Rabiah ibn Ka'ab- mwambata wa Mtume Muhammad (SAW)
Hiki ni kisa cha Rabiah kama
mwenyewe anavyosimulia.
“Nilikuwa bado ndogo pale nuru ya
imani iliponimulika na moyo wangu kufunguka na mafundisho ya dini ya kiislam na
pale macho yangu yalipomuona mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwa mara ya kwanza.
Nilimpenda pendo lisilokuwa na mfano. Nilimpenda kuliko mtu mwengine
yoyote. Siku moja nikajisemea mwenyewe moyoni:
“Ole wako Rabiah, kwanini hujitolei
nafsi yako kumhudumia Mtume (SAW). Nenda na mtake shauri kwa hili.
Ikiwa ataridhika na wewe, utaona raha kuwa karibu naye, utakuwa na mafanikio
kupitia mapenzi yako kwake na utakuwa na bahati nzuri ya kupata mambo mema hapa
duniani na mema huko akhera.”
Nikafanya kama nafsi yangu
ilivyoniagiza. Mtume (SAW) hakunivunja moyo na alifurahi sana.
Tokea siku hiyo nikaanza kuishi chini ya kivuli cha Al-Habib Mustafa.
Niliongozana naye kila anapokwenda na kila anapogeuza uso wake na kunitazama,
basi huruka haraka na kuwa mbele yake. Akitaja tu shida yake, hunikuta
tayari nimeshaanza kuitimiza.
Nitamshughulikia mchana na usiku
unapoingia, na Mtume (SAW) kumaliza kusali sala ya Isha na kurudi nyumbani
kwake, hufikiria kuondoka, lakini papo hapo hujisema moyoni:
“Wapi utakwenda Rabiah? Labda
utaweza kuhitajika kumfanyia jambo Mtume (SAW) usiku. Hivyo hubakia
mlangoni kwake. Mtume (SAW) huutumia baadhi ya usiku kwa
kusali. Humsikia akisoma suratul Fatiha na huendelea kusoma nusu ya thuluthi
ya usiku. Mimi huchoka na kuondoka au macho yangu kuchoka na kulala.
Ilikuwa ni tabia ya Mtume (SAW),
ikiwa mtu atamtendea jambo loloate zuri basi na yeye humrudishia mara mbili
yake. Alitaka kunifanya na mimi pia kwa jinsi nilivyokuwa nikimhudumia.
Siku moja akanijia na kuniambia:
“Ewe Rabiah ibn Kaab!
Nikamuitika, “Labbayka yaa
Rasulullah.”
“Niombe kitu chochote utakacho
na nitakupa.”
Nikafikiri kidogo kisha nikamwambia
Mtume (SAW):
“Nipe muda kidogo, ewe mjumbe wa
Mwenyezi Mungu, kufikiria hicho ninachokitaka halafu nitakujulisha.”
Kipindi hicyo nilikuwa bado kijana
na maskini. Sikuwa na aila wala utajiri na hata sikuwa na pahala pangu
mwenyewe. Nilikuwa nikilala msikitini kama walivyokuwa waislam wengine
maskini kama mimi. Watu walikuwa wanatutania ‘wageni wa uislam’.
Endapo muislam yoyote akileta sadaqa kwa Mtume (SAW) hutuletea sisi yote.
Na kama akipewa zawadi huchukua kidogo na iliyobaki pia kutuletea sisi.
Ikamjia nimuombe Mtume (SAW) jambo
zuri la kidunia ambalo lingeniepusha na ufukara na kuwa kama wale wenye
utajiri, wake na watoto. Hapo hapo nikajisuta:
“Angamia wee Rabiah, dunia hii ni ya
muda tu, una rizki yako ambayo tayari Mwenyezi Mungu amekuandikia na
utaipata. Mtume (SAW) anayo sehemu maalum kwa mola wake na ombi lake
halikataliwi. Kwa hivyo muombe Mtume (SAW) amuombe Mwenyezi Mungu akupe
jambo la kheri na wewe akhera!”
Nikajihisi kuwa na furaha na wao
hili na nikaenda kwa Mtume (SAW) na akaniuliza:
“Unasemaje Rabiah?”
Nikamjibu, “ewe mjumbe wa Mwenyezi
Mungu, ninakuomba uniombee kwa mola kwa niaba yangu niwe mwenzako peponi.”
Mtume akauniuliza,
“ni nani aliyekupa wazo hili?”
“Hakuna mtu yoyote aliyenipa
wazo. Lakini pale uliponiambia niombe chochote na nitakupa, nikafikiri
kukuomba khayraat za kidunia. Baada ya muda tu nikaongozwa kuchagua kitu
cha kidunia na milele kuliko kitu cha kupita na kumalizika ndo maana nikaomba
hilo.”
Mtume Muhammad (SAW) akanyamaza kwa
muda kisha akasema:
“Huna ombi jengine zaidi ya
hilo Rabiah?”
Nikamjibu, “sina, mjumbe wa Mwenyezi
Mungu hakuna chengine kitakachoweza kufanana na nililoliomba.”
“Ikiwa ni hivyo, basi nisaidie kwa
minajili yako kwa kuzidisha sijda kwa Mwenyezi Mungu (SW),” akasema Mtume
(SAW).
Hivyo nikazidisha juhudi katika
kufanya ibada ili kupata bahati ya kuwa pamoja na Mtume (SAW) peponi.
Nilivyopata bahati ya kuwa mtumishi na sahaba wake hapa duniani.
Haikupita muda Mtume (SAW) akaniita
na kuniuliza:
“Hutaki kuoa Rabiah?”
“Sitaki kitu chochote
kitakachonishughulisha katika kukuhudumia.” Nikamjibu.
“Halikadhalika sina chochote cha
kutoa mahari na wala pahala pa kukaa na mke.”
Mtume (SAW) akatulia kimya hakusema
kitu siku hiyo. Aliponiona tena siku nyengine akaniuliza tena suala la
kuoa na jibu likawa lile lile.
Nilipokuwa peke yangu na kufikiria
zaidi nikajuta kauli yangu ile na kujilaumu mwenyewe;
“Ole wako Rabiah, Mtume (SAW)
anafahamu zaidi yako kujua lipi zuri kwako hapa duniani na huko akhera na
anajua zaidi yako nini ulichonacho. Basi ikiwa Mtume (SAW) ataniuliza
tena kuhusu kuoa, nitamjibu nipo tayari.
Haukupita muda, Mtume (SAW)
akaniuliza tena:
“Hutaki kuoa Rabiah?”
“Ninataka, ewe mjumbe wa Mwenyezi
Mungu,” nikamjibu. “Lakini nani atakuwa tayari kuolewa na mimi hasa
katika hali hii ambayo unaijua? Nikamuuliza.
Mtume (SAW) akasema,
“nenda kwa familia ya
fulani na uwaambie: Mtume (SAW) ameagiza nije kuposa kwenu.”
“Kwa unyonge nikaenda na kusema kama
nilivyoambiwa na Mtume Muhammad (SAW). Wakashangaa na kusema, “mtoto
wetu! ?”
Nikawajibu, “ndio mtoto wenu.”
“Karibu Mtume wa Mwenyezi Mungu,
karibu mjumbe wake, mjumbe wa Mtume wa Mwenyezi Mungu atarudi huku amefanikiwa
lengo lake. Wakatufungisha ndoa. Nikarudi kwa Mtume (SAW) kumpa
habari njema.
“Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu,
nimekuja kutoka nyumba iliyobora kabisa. Waliniamini (maneno yangu),
wakanikaribisha na kunifungisha ndoa na binti yao. Lakini wapi nitapata
mahari ya kumpa mke wangu?”
Mtume (SAW) akaagiza kuitwa
Buraydah ibn Al-Khasib mmoja katika wakubwa wa kabila langu Banu Asiam na
kumwambia, “ewe Burayadah kusanya kiasi fulani cha dhahabu kwa ajili ya
Rabiah.”
Zikakusanywa na kuletwa kwa Mtume
(SAW) na kuniambia:
“Chukua hizi wapelekee na
uwaambie hii ni mahari ya binti yenu.”
Nikapeleka yakapokelewa kwa mikono
miwili na walifurahi sana na kusema, ni nyingi na nzuri. Nilirudi kwa
Mtume Muhammad (SAW) na kumhadithia:
“Sijawahi kuona watu wakarimu kama
wale. Wamependezewa sana na kile nilichowapa ijapokuwa ni kichache……,
sasa nitapata wapi chakula cha walima, ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu?”
Mtume (SAW) akamwambia
Buraydah “kusanya kiasi cha fedha thamani ya kondoo kwa ajili ya
Rabiah!”
Wakanunua kondoo aliyenona na kisha
Mtume (SAW) akaniambia:
“Nenda kwa Bi Aisha na
umwambie akupe kiasi chochote cha ‘mawele’ alichonacho.”
Bi Aisha akanipa pishi saba na
kusema, “Wallahi hatuna tena chakula!:
Nikatoka na kuelekea nyumban
ya familia ya mke wangu na wakaniambia:
“Sisi tutayatengeneza haya mawele
lakini tafuta marafiki zako mumtengeneze huyu kondoo.”
Tukamchinja, kumchuna ngozi na
kumpika. Hivyo tukala mkate na nyama na nikamualika Mtume (SAW) na
akahudhuria.
Mtume Muhammad (SAW) akampa kipande
cha ardhi jirani na Abubakar. Kuanzia hapo tena nikaanza kujishughulisha
na dunia. Nikawa na ugomvi kati yangu na Abubakar juu ya mtende.
“Uko ndani ya mpaka wangu” nikadai.
“Uko kwangu” akajibu Abubakar.
Tukaanza kubishana, Abubakar
akanitukana, lakini ghafla tu akajirudi nafsi yake na kuniomba msamaha na
kuniambia, “Rabiah, tamka kama nilivyotamka mimi ili kihisabike kama kisasi.
“Hapana, sitofanya hivyo.” Nikamjibu.
“Ikiwa ni hivyo, nitakwenda
kukushitakia kwa mjumbe wa Mwenyezi Mungu kukataa kwako kulipiza kisasi.”
Alikwenda na nilimfuata. Jamaa
wa kabila langu pia likafuata:
“Yeye ndiye aliyeanza kwa kukutukana
halafu anakwenda kwa Mtume (SAW) kukushtakia?”
Nikawageukia na kuwaambia, “Ole
wenu, mnajua ni nani huyu? Ni Assiddiq……. Na ni mtu mzima anaeheshimika
miongoni mwa waislam. Rudini kabla hajatizama nyuma na kukuoneni na
kufikiria labda umekuja kunisaidia dhidi yake, kwani atazidi kukasirika na
kwenda kwa Mtume (SAW) na ghadhabu. Mtume naye atakasirika kasha Mwenyezi
Mungu atakasirika wote na Rabiah kumalizika! Wakarudi.”
Abubakar akamhadithia Mtume (SAW)
kama ilivyotokea na Mtume alipomaliza kumsikiliza akainua kichwa chake na
kuniambia:
“Ewe Rabiah, mna matatizo gani
wewe na Assiddiq?”
“Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alinitaka
niseme maneno yale yale kama alivyonitamkia na mini nikakataa.”
“Ndio, usiseme maneno yale
kama alivyokutamkia, badala yake sema, ‘Inshallah Mwenyezi Mungu amsamehe
Abubakar.”
Abubakar akaondoka huku akitokwa na machozi huku
akisema, “Inshaallah Mwenyezi Mungu akulipe mema kwa sababu yangu ewe Rabiah
ibn Kaab……..”