009 - Hadiyth Ya 9: Neema Mbili Watu Wengi Wameghilibika Nazo; Siha Na Faragha

009 - Hadiyth Ya 9: Neema Mbili Watu Wengi Wameghilibika Nazo; Siha Na Faragha



عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ (صلى الله عليه و آله وسلم): ((نِعْمَتَانِ مَغْبُونٌ فِيهِمَا كَثِيرٌ مِنْ النَّاسِ: الصِّحَّةُ وَالْفَرَاغُ))  رواه  البخاري
Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amesema: Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Watu wengi wameghilibika katika neema mbili; siha na faragha [wasaa])).[1]
 
Mafunzo Na Hidaaya:
 
  1. Kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) hata wakati wa faragha.
 
 فَإِذَا فَرَغْتَ فَانصَبْ . وَإِلَىٰ رَبِّكَ فَارْغَب
Na kwa Mola wako elemeza raghba (zako, niyyah zako, du’aa, matarajio nk)[2]
 
  1. Siha na faragha yaani kuwa na wasaa (nafasi) ni raasilmali ya mtu, basi atakayetumia raasilmali yake vyema atapata faida, na atakayeipoteza atakhasirika na kujuta.
 
  1. Umuhimu wa kunufaika kwa siha na faragha kabla ya kutoweka kwake, kwa kujikurubisha kwa Allaah (سبحانه وتعالى) na kujitendea ‘amali njema. [Hadiyth: ((Nufaika kwa mambo matano kabla ya matano; ujana wako kabla ya uzee wako, siha yako kabla ya maradhi yako, mali yako kabla ya ufukara wako, wakati wako wa faragha kabla ya kushughulishwa kwako, na uhai wako kabla ya mauti yako))].[3]
 
  1. Watu wengi hawathamini neema mbili hizi, wale wanaopoteza muda wao kwa mambo yasiyokuwa na faida nao kwa Aakhirah, na wanaharibu miili yao na hali Uislamu umesisitiza kuchunga wakati na viwiliwili.
 
  1. Muumin atumie wakati wake wote kwa kutenda mema na kwa ajili ya Allaah (سبحانه وتعالى) ili ajiepushe na upuuzi na aweze kupata sifa miongoni mwa sifa za Waumini watakaopata Pepo ya Al-Firdaws [Al-Muuminuun 23: 1-11].
 
  1. Kutotumia neema alizopatiwa na Allaah (سبحانه وتعالى) ni kukhasirika kwa mja duniani na Aakhirah. [Al-‘Aswr 103: 1-2].
 
 



[1]  Al-Bukhaariy.
[2]  Ash-Sharh (94: 7-8).
[3]  Al-Haakim, Al-Bayhaqiy Ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ 1077.