Nuaim Ibn Masoud - Vita ni Hadaa
Nu’aim
ibn Masoud ni kijana alie na moyo mpana na akili nyingi na mbinu za kutosha na
asieshindwa na jambo bali huwa na hila na njia za kutoka. Ni mfano bora wa
kijana wa jangwani kwa kila maana, kutokana na sifa aliyopewa na Allah
Subhaanahu Wata’ala ya kufikiria.
Lakini alikuwa ni mwenye kupenda raha na urafiki ambao
aliudhihirisha kwa marafiki zake wa kiyahudi wa Madina. Alikuwa kila anapotaka
starehe ya waimbaji wa kike na masikio yakitamani nyuzi za ala (Muziki na
nyimbo), hufanya safari kutoka kwao Najd na kuelekea Madina ambapo hupoteza
mali nyingi kwa mwanamke wa kiyahudi ili apate starehe kwa wingi.
Hili
lilimfanya mara kwa mara aende na kurudi Madina jambo lililopelekea awe na
urafiki mkubwa na mayahudi hasa wa kabila la Bani Quraidhah.
Mwenyezi
Mungu aliukarimu ubinadamu kwa kuwateremshia Mtume wa uongofu na haki na
vichochoro vya Madina kung’ara kwa nuru ya Uislamu. Alikuwa Nu’aim bado ni
mwenye kuzama nafsi yake katika dimbwi la matamanio, akaupinga uislam kwa nguvu
zake zote, akiogopea usijemzuia na matamanio yake na raha zake. Akajikuta
nafsi yake ni mwenye kujiunga na mahasimu wa Uislamu wakubwa akiwa tayari kutoa
upanga dhidi yake.
Lakini
Nu’aim ibn Masoud alifungua ukurasa mpya siku ya vita ya Al - Ahzaab katika
tarehe ya da’awah ya kiislamu na akajiweka katika kurasa hizo za kitabu cha
mbinu na hadaa za kivita. Kisa ambacho kingali kinasimuliwa na tarehe kwa
mshangao kwa milango yake madhubuti na kwa mshangao wa ushujaa wake na umahiri
wa akili yake. Ili usimame katika kisa hiki cha Nu’aim ni lazima urejee kwanza
nyuma kidogo.
Kabla
ya vita vya Al - Ahzaab kwa muda mdogo, mayahudi walikutana Madina na viongozi
wao wakawa wanakusanya makundi kwa ajili ya kumpiga vita Mtume (Sallallahu
‘Alayhi Wasallam) na kuivunja dini yake.
Wakawaendea
Makureshi, Makkah na kuwashawishi kupambana dhidi ya waislamu na wakawaahidi
kuwaunga mkono watakapowasili Madina na wakapeana ahadi bila ya kuivunja na
wakawapa wakati maalum.
Makureshi
walitoka Makkah kwa jumla yao, walio juu ya vipando na waendao kwa miguu
wakiongozwa na Abu Sufiyan wakielekea Madina. Wakatoka Ghatfan kutoka Najd na
kila kitu chao na watu wao wakiongozwa na kiongozi wao Uyeynah ibn Hisnu Al
-Ghatfany na miongoni mwao ni shujaa wa kisa hichi Nu’aim ibn Masoud.
Mtume
(Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) alipopata habari ya kutoka kwao, aliwakusanya
masahaba wake na kuwashauri juu ya hali hii na hatua ya kuchimba Khandak
ikapitishwa kuuzunguka mji wa Madina, ili kuzuia uvamizi huu na Khandak kuwa ni
kizuizi kikuu dhidi ya jeshi hilo.
Kabla
ya kukaribia vikosi vya Makkah na Najd milangoni mwa Madina, viongozi wa
Mayahudi Banu Nadhir waliwaendea viongozi wa mayahudi wa Bani Quraidhah na
kuaanza kuwashawishi kuingia vitani pamoja nao dhidi ya Muhammad na kuwataka
kuyaunga mkono majeshi ya Makkah na Najd. Lakini viongozi wa Banu Quraidhah
wakawajibu; “Hakika mumetuambia jambo tunalolipenda na kulitaka lakini mnajua
kuwa sisi na Muhammad tuna mikataba ili tuweze kuishi Madina kwa salama na
amani, na hata wino wa mikataba hiyo bado haujakauka.”
“Nasi
tunaogopa atakaposhinda Muhammad vita, atatushambulia kwa nguvu zote, na
kututoa Madina ikiwa ni malipo ya khiyana yetu.”
Lakini
viongozi wa Banu Nadhir wakazidi kuwaghururi Banu Quraidhah kuvunja
mkataba na kuwahakikishia ushindi na hilo halina muhali.
Wakawatia
tamaa kwa sababu ya vikosi viwili vikubwa ambavyo vinashiriki. Banu Quraidhah
wakalainika na kuvunja mkataba wao na Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam).
Wakachanachana waraka wa mkataba na wakatangaza kujiunga na washirika wa Al -
Ahzaab katika vita. Waislam waliipokea habari hii kama vile radi. Majeshi ya Al
- Ahzaab yaliuzunguka mji wa Madina na kukata njia za misaada na vyakula. Mtume
(Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) akahisi hakika sasa yumo ndani ya midomo ya
makulabu ya adui.
Makureshi
na Ghatfan wamepiga kambi uso na macho na waislam nje ya mji wa Madina. Na Banu
Quraidhah wanaangaza ndani na kujitayarisha nyuma ya waislamu. Vilevile
ndani ya Madina wanafiki na wale madhaifu wenye maradhi nyoyoni wameanza
kufichua siri zao na kusema; “Muhammad alikuwa daima akituahidi kumiliki hazina
za mfalme Kisra na Kaizari na sisi leo hakuna hata mmoja alie na dhamana ya
usalama wa nafsi yake au kwenda hata chooni kufanya haja yake".
Wakaanza
kutawanyika toka kwa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) kundi baada ya kundi,
kwa hoja ya woga na hofu kwa wake zao, watoto wao na nyumba zao dhidi ya
shambulizi linalotarajiwa toka Banu Quraidhah vita vitakapoanza. Na hawakubakia
pamoja na Mtume ila mamia machache ya waislam walio wakweli.
Katika
usiku mmoja wa mzunguko uliodumu siku ishirini, Mtume (Sallallahu ‘Alayhi
Wasallam) alielekeza uso kwa Mola wake na kumuomba du’aa ya mwenye shida na
kusema; “Ewe Mola nakuomba ile ahadi yako, ewe Mola nakuomba ile ahadi
yako".
Usiku
ule Nu’aim ibn Masoud alikuwa akihangaika mchagoni (kitandani) pake kama vile
mtu aliegongomelewa misumari. Macho kayafumbua usingizi umeruka. Akawa ni
mwenye kukodolea nyota zilizotanda kwenye mbingu zilizo safi kabisa huku
amezama ndani ya tafakuri. Ghafla akajikuta ni mwenye kujiuliza;
“Una
nini ewe Nu’aim?! Ni kitu gani kilichokuleta toka mbali huko Najd kuja kumpiga
vita mtu huyo na wenzake".
“Wewe
humpigi vita kwa kunusuru haki aliyoiiba au kulinda heshima iliyovunjwa bali
umekuja pasina sababu ijulikanayo".
"Inasihi
kwa mtu mwenye akili mithili yako kupigana ukauawa au kuuwa pasina
sababu?"
"Ewe
Nu’aim ni jambo gani linakupelekea kunyanyua upanga wako mbele ya uso wa mtu
huyu mwema, mwenye kuamrisha wafuasi wake uadilifu, na ihsani na kutendea wema
walio karibu?".
"Ni
kitu gani kinakufanya uchomoe mkuki wako ndani ya ala dhidi ya wafuasi wake
ambao amewalingania haki na uongofu?".
Hakumaliza
mazungumzo haya mazito na nafsi yake ila ni uamuzi wa mwisho kabisa
aliyoutekeleza hapo hapo.
Nu’aim
akanyemelea kutoka katika kambi yake chini ya kiza kizito, na kupiga hatua
kuelekea kwa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam). Mtume alipomuona mbele yake
alimwita;
“Nu’aim
ibn Masoud?”. Akasema;
“Ndio
ewe Mtume wa Allah”
"Kitu
gani kimekuleta saa hizi?”
“
Nimekuja kutamka shahada. Na wewe ni mja na mjumbe wa Allah na uliyokuja nayo
ni haki" Akaendelea: “Mimi nimesilimu ewe Mtume wa Allah na watu wangu
hawajui kusilimu kwangu. Niamrishe utakalo"
Mtume
(Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) akasema;
“Wewe
ni mmoja wetu. Hebu nenda kwa watu wako na ufanye hila utuepushe nao. Hakika
vita ni hadaa".
Akasema;
“Naam ewe Mtume wa Allah utaona yale yenye kukupendeza InshaAllah"
Akatoka
Nu’aim hapo hapo na kuelekea kwa Banu Quraidhah, kwani kabla alikuwa ni
marafiki na vipenzi wake. Akawaambia. “Enyi Banu Quraidhah, mnajuwa mapenzi na
urafiki wangu kwenu hivyo nimekuja kuwapa nasaha" Wakasema;
“Ndio
wewe kwetu siye mwenye tuhuma”.
Akasema;
"Hakika Makureshi na Ghatfan ni wenye nafasi kubwa kwenye vita hivi,
kinyume nanyi"
Wakasema;
“vipi”?
Akasema;
“Nyinyi hii ni nchi yenu mna mali zenu, watoto wenu na wake zenu. Hamna nafasi
ya kuhama kwenda kwengine. Ama Makureshi na Ghatfan, nchi yao, mali zao, watoto
wao na wake zao wako nje ya mji huu. Wamekuja kupigana na Muhammad na
wamekutakeni mvunje mikataba na muwaunge mkono mkakubali”.
“Wakifanikiwa
basi mmefanikiwa ama wakishindwa kumpiga vita wakirudi kwao, kwa salama
watakuacheni nyinyi na Muhammad nae atakulipizieni kisasi kibaya kabisa".
“Na
mnajua hamna uwezo kwake peke yenu".
Wakasema;
“ Umesema kweli sasa nini ushauri wako”?
Akasema;
“Ushauri wangu, ni kwamba msipigane nae mpaka, kundi la watu bora wao muwe nalo
kama rehani mikononi mwenu. Kwa hilo mtafanya wapigane na Muhammad mpaka
kushinda, au watu wote nyinyi nao mmalizike"
Wakasema;
“Umeelekeza na kutoa nasaha"
Nu’aim
akatoka na kumuelekea Abu Sufiyani ibn Harb, mkuu wa Makureshi akamwambia yeye
na walio nae;
“Enyi
makundi! Mnajua tosha mapenzi yangu kwenu na mnajua uadui wangu kwa Muhammad.
Lakini nimepata habari nimeona ni vyema na haki nikujuilisheni kama ni nasaha,
mzifiche na wala msizitangaze kuwa ni mimi niliekwambieni"
Wakasema;
"Umepata ahadi hiyo"
Akasema;
“Banu Quraidhah wanajutia juu ya uadui wao kwa Muhammad, na wamemtuma mjumbe
kumwambia. ‘Hakika sisi tunajuta juu ya matendo yetu na tumedhamiria kurudi
kwenye mkataba wetu na amani yetu’. ‘Je utaridhika tukikukabidhi watu bora na
wengi baina ya Makureshi na Ghatfan ili uwauwe, kisha tutajiunga nawe kuwapiga
vita?".
Akaendelea
kuwaambia; “Basi watakujieni Mayahudi wanataka kwenu rehani ya watu wenu
msiwape hata mtu mmoja".
Akasema
Abu Sufiyan; “Wewe ni rafiki mwema utalipwa kheri”
Kisha
akatoka Nu’aim kuelekea watu wake wa Ghatfan akawaambia kama yale aliyomwambia
Abu Sufiyan na akawahadharisha aliyomtahadharisha.
Abu
Sufiyan alitaka kuwajaribu Banu Quraidhah. Akamtuma mwanawe akasema; "Abu
Sufiyan anakusalimieni na anasema ‘muda umekuwa mwingi wa kumzunguka Muhammad
na watu wake na tushachoka. Nasi tumeazimia kupigana nae tumalizane nae’.
"Hivyo
baba yangu amenituma nikwambieni kwamba kesho tupambane".
Wakasema;
“Kesho ni Jumamosi na sisi hatufanyi kazi. Halafu sisi hatutapigana pamoja
nanyi hadi mtupatie watu wenu bora sabini pamoja na Ghatfan wawe ni rehani.
Sisi tuna wasiwasi vita vikipamba moto mtakimbilia kwenu haraka na kutuacha
peke yetu na Muhammad na mnajua sisi hatumuwezi Muhammad".
Aliporudi
mtoto wa Abu Sufiyan kwa jamaa zake akawapa habari kwa aliyoyasikia toka Banu
Quraidhah, wakasema kwa pamoja; “Waovu gani hawa wajukuu wa manyani na nguruwe,
Wallahi wangelitaka kondoo tu awe ni rehani tusingaliwapa”
Amefanikiwa
Nu’aim ibn Masoud kuvunja safu za Al-Ahzaab na kuuvunja umoja wao.
Allah
akawapelekea makureshi na washirika wao upepo mkali uliong'oa mahema na
kuangusha vyungu kwenye mafya. Moto ukazimika, nyuso zikamiminiwa mavumbi
hawakuwa na hila ila kuvunja kambi na kurudi makwao ndani ya kiza kizito.
Asubuhi
kuchomoza waislamu wanakuta maadui wameshaondoka. Wakawa wanasema;
“Alhamdulillahi alienusuru waja wake, akatukuza jeshi lake, akayashinda makundi
peke yake".
Akabakia
Nu’aim tangu siku ile ni mwenye kuaminiwa na Mtume (Sallallahu ‘Alayhi
Wasallam) akampa majukumu mbali mbali na akabeba mikononi mwake bendera (ya
jihadi). Ilipofika siku ya Fat-h (kuikomboa) Makkah, Abu Sufiyan alisimama na
kuangalia vikosi vya waislamu, alimuona Nu’aim akibeba bendera ya Ghatfan.
Akawauliza
walio nae; "Nani yule?”
Wakajibu;
“Nu’aim ibn Masoud”
Akasema; “Ametutendea uovu huyo siku ya Khandak.
Wallahi alikuwa ni mtu adui mkubwa wa Muhammad na huyu sasa anabeba bendera ya
Qaumu yake na anakuja kwa kutupiga vita chini ya bendera yake!?”.