Al-Ghaashiyah (88)


سُورَةُ الْغَاشِيَة
Al-Ghaashiyah (88)

(Imeteremka Makka)

 
Imeanza Sura hii kwa njia ya kutia shauku kuisikiliza hadithi ya Siku ya Kiyama, na hayo mambo yatakayo tokea humo. Inaashiria kwamba watu ni makundi mawili: miongoni mwao wapo ambao hawatapata hishima yoyote kwa watakavyo pokewa na wataingia kwenye Moto mkali. Na wapo watakao ifikia siku hiyo kwa furaha kwa namna ya rehema na radhi zilizo andaliwa kwa ajili yao. Kisha Sura ikaeleza dalili zilizo wazi za uweza wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kufufua kutokana na wanavyo ona wenyewe kwa macho yao na wanayo nafiika kwayo katika uhai wao. Na baada ya kuzitaja dalili hizi ikageukia khabari za Mtume s.a.w. kwa kukumbusha kwamba waajibu wake mkubwa kwa mintarafu yao ni wazi, ya kwamba yeye hakutawalishwa juu yao awalazimishe kuamini, na kwamba mwenye kugeuka na akakufuru baada ya waadhi huu ni Mwenyezi Mungu ndiye atakaye mshika kwa dhambi zake, na atamuadhibu kwa adhabu kubwa kabisa, atapo rejea kwake baada ya kufa, kwani marejeo ya wote na kuhisabiwa kwao wote ni kwake Yeye Mwenyezi Mungu.


بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ الْغَاشِيَةِ ﴿١﴾

1. Je, imekujia hadiyth ya kufunikiza?

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ خَاشِعَةٌ ﴿٢﴾

2. (Baadhi ya) Nyuso siku hiyo zitanyenyekea.

عَامِلَةٌ نَّاصِبَةٌ ﴿٣﴾

3. Zenye kufanya kazi ngumu na kuchoka.

تَصْلَىٰ نَارًا حَامِيَةً ﴿٤﴾

4. Zitaingia na kuungua (kwenye) Moto mkali (uwakao) kabisa.

تُسْقَىٰ مِنْ عَيْنٍ آنِيَةٍ ﴿٥﴾

5. Zitanyweshwa katika chemchemu ichemkayo.

لَّيْسَ لَهُمْ طَعَامٌ إِلَّا مِن ضَرِيعٍ ﴿٦﴾

6. Hawatokuwa na chakula isipokuwa kutokana na mti wa sumu wenye miba.

لَّا يُسْمِنُ وَلَا يُغْنِي مِن جُوعٍ ﴿٧﴾

7. Hakinenepeshi, na wala haitoshelezi (kuondosha) njaa.

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاعِمَةٌ ﴿٨﴾

8. (Baadhi ya) Nyuso siku hiyo zitakuwa zenye bashasha.


لِّسَعْيِهَا رَاضِيَةٌ ﴿٩﴾

9. Zitakuwa radhi kwa juhudi zao.

فِي جَنَّةٍ عَالِيَةٍ ﴿١٠﴾

10. Kwenye Jannah ya juu.

لَّا تَسْمَعُ فِيهَا لَاغِيَةً ﴿١١﴾
11. Hazitosikia humo upuuzi.

فِيهَا عَيْنٌ جَارِيَةٌ ﴿١٢﴾

12. Humo (kuna) chemchemu inayobubujika.

فِيهَا سُرُرٌ مَّرْفُوعَةٌ ﴿١٣﴾

13. Humo (kuna) vitanda viliyonyanyuliwa.

وَأَكْوَابٌ مَّوْضُوعَةٌ ﴿١٤﴾

14. Na vikombe viliopangwa tayari.

وَنَمَارِقُ مَصْفُوفَةٌ ﴿١٥﴾

15. Na matakia (mito ya kuegemea) iliyopangwa safusafu.

وَزَرَابِيُّ مَبْثُوثَةٌ ﴿١٦﴾

16. Na mazulia (mazuri mno) yaliyotandikwa.

أَفَلَا يَنظُرُونَ إِلَى الْإِبِلِ كَيْفَ خُلِقَتْ ﴿١٧﴾

17. Je, hawamtazami ngamia namna alivyoumbwa?

وَإِلَى السَّمَاءِ كَيْفَ رُفِعَتْ ﴿١٨﴾

18. Na mbingu vipi ilivyonyanyuliwa?

وَإِلَى الْجِبَالِ كَيْفَ نُصِبَتْ ﴿١٩﴾

19. Na majabali vipi yalivyothibitishwa?

وَإِلَى الْأَرْضِ كَيْفَ سُطِحَتْ ﴿٢٠﴾

20. Na ardhi vipi ilivyotandazwa?


فَذَكِّرْ إِنَّمَا أَنتَ مُذَكِّرٌ ﴿٢١﴾

21. Basi kumbusha (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم); hakika wewe ni mkumbushaji (tu).

لَّسْتَ عَلَيْهِم بِمُصَيْطِرٍ ﴿٢٢﴾

22. Wewe si mwenye kuwadhibiti.

إِلَّا مَن تَوَلَّىٰ وَكَفَرَ ﴿٢٣﴾

23. Isipokuwa yule atayegeuka na akakufuru.

فَيُعَذِّبُهُ اللَّـهُ الْعَذَابَ الْأَكْبَرَ ﴿٢٤﴾

24. Basi Allaah Atamuadhibu adhabu kubwa kabisa.

إِنَّ إِلَيْنَا إِيَابَهُمْ ﴿٢٥﴾

25. Hakika ni Kwetu (ndio) marejeo yao.

ثُمَّ إِنَّ عَلَيْنَا حِسَابَهُم ﴿٢٦﴾

26. Kisha bila shaka ni juu Yetu hesabu yao.





Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejeauliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii falhaqqiy@gmail.com