho yao, na ngozi zao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.


وَقَالُوا لِجُلُودِهِمْ لِمَ شَهِدتُّمْ عَلَيْنَا ۖ قَالُوا أَنطَقَنَا اللَّـهُ الَّذِي أَنطَقَ كُلَّ شَيْءٍ وَهُوَ خَلَقَكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ﴿٢١﴾
21. Na wataziambia ngozi zao: “Mbona mnashuhudia dhidi yetu?” Zitasema: “Ametutamkisha Allaah Ambaye Ametamkisha kila kitu, Naye (Ndiye) Aliyekuumbeni mara ya kwanza na Kwake mtarejeshwa.


وَمَا كُنتُمْ تَسْتَتِرُونَ أَن يَشْهَدَ عَلَيْكُمْ سَمْعُكُمْ وَلَا أَبْصَارُكُمْ وَلَا جُلُودُكُمْ وَلَـٰكِن ظَنَنتُمْ أَنَّ اللَّـهَ لَا يَعْلَمُ كَثِيرًا مِّمَّا تَعْمَلُونَ﴿٢٢﴾
22. “Na hamkuwa mkijisitiri hata yasishuhudie masikio yenu, na wala macho yenu, na wala ngozi zenu; lakini mlidhania kwamba Allaah Hajui mengi katika yale mnayoyatenda.


وَذَٰلِكُمْ ظَنُّكُمُ الَّذِي ظَنَنتُم بِرَبِّكُمْ أَرْدَاكُمْ فَأَصْبَحْتُم مِّنَ الْخَاسِرِينَ﴿٢٣﴾
23. “Na hivyo dhana yenu mliyokuwa mkimdhania Rabb (Mola) wenu, imekuangamizeni, mmekuwa miongoni mwa waliokhasirika.”


فَإِن يَصْبِرُوا فَالنَّارُ مَثْوًى لَّهُمْ ۖ وَإِن يَسْتَعْتِبُوا فَمَا هُم مِّنَ الْمُعْتَبِينَ﴿٢٤﴾
24. Basi (hata) wakivuta subira, Moto ndio makazi yao; na wakitafuta kuomba radhi, basi wao hawatokuwa miongoni mwa wenye kuruhusiwa kuridhisha.


وَقَيَّضْنَا لَهُمْ قُرَنَاءَ فَزَيَّنُوا لَهُم مَّا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَحَقَّ عَلَيْهِمُ الْقَوْلُ فِي أُمَمٍ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِم مِّنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ ۖ إِنَّهُمْ كَانُوا خَاسِرِينَ﴿٢٥﴾
25. Na Tuliwawekea marafiki wandani (wa kishaytwaan) wakawapambia yale yaliyo mbele yao na ya nyuma yao (ya madhambi), na ikawathibitikia kauli (ya adhabu wawe) katika umati nyingi zilizokwishapita kabla yao miongoni mwa majini na wanadamu; kwamba wao wamekuwa wenye kukhasirika.


وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَا تَسْمَعُوا لِهَـٰذَا الْقُرْآنِ وَالْغَوْا فِيهِ لَعَلَّكُمْ تَغْلِبُونَ﴿٢٦﴾
26. Na wale waliokufuru wakasema: “Msiisikilize hii Qur-aan na ifanyieni rabsha (inaposomwa) huenda mkashinda.”


فَلَنُذِيقَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا عَذَابًا شَدِيدًا وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَسْوَأَ الَّذِي كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٢٧﴾
27. Bila shaka Tutawaonjesha wale waliokufuru adhabu kali, na bila shaka Tutawalipa uovu zaidi wa yale waliokuwa wakiyatenda.


ذَٰلِكَ جَزَاءُ أَعْدَاءِ اللَّـهِ النَّارُ ۖ لَهُمْ فِيهَا دَارُ الْخُلْدِ ۖ جَزَاءً بِمَا كَانُوا بِآيَاتِنَا يَجْحَدُونَ﴿٢٨﴾
28. Hiyo ndio jazaa ya maadui wa Allaah – Moto; watapata humo makazi yenye kudumu; ndio jazaa (yao) kwa sababu walikuwa wakizikanusha Aayaat, (dalili na ishara) Zetu.


وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا رَبَّنَا أَرِنَا اللَّذَيْنِ أَضَلَّانَا مِنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ نَجْعَلْهُمَا تَحْتَ أَقْدَامِنَا لِيَكُونَا مِنَ الْأَسْفَلِينَ﴿٢٩﴾
29. Na watasema wale waliokufuru: “Rabb (Mola) wetu! Tuonyeshe wale waliotupotoa miongoni mwa majini na wanadamu tuwaweke chini ya miguu yetu ili wawe miongoni mwa wa chini kabisa (Motoni).”


إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ﴿٣٠﴾
30. Hakika wale waliosema: “Rabb (Mola) wetu ni Allaah.” Kisha wakathibitika imara; Malaika huwateremkia (wanapofishwa kuwaambia): “Msikhofu, na wala msihuzunike, na pokeeni bishara njema ya Jannah ambayo mlikuwa mkiahidiwa.”


نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ﴿٣١﴾
31. “Sisi ni marafiki walinzi wenu katika uhai wa dunia na katika Aakhirah. Na mtapata humo yale yanayotamani nafsi zenu, na mtapata humo yale mtakayoomba.


نُزُلًا مِّنْ غَفُورٍ رَّحِيمٍ﴿٣٢﴾
32. “Ni takrima kutoka kwa Ghafuwrir-Rahiym (Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu).”


وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّـهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ﴿٣٣﴾
33. Na nani mwenye kauli nzuri zaidi kuliko yule anayelingania (watu) kwa Allaah na akatenda mema na akasema: “Hakika mimi ni miongoni mwa Waislamu.”


وَلَا تَسْتَوِي الْحَسَنَةُ وَلَا السَّيِّئَةُ ۚ ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ فَإِذَا الَّذِي بَيْنَكَ وَبَيْنَهُ عَدَاوَةٌ كَأَنَّهُ وَلِيٌّ حَمِيمٌ﴿٣٤﴾
34. Na wala haulingani sawa wema na uovu. Lipiza (uovu ulilotendewa) kwa ambalo ni zuri zaidi; tahamaki yule ambaye baina yako na baina yake kuna uadui, atakuwa kama ni rafiki mwandani.


وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا ذُو حَظٍّ عَظِيمٍ﴿٣٥﴾
35. Na hawatopewa (sifa hii) isipokuwa wale waliovuta subira, na hapewi hayo isipokuwa mwenye fungu (jema) adhimu.


وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ﴿٣٦﴾
36. Na utakapokuchochea uchochezi kutoka kwa shaytwaan, basi omba kinga kwa Allaah. Hakika Yeye Ndiye As-Samiy’ul-‘Aliym (Mwenye kusikia yote - Mjuzi wa yote).


وَمِنْ آيَاتِهِ اللَّيْلُ وَالنَّهَارُ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ ۚ لَا تَسْجُدُوا لِلشَّمْسِ وَلَا لِلْقَمَرِ وَاسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي خَلَقَهُنَّ إِن كُنتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ﴿٣٧﴾
37. Na katika Aayaat (ishara, dalili) Zake, ni usiku na mchana, na jua na mwezi.  (Basi) Msisujudie jua wala mwezi; bali msujudieni Allaah Ambaye Aliyeviumba ikiwa Yeye Pekee mnawambudu.


فَإِنِ اسْتَكْبَرُوا فَالَّذِينَ عِندَ رَبِّكَ يُسَبِّحُونَ لَهُ بِاللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَهُمْ لَا يَسْأَمُونَ ۩﴿٣٨﴾
38. Lakini wakitakabari, basi wale (Malaika) walio kwa Rabb (Mola) wako wanamsabbih usiku na mchana, nao wala hawachoki.


وَمِنْ آيَاتِهِ أَنَّكَ تَرَى الْأَرْضَ خَاشِعَةً فَإِذَا أَنزَلْنَا عَلَيْهَا الْمَاءَ اهْتَزَّتْ وَرَبَتْ ۚ إِنَّ الَّذِي أَحْيَاهَا لَمُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۚ إِنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٣٩﴾
39. Na katika Aayaat (ishara, dalili) Zake, ni kwamba utaona ardhi imetulia (kavu) kisha Tunapoiteremshia maji, hutikisika na hututumka (iote mimea). Hakika Yule Aliyeihuisha, bila shaka ni Mwenye kuhuisha wafu, hakika Yeye juu ya kila kitu ni Qadiyr (Muweza).


إِنَّ الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي آيَاتِنَا لَا يَخْفَوْنَ عَلَيْنَا ۗ أَفَمَن يُلْقَىٰ فِي النَّارِ خَيْرٌ أَم مَّن يَأْتِي آمِنًا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ اعْمَلُوا مَا شِئْتُمْ ۖ إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ﴿٤٠﴾
40. Hakika wale wanaozipotosha Aayaat Zetu hawawei kujificha kwetu. Je, basi yule atakayetupwa katika Moto ni bora au yule atakayekuja akiwa katika amani Siku ya Qiyaamah? Tendeni mpendavyo; hakika Yeye kwa myatendayo ni Baswiyr (Mwenye kuona).


إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِالذِّكْرِ لَمَّا جَاءَهُمْ ۖ وَإِنَّهُ لَكِتَابٌ عَزِيزٌ﴿٤١﴾
41. Hakika wale waliokanusha Adh-Dhikri (Qur-aan) ilipowajia (wataangamia). Na hakika hicho ni Kitabu chenye utukufu na udhibiti.


لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ ۖ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ﴿٤٢﴾
42. Haitokifikia ubatili mbele yake, na wala nyuma yake; ni uteremsho kutoka kwa Hakiymin-Hamiyd (Mwenye hikmah wa yote - Mwenye kustahiki kuhimidiwa kwa yote).


مَّا يُقَالُ لَكَ إِلَّا مَا قَدْ قِيلَ لِلرُّسُلِ مِن قَبْلِكَ ۚ إِنَّ رَبَّكَ لَذُو مَغْفِرَةٍ وَذُو عِقَابٍ أَلِيمٍ﴿٤٣﴾
43. Huambiwi (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) isipokuwa yale yale waliyokwisha ambiwa Rasuli kabla yako. Hakika Rabb (Mola) wako ni Mwenye maghfirah na Mwenye adhabu iumizayo.


وَلَوْ جَعَلْنَاهُ قُرْآنًا أَعْجَمِيًّا لَّقَالُوا لَوْلَا فُصِّلَتْ آيَاتُهُ ۖ أَأَعْجَمِيٌّ وَعَرَبِيٌّ ۗ قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدًى وَشِفَاءٌ ۖ وَالَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ فِي آذَانِهِمْ وَقْرٌ وَهُوَ عَلَيْهِمْ عَمًى ۚ أُولَـٰئِكَ يُنَادَوْنَ مِن مَّكَانٍ بَعِيدٍ﴿٤٤﴾
44. Na lau Tungeliifanya Qur-aan lugha isiyokuwa ya Kiarabu bila shaka wangelisema: “Mbona hazikufasiliwa Aayaat zake?  Ah! Ya lugha ya kigeni na hali (Nabiy) ni Mwarabu!?” Sema: “Hiyo ni kwa walioamini ni Mwongozo na shifaa. Na wale wasioamini, wana uziwi masikioni mwao nayo ni upofu kwao. Hao wanaitwa kutoka mahali mbali.


وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ فَاخْتُلِفَ فِيهِ ۗ وَلَوْلَا كَلِمَةٌ سَبَقَتْ مِن رَّبِّكَ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ ۚ وَإِنَّهُمْ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ مُرِيبٍ﴿٤٥﴾
45. Na kwa yakini Tulimpa Muwsaa Kitabu (Tawraat), kisha kikahitilafiwa. Na lau si neno lilotangulia (kuwaakhirishia adhabu) kutoka kwa Rabb (Mola) wako, bila shaka ingelihukumiwa baina yao. Na hakika wao bila shaka wamo katika shaka nayo (Qur-aan, shaka) yenye kuwatia wasiwasi.


مَّنْ عَمِلَ صَالِحًا فَلِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ أَسَاءَ فَعَلَيْهَا ۗ وَمَا رَبُّكَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ﴿٤٦﴾
46. Yeyote yule atakayetenda mema basi ni kwa ajili ya nafsi yake, na yeyote yule atakayefanya uovu, basi ni dhidi yake; na Rabb (Mola) wako si dhalimu kamwe kwa waja (Wake).



إِلَيْهِ يُرَدُّ عِلْمُ السَّاعَةِ ۚ وَمَا تَخْرُجُ مِن ثَمَرَاتٍ مِّنْ أَكْمَامِهَا وَمَا تَحْمِلُ مِنْ أُنثَىٰ وَلَا تَضَعُ إِلَّا بِعِلْمِهِ ۚ وَيَوْمَ يُنَادِيهِمْ أَيْنَ شُرَكَائِي قَالُوا آذَنَّاكَ مَا مِنَّا مِن شَهِيدٍ﴿٤٧﴾
47. Kwake (Pekee) unarudishwa ujuzi wa Saa (Qiyaamah). Na hayatoki matunda yoyote kutoka mafumbani mwake, na wala habebi mimba mwanamke yeyote na wala hazai isipokuwa kwa ujuzi Wake. Na Siku Atakayowaita (Aseme): “Wako wapi washirika Wangu?” Watasema: “Tunakiri Kwako hapana miongoni mwetu anayeshudia (hayo).”


وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَدْعُونَ مِن قَبْلُ ۖ وَظَنُّوا مَا لَهُم مِّن مَّحِيصٍ﴿٤٨﴾
48. Na yatawapotea yale waliyokuwa wakiyaomba kabla na watayakinisha hawana mahali pa kukimbilia.


لَّا يَسْأَمُ الْإِنسَانُ مِن دُعَاءِ الْخَيْرِ وَإِن مَّسَّهُ الشَّرُّ فَيَئُوسٌ قَنُوطٌ﴿٤٩﴾
49. Insani hachoki kuomba du’aa za kheri. Na inapomgusa shari, basi huwa mwenye kukosa tumainio lolote, mwenye kukata tamaa kabisa.


وَلَئِنْ أَذَقْنَاهُ رَحْمَةً مِّنَّا مِن بَعْدِ ضَرَّاءَ مَسَّتْهُ لَيَقُولَنَّ هَـٰذَا لِي وَمَا أَظُنُّ السَّاعَةَ قَائِمَةً وَلَئِن رُّجِعْتُ إِلَىٰ رَبِّي إِنَّ لِي عِندَهُ لَلْحُسْنَىٰ ۚ فَلَنُنَبِّئَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِمَا عَمِلُوا وَلَنُذِيقَنَّهُم مِّنْ عَذَابٍ غَلِيظٍ﴿٥٠﴾
50. Na Tunapomuonjesha Rahmah kutoka Kwetu baada ya dhara iliyomgusa, bila shaka husema: “Hii ni kwa ajili yangu (nastahiki) na sidhani kama Saa (Qiyaamah) itasimama. Na nitakaporejeshwa kwa Rabb (Mola) wangu hakika nitapata mazuri Kwake.” Basi bila shaka Tutawabainishia wale waliokufuru yale waliyoyatenda, na bila shaka Tutawaonjesha adhabu nzito.


وَإِذَا أَنْعَمْنَا عَلَى الْإِنسَانِ أَعْرَضَ وَنَأَىٰ بِجَانِبِهِ وَإِذَا مَسَّهُ الشَّرُّ فَذُو دُعَاءٍ عَرِيضٍ﴿٥١﴾
51. Na Tunapomneemesha insani hukengeuka na kujitenga upande. Na inapomgusa shari, basi mara huwa mwenye du’aa refu refu.



قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِن كَانَ مِنْ عِندِ اللَّـهِ ثُمَّ كَفَرْتُم بِهِ مَنْ أَضَلُّ مِمَّنْ هُوَ فِي شِقَاقٍ بَعِيدٍ﴿٥٢﴾
52. Sema: “Je, mnaonaje ikiwa (Qur-aan) ni kutoka kwa Allaah, kisha mkaikufuru, ni nani aliyepotoka zaidi kuliko yule aliye katika upinzani wa mbali?”


سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ ۗ أَوَلَمْ يَكْفِ بِرَبِّكَ أَنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ﴿٥٣﴾
53. Tutawaonyesha Aayaat (ishara, dalili) Zetu katika peo (sayari) za mbali na katika nafsi zao, mpaka iwabainike kwamba hiyo ni haki! Je, haitoshelezi Rabb (Mola) wako kuwa Yeye juu ya kila kitu ni Shahiyd (Mwenye kushuhudia).


أَلَا إِنَّهُمْ فِي مِرْيَةٍ مِّن لِّقَاءِ رَبِّهِمْ ۗ أَلَا إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ مُّحِيطٌ﴿٥٤﴾
54. Tanabahi! Hakika wao wamo katika shaka ya kukutana na Rabb (Mola) wao. Tanabahi! Hakika Yeye kwa kila kitu ni Muhiytw (Mwenye kukizunguka kwa ujuzi Wake).




Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejeauliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii falhaqqiy@gmail.com