Al-Qalam (68)

سُورَةُ  الْقَلَم
Al-Qalam (68)

(Imeteremka Makka)




Sura hii tukufu imekusanya kumtetea Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. na kuipelekea hima yake na azma yake hata abakie mwenye kushikilia Haki bila ya kumlegezea yeyote, na kushabihisha adhabu iliyo wapata watu wa Makka na adhabu iliyo wapata watu wenye shamba ambao kisa chao kimesimuliwa katika Sura. Na Waumini wanabashiriwa watayo yapata kutoka kwa Mola wao Mlezi; na hapana usawa baina yao na makafiri.  Wanao kadhibisha wanakanywa madai yao wanao jidaia nafsi zao bila ya haki, na wanatiwa khofu kwa kuelezwa hali yao itakavyo kuwa Akhera, na wanatishwa. Na Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w. ananasihiwa asubiri na astahamili. Mwishoe Sura inakhitimisha kwa kuitukuza Qur'ani tukufu.


 
بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

ن ۚ وَالْقَلَمِ وَمَا يَسْطُرُونَ ﴿١﴾

1. Nuwn. Naapa kwa kalamu na yale wayaandikayo.


مَا أَنتَ بِنِعْمَةِ رَبِّكَ بِمَجْنُونٍ ﴿٢﴾

2. Kwa neema ya Rabb (Mola) wako, wewe (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) si majnuni.

وَإِنَّ لَكَ لَأَجْرًا غَيْرَ مَمْنُونٍ ﴿٣﴾

3. Na hakika wewe bila shaka una ujira usiokatika.

وَإِنَّكَ لَعَلَىٰ خُلُقٍ عَظِيمٍ ﴿٤﴾

4. Na hakika wewe bila shaka una tabia nzuri mno.


فَسَتُبْصِرُ وَيُبْصِرُونَ ﴿٥﴾

5. Basi hivi karibuni utaona, na wao wataona.


بِأَييِّكُمُ الْمَفْتُونُ ﴿٦﴾

6. Ni nani kati yenu aliyesibiwa (na uwendawazimu).

إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ ﴿٧﴾

7. Hakika Rabb (Mola) wako Yeye Anamjua zaidi aliyepotea njia Yake, Naye Anawajua zaidi walioongoka.

فَلَا تُطِعِ الْمُكَذِّبِينَ ﴿٨﴾

8. Basi usiwatii wanaokadhibisha.

وَدُّوا لَوْ تُدْهِنُ فَيُدْهِنُونَ ﴿٩﴾

9. Wanatamani lau kama ungelilainisha, nao pia walainishe.

وَلَا تُطِعْ كُلَّ حَلَّافٍ مَّهِينٍ ﴿١٠﴾

10. Na wala usimtii kila mwingi wa kuapa, dhalili.

هَمَّازٍ مَّشَّاءٍ بِنَمِيمٍ ﴿١١﴾

11. Mzushi, mwenye kutembea kwa kufitinisha.

مَّنَّاعٍ لِّلْخَيْرِ مُعْتَدٍ أَثِيمٍ ﴿١٢﴾

12. Mzuiaji (mambo ya) kheri, anayevuka mipaka, mwingi wa dhambi.

عُتُلٍّ بَعْدَ ذَٰلِكَ زَنِيمٍ ﴿١٣﴾

13. Katili, (na) baada ya hivyo ni mwenye kujipachika tu (hakuzaliwa kwenye ndoa).

أَن كَانَ ذَا مَالٍ وَبَنِينَ ﴿١٤﴾

14. Kwa kuwa (anajiona) ana mali na watoto?

إِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِ آيَاتُنَا قَالَ أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ ﴿١٥﴾

15. Anaposomewa Aayaat Zetu, anasema: “Hekaya za (watu) wa kale.”

سَنَسِمُهُ عَلَى الْخُرْطُومِ ﴿١٦﴾

16. Tutamtia chapa juu pua yake.

إِنَّا بَلَوْنَاهُمْ كَمَا بَلَوْنَا أَصْحَابَ الْجَنَّةِ إِذْ أَقْسَمُوا لَيَصْرِمُنَّهَا مُصْبِحِينَ ﴿١٧﴾

17. Hakika sisi Tumewajaribu (Maquraysh) kama Tulivyowajaribu watu wa bustani, pale walipoapa kuwa bila shaka watayavuna (mazao yake) watakapopambaukiwa.

وَلَا يَسْتَثْنُونَ ﴿١٨﴾

18. Na wala hawakusema: “In-shaa-Allaah (Allaah Akipenda).”

فَطَافَ عَلَيْهَا طَائِفٌ مِّن رَّبِّكَ وَهُمْ نَائِمُونَ ﴿١٩﴾

19. Basi (shamba lao) ikazungukwa na twaaifun (balaa kubwa ya moto usioeleweka ulianzaje) kutoka kwa Rabb (Mola) wako na hali wao wamelala.

فَأَصْبَحَتْ كَالصَّرِيمِ ﴿٢٠﴾

20. (Shamba) Likawa kama iliyovunwa (ikabakishwa majivu meusi kwa namna ilivoteketea).

فَتَنَادَوْا مُصْبِحِينَ ﴿٢١﴾

21. Wakaitana, walipopambaukiwa.


أَنِ اغْدُوا عَلَىٰ حَرْثِكُمْ إِن كُنتُمْ صَارِمِينَ ﴿٢٢﴾

22. Kwamba nendeni asubuhi mapema kondeni kwenu, mkiwa mnataka kuvuna.

فَانطَلَقُوا وَهُمْ يَتَخَافَتُونَ ﴿٢٣﴾

23. Wakatoka na huku wananong’onezana.

أَن لَّا يَدْخُلَنَّهَا الْيَوْمَ عَلَيْكُم مِّسْكِينٌ ﴿٢٤﴾

24. Kwamba: “Asikuingilieni humo leo masikini yeyote yule.”

وَغَدَوْا عَلَىٰ حَرْدٍ قَادِرِينَ ﴿٢٥﴾

25. Wakatoka asubuhi mapema na azimio, wakidhani wana uwezo (wa kuwazuia maskini).

فَلَمَّا رَأَوْهَا قَالُوا إِنَّا لَضَالُّونَ ﴿٢٦﴾

26. Basi walipoliona (lile shamba lao lilivyoteketea), wakasema: “Hakika sisi bila shaka Tumepotea.”

بَلْ نَحْنُ مَحْرُومُونَ ﴿٢٧﴾

27. (Walivyotanabahi wakasema): “Bali sisi tumeharamishwa (mavuno yake),”

قَالَ أَوْسَطُهُمْ أَلَمْ أَقُل لَّكُمْ لَوْلَا تُسَبِّحُونَ ﴿٢٨﴾

28. Wa wastani wao akasema: “Je, sikukuambieni kwanini hamumsabbih (Allaah?)”

قَالُوا سُبْحَانَ رَبِّنَا إِنَّا كُنَّا ظَالِمِينَ ﴿٢٩﴾

29. Wakasema: “Subhaana Rabbinnaa (Ametakasika Mola wetu!) Hakika Sisi tulikuwa madhalimu.”

فَأَقْبَلَ بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ يَتَلَاوَمُونَ ﴿٣٠﴾
30. Wakakabiliana wenyewe kwa wenyewe wakilaumiana.

قَالُوا يَا وَيْلَنَا إِنَّا كُنَّا طَاغِينَ ﴿٣١﴾

31. Wakasema: “Ole wetu! Hakika sisi tumekuwa warukao mipaka.”

عَسَىٰ رَبُّنَا أَن يُبْدِلَنَا خَيْرًا مِّنْهَا إِنَّا إِلَىٰ رَبِّنَا رَاغِبُونَ ﴿٣٢﴾

32. “Huenda Rabb (Mola) wetu Akatubadilishia lililo bora kuliko hilo (shamba letu), hakika sisi tunaelemea kwa Rabb wetu.”

كَذَٰلِكَ الْعَذَابُ ۖ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَكْبَرُ ۚ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿٣٣﴾

33. Hivyo ndivyo adhabu (ya dunia inavyokuwa), na bila shaka adhabu ya Aakhirah ni kubwa zaidi lau wangelikuwa wanaelewa.

إِنَّ لِلْمُتَّقِينَ عِندَ رَبِّهِمْ جَنَّاتِ النَّعِيمِ ﴿٣٤﴾

34. Hakika wenye taqwa watapata kwa Rabb (Mola) wao Jannaat za Na’iym.   

أَفَنَجْعَلُ الْمُسْلِمِينَ كَالْمُجْرِمِينَ ﴿٣٥﴾

35. Je, Tuwajaalie Waislamu kama wahalifu?

مَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ ﴿٣٦﴾

36. Mna nini! Vipi mnahukumu?

أَمْ لَكُمْ كِتَابٌ فِيهِ تَدْرُسُونَ ﴿٣٧﴾

37. Au mna kitabu chochote (kile) mkisomacho humo?

إِنَّ لَكُمْ فِيهِ لَمَا تَخَيَّرُونَ ﴿٣٨﴾

38. Kwamba mtapata humo mnachopendelea?

أَمْ لَكُمْ أَيْمَانٌ عَلَيْنَا بَالِغَةٌ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ ۙ إِنَّ لَكُمْ لَمَا تَحْكُمُونَ ﴿٣٩﴾

39. Au mnazo ahadi za viapo juu Yetu zinazofikia mpaka Siku ya Qiyaamah, kwamba mtapata mnayojihukumia?

سَلْهُمْ أَيُّهُم بِذَٰلِكَ زَعِيمٌ ﴿٤٠﴾

40. Waulize (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Ni nani kati yao mdhamini ya hayo?”

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ فَلْيَأْتُوا بِشُرَكَائِهِمْ إِن كَانُوا صَادِقِينَ ﴿٤١﴾

41. Au wana washirika? Basi wawalete washirika wao wakiwa wasema kweli.

يَوْمَ يُكْشَفُ عَن سَاقٍ وَيُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ فَلَا يَسْتَطِيعُونَ ﴿٤٢﴾

42. Siku utakapofunuliwa muundi na wataitwa kusujudu lakini hawatoweza.

خَاشِعَةً أَبْصَارُهُمْ تَرْهَقُهُمْ ذِلَّةٌ ۖ وَقَدْ كَانُوا يُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ وَهُمْ سَالِمُونَ ﴿٤٣﴾

43. Macho yao yatanyenyekea (kwa khofu) udhalilifu utawafunika. Na kwa yakini walikuwa wakiitwa wasujudu (kuswali duniani) walipokuwa salama (lakini hawakuitikia wito).

فَذَرْنِي وَمَن يُكَذِّبُ بِهَـٰذَا الْحَدِيثِ ۖ سَنَسْتَدْرِجُهُم مِّنْ حَيْثُ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٤٤﴾

44. Basi Niache (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) na anayekadhibisha al-hadiyth hii (Qur-aan); Tutawavuta pole pole kwa namna wasiyoijua.

وَأُمْلِي لَهُمْ ۚ إِنَّ كَيْدِي مَتِينٌ ﴿٤٥﴾

45. Na Ninawapa muhula (wa kungojeshwa adhabu), hakika mpango Wangu ni thabiti.

أَمْ تَسْأَلُهُمْ أَجْرًا فَهُم مِّن مَّغْرَمٍ مُّثْقَلُونَ ﴿٤٦﴾

46. Au unawaomba ujira (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), basi wao wamekuwa wazito kwa gharama zake?

أَمْ عِندَهُمُ الْغَيْبُ فَهُمْ يَكْتُبُونَ ﴿٤٧﴾

47. Au wanayo (elimu ya) ghayb, basi wao wanayaandika?

فَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ وَلَا تَكُن كَصَاحِبِ الْحُوتِ إِذْ نَادَىٰ وَهُوَ مَكْظُومٌ ﴿٤٨﴾

48. Basi subiri (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwa hukumu ya Rabb (Mola) wako, na wala usiwe kama swahibu wa samaki (Nabii Yuwnus) pale aliponadi (kutuomba) naye akiwa amebanwa na dhiki.

لَّوْلَا أَن تَدَارَكَهُ نِعْمَةٌ مِّن رَّبِّهِ لَنُبِذَ بِالْعَرَاءِ وَهُوَ مَذْمُومٌ ﴿٤٩﴾

49. Lau isingelimfikia neema kutoka Rabb (Mola) wake, bila shaka angelitupwa ufukoni hali akiwa mwenye kulaumiwa.


فَاجْتَبَاهُ رَبُّهُ فَجَعَلَهُ مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿٥٠﴾

50. (Lakini) Rabb (Mola) wake Amemchagua na akamjaalia (kuwa) miongoni mwa (waja) wema.

وَإِن يَكَادُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَيُزْلِقُونَكَ بِأَبْصَارِهِمْ لَمَّا سَمِعُوا الذِّكْرَ وَيَقُولُونَ إِنَّهُ لَمَجْنُونٌ ﴿٥١﴾

51. Na wale waliokufuru hukaribia kukutelezesha kwa macho yao wanaposikia dhikri (Qur-aan) na wanasema: “Hakika yeye bila shaka ni majnuni.”

وَمَا هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ لِّلْعَالَمِينَ ﴿٥٢﴾

52. Na haikuwa (hii Qur-aan) isipokuwa ni dhikri (ukumbusho, mawaidha na kumbukumbu) kwa walimwengu.





Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejeauliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii falhaqqiy@gmail.com