018 - Hadiyth Ya 18: Alama Za Mnafiki Ni Tatu: Uongo, Kutokutimiza Ahadi, Kufanya Khiyana


عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم): ((آيَةُ الْمُنَافِقِ ثلاَثٌ إِذَا حَدَّثَ كَذَبَ وَإِذَا وَعَدَ أَخْلَفَ وَإِذَا اؤْتُمِنَ خَانَ)) متفق عليه . وفي رواية: ((وَإِنْ صَامَ وَصَلَّى وَزَعَمَ أَنَّهُ مُسْلِمٌ)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (رضي الله عنه)  kwamba Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Alama za mnafiki ni tatu: anapozungumza husema uongo, anapotoa ahadi hukhalifu (hatimizi), na anapoaminiwa hufanya khiyana))[1]. Na katika riwaaya nyingine: ((Hata akifunga na akiswali na akidai kuwa yeye ni Muislamu))[2]
 
Mafunzo Na Hidaaya:
 
  1. Unafiki ni miongoni mwa maradhi ya moyo ya hatari yanayokemewa sana katika Uislamu. [Al-Maaidah 5: 52, Al-Anfaal 8: 49, Al-Hajj 22: 53].
 
  1. Sifa tatu hizo ni sifa mashuhuri miongoni mwa sifa za wanafiki. [An-Nisaa 4: 143, Al-Baqarah 2: 8-15] Lakini hizo sio zote zinazowahusu, bali wanazo sifa mbaya zaidi ya hizo. 
 
  1. Mwenye kuwa na sifa zote tatu hizo ajitambue kuwa ni mnafiki.
 
  1. Kukimbilia kujirekebisha pindi Muislamu anapotambua kuwa ana sifa mojawapo kabla ya kumiliki sifa zote tatu.
 
  1. Uislamu unafunza sifa njema za ukweli, kutimiza ahadi na uaminifu. [An-Nisaa 4: 58, An-Nahl 16: 91]. Nazo ni miongoni mwa sifa za watakaopata Pepo ya Al-Firdaws [Al-Muuminuwn 23: 8]. Na pia:
وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ
Na ambao amana zao na ahadi zao wanazichunga (kuzitimiza)[3]
 
  1. Mtu anaweza kudhaniya kuwa ni Muislamu wa kweli kwa sababu ya utekelezaji wake wa ‘Ibaadah, kumbe ni mnafiki.
 


[1]  Al-Bukhaariy na Muslim.
[2]  Al-Bukhaariy na Muslim.
[3]  Al-Ma’aarij (70: 32)