Al-Mulk (67)

سُورَةُ  الْمُلْكُ
Al-Mulk (67)

(Imeteremka Makka)




Sura hii inaitwa Surat Al-Mulk kwa kutokana na neno Al-Mulk, yaani Ufalme,  linalo tokea katika Aya ya kwanza katika Sura. Na muhimu ya makusudio ya Sura hii tukufu ni kuelekeza fikra na nadhari zizingatie athari ya uweza wa Mwenyezi Mungu ulio zagaa katika nafsi za watu na katika viumbe vya Mwenyezi Mungu mnavyo viona katika ardhi na mbinguni upeo wa macho yenu, ili hayo yawe ndiyo njia ya kupelekea kumuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na pia Sura hii inabainisha hali ya makafiri ambao watatupwa katika Jahannamu, na watasikilizana mikoromo yao, na wataungua katika Moto wake, na wataungama madhambi yao, na watajuta kwa  watavyo ishia, watapo wauliza Malaika kwa kuto mwitikia Mtume alipo waita na akawahadharisha.
Na ama walio mkhofu Mola wao Mlezi, na wakamuamini, hao watapata maghfira na msamaha kwa makosa yaliyo waporonyoka, na ujira mkubwa kwa mema waliyo yatanguliza na wakayatenda.

 
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿١﴾

1. Amebarikika Ambaye Mkononi Mwake umo ufalme Naye juu ya kila kitu ni Qadiyr (Muweza).

الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْغَفُورُ ﴿٢﴾

2. Ambaye Ameumba mauti na uhai ili Akujaribuni ni nani kati yenu mwenye ‘amali nzuri zaidi. Naye ni Al- ‘Aziyzul-Ghafuwr (Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika daima - Mwingi wa kughufuria).

الَّذِي خَلَقَ سَبْعَ سَمَاوَاتٍ طِبَاقًا ۖ مَّا تَرَىٰ فِي خَلْقِ الرَّحْمَـٰنِ مِن تَفَاوُتٍ ۖ فَارْجِعِ الْبَصَرَ هَلْ تَرَىٰ مِن فُطُورٍ ﴿٣﴾

3. Ambaye Ameumba mbingu saba matabaka, hutaona katika uumbaji wa Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rahmah) tofauti yoyote. Basi rejesha jicho (mbinguni), je, unaona mpasuko wowote (ule)?

ثُمَّ ارْجِعِ الْبَصَرَ كَرَّتَيْنِ يَنقَلِبْ إِلَيْكَ الْبَصَرُ خَاسِئًا وَهُوَ حَسِيرٌ ﴿٤﴾

4. Kisha rejesha jicho mara ya pili (mara kwa mara), litakupindukia jicho likiwa limehizika na lenye kunyong’onyezwa.


وَلَقَدْ زَيَّنَّا السَّمَاءَ الدُّنْيَا بِمَصَابِيحَ وَجَعَلْنَاهَا رُجُومًا لِّلشَّيَاطِينِ ۖ وَأَعْتَدْنَا لَهُمْ عَذَابَ السَّعِيرِ ﴿٥﴾

5. Na kwa yakini Tumeipamba mbingu ya dunia kwa mataa, na Tukazijaalia kuwa ni kipigo kwa mashaytwaan, na Tumewaandalia adhabu ya (Moto wa) As-Sa’iyr (uwakao kwa nguvu).”

وَلِلَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ عَذَابُ جَهَنَّمَ ۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ ﴿٦﴾

6. Na kwa wale waliomkanusha Rabb (Mola) wao (imeandaliwa) adhabu ya (Moto wa) Jahannam, na pabaya paliyoje mahali pa kuishia mwishoni.

إِذَا أُلْقُوا فِيهَا سَمِعُوا لَهَا شَهِيقًا وَهِيَ تَفُورُ ﴿٧﴾

7. Watakapotupwa humo, watasikia (mngurumo mbaya wa) pumzi yake, nao unafoka.

تَكَادُ تَمَيَّزُ مِنَ الْغَيْظِ ۖ كُلَّمَا أُلْقِيَ فِيهَا فَوْجٌ سَأَلَهُمْ خَزَنَتُهَا أَلَمْ يَأْتِكُمْ نَذِيرٌ ﴿٨﴾

8. Unakaribia kupasuka kwa ghaidhi. Kila wanapotupwa humo kundi, walinzi wake (Malaika) watawauliza: “Je, hajakufikieni mwonyaji yeyote?”

قَالُوا بَلَىٰ قَدْ جَاءَنَا نَذِيرٌ فَكَذَّبْنَا وَقُلْنَا مَا نَزَّلَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ إِنْ أَنتُمْ إِلَّا فِي ضَلَالٍ كَبِيرٍ ﴿٩﴾

9. Watasema: Ndio! Kwa yakini alitujia mwonyaji, tukakadhibisha, na tukasema (kuwaambiwa waonyaji): “Allaah Hakuteremsha kitu chochote; nyinyi si chochote isipokuwa mumo katika upotofu mkubwa.”


وَقَالُوا لَوْ كُنَّا نَسْمَعُ أَوْ نَعْقِلُ مَا كُنَّا فِي أَصْحَابِ السَّعِيرِ ﴿١٠﴾

10. Na watasema: “Lau tungelikuwa tunasikilia (na kusikiliza) au tunatia akilini, tusingelikuwa miongoni mwa wakaazi wa (Moto wa) As-Sa’iyr (uwakao kwa nguvu).”

فَاعْتَرَفُوا بِذَنبِهِمْ فَسُحْقًا لِّأَصْحَابِ السَّعِيرِ ﴿١١﴾

11. Basi watakiri madhambi yao, na (itasemwa): “Tokomeeni wakaazi wa (Moto wa) As-Sa’iyr (uwakao kwa nguvu).”

إِنَّ الَّذِينَ يَخْشَوْنَ رَبَّهُم بِالْغَيْبِ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ كَبِيرٌ ﴿١٢﴾

12. Hakika wale wanaomuogopa Rabb (Mola) wao kwa ghayb (bila ya kumuona) watapata maghfirah na ujira mkubwa.

وَأَسِرُّوا قَوْلَكُمْ أَوِ اجْهَرُوا بِهِ ۖ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ ﴿١٣﴾

13. Na fanyeni siri kauli zenu, au zidhihirisheni, hakika Yeye ni ‘Aliym (Mjuzi) wa yaliyomo vifuani.

أَلَا يَعْلَمُ مَنْ خَلَقَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ ﴿١٤﴾

14. Kwani Hajui Yule Aliyeumba! Na hali Yeye ni Al-Latwiyful-Khabiyr (Mwenye kudabiri mambo kwa utuvu - Mjuzi wa vilivyodhahiri na vilivyofichikana).

هُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ ذَلُولًا فَامْشُوا فِي مَنَاكِبِهَا وَكُلُوا مِن رِّزْقِهِ ۖ وَإِلَيْهِ النُّشُورُ ﴿١٥﴾

15. Yeye Ndiye Aliyeijaaliya ardhi kuwa dhalili (kwa manufaa yenu), basi nendeni katika pande zake, na kuleni katika riziki Yake, na Kwake kufufuliwa.

أَأَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يَخْسِفَ بِكُمُ الْأَرْضَ فَإِذَا هِيَ تَمُورُ ﴿١٦﴾

16. Je, mnadhani mko (katika) amani na Aliyeko mbinguni (juu) kwamba Hatokudidimizeni ardhini, tahamaki hiyo inatikisika?

أَمْ أَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يُرْسِلَ عَلَيْكُمْ حَاصِبًا ۖ فَسَتَعْلَمُونَ كَيْفَ نَذِيرِ ﴿١٧﴾

17. Au mnadhani mko (katika) amani na Aliyeko mbinguni (juu) kwamba Hatokutumieni kimbunga (cha mawe), basi mtajua vipi (makali) maonyo Yangu.

وَلَقَدْ كَذَّبَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَكَيْفَ كَانَ نَكِيرِ ﴿١٨﴾

18. Na kwa yakini walikadhibisha wale walio kabla yao, basi vipi ilikuwa (kali) adhabu Yangu.

أَوَلَمْ يَرَوْا إِلَى الطَّيْرِ فَوْقَهُمْ صَافَّاتٍ وَيَقْبِضْنَ ۚ مَا يُمْسِكُهُنَّ إِلَّا الرَّحْمَـٰنُ ۚ إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ بَصِيرٌ ﴿١٩﴾

19. Je, hawawaoni ndege juu yao, wakiwa safusafu na wakikunja (mbawa zao), hakuna anayewashika (wasianguke) isipokuwa Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rahmah), hakika Yeye kwa kila kitu ni Baswiyr (Mwenye kuona).

أَمَّنْ هَـٰذَا الَّذِي هُوَ جُندٌ لَّكُمْ يَنصُرُكُم مِّن دُونِ الرَّحْمَـٰنِ ۚ إِنِ الْكَافِرُونَ إِلَّا فِي غُرُورٍ ﴿٢٠﴾

20. Au ni lipi hilo jeshi lenu linaloweza kukunusuruni badala ya Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rahmah)? Hawamo makafiri isipokuwa katika ghururi.

أَمَّنْ هَـٰذَا الَّذِي يَرْزُقُكُمْ إِنْ أَمْسَكَ رِزْقَهُ ۚ بَل لَّجُّوا فِي عُتُوٍّ وَنُفُورٍ ﴿٢١﴾

21. Au ni nani huyu ambaye (anaweza) kukuruzukuni ikiwa (Allaah) Atazuia riziki Yake? Bali wanang’ang’ania kwenye ujeuri na kukimbia mbali (na haki).

أَفَمَن يَمْشِي مُكِبًّا عَلَىٰ وَجْهِهِ أَهْدَىٰ أَمَّن يَمْشِي سَوِيًّا عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٢٢﴾

22. Je, yule anayekwenda akisinukia jua ya uso wake (akawa haoni; ndiye) ameongoka zaidi, au yule anayekwenda sawasawa kuelekea njia iliyonyooka?

قُلْ هُوَ الَّذِي أَنشَأَكُمْ وَجَعَلَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَالْأَفْئِدَةَ ۖ قَلِيلًا مَّا تَشْكُرُونَ ﴿٢٣﴾

23. Sema: “Yeye Ndiye Yule Aliyekuanzisheni na Akakujaalieni masikio, na macho, na nyoyo.” Ni kidogo sana mnayoshukuru.

قُلْ هُوَ الَّذِي ذَرَأَكُمْ فِي الْأَرْضِ وَإِلَيْهِ تُحْشَرُونَ ﴿٢٤﴾

24. Sema: “Yeye Ndiye Yule Aliyekutawanyeni kwenye ardhi, na Kwake mtakusanywa.”

وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا الْوَعْدُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٢٥﴾

25. Na (makafiri) wanasema: “Ni lini hiyo ahadi (ya Qiyaamah), mkiwa ni wasemao kweli?”

قُلْ إِنَّمَا الْعِلْمُ عِندَ اللَّـهِ وَإِنَّمَا أَنَا نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٢٦﴾

26. Sema: “Hakika ujuzi (wake) uko kwa Allaah; na hakika mimi ni mwonyaji (tu) bayana.”

فَلَمَّا رَأَوْهُ زُلْفَةً سِيئَتْ وُجُوهُ الَّذِينَ كَفَرُوا وَقِيلَ هَـٰذَا الَّذِي كُنتُم بِهِ تَدَّعُونَ ﴿٢٧﴾

27. Basi watakapoiona (adhabu ya Qiyaamah) inakaribia, zitadhikika nyuso za wale waliokufuru, na itasemwa: “Hii ndio (ile ahadi) mliyokuwa mkiiomba.”

قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ أَهْلَكَنِيَ اللَّـهُ وَمَن مَّعِيَ أَوْ رَحِمَنَا فَمَن يُجِيرُ الْكَافِرِينَ مِنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٢٨﴾

28. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Je, mnaonaje ikiwa Allaah Ataniangamiza na walio pamoja nami, au Akiturehemu; basi ni nani atakayewakinga makafiri na adhabu iumizayo?”

قُلْ هُوَ الرَّحْمَـٰنُ آمَنَّا بِهِ وَعَلَيْهِ تَوَكَّلْنَا ۖ فَسَتَعْلَمُونَ مَنْ هُوَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٢٩﴾

29. Sema: “Yeye Ndiye Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rahmah) tumemwamini, na Kwake tunatawakali, basi karibuni hivi mtakuja kujua ni nani ambaye yumo katika upotofu wa bayana.”

قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِنْ أَصْبَحَ مَاؤُكُمْ غَوْرًا فَمَن يَأْتِيكُم بِمَاءٍ مَّعِينٍ ﴿٣٠﴾

30. Sema: “Mnaonaje yakijakuwa maji yenu yamedidimia; basi ni nani atakayeweza kukuleteeni (chemchemu za) maji yatiririkayo?”





Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejeauliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii falhaqqiy@gmail.com