025 - Hadiyth Ya 25: Wanyonge Na Masikini Watakuwa Peponi, Na Majabari Na Wenye Kiburi Watakuwa Motoni



 عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم): ((احْتَجَّتْ الْجَنَّةُ وَالنَّارُ فَقَالَتْ النَّارُ: فِيَّ الْجَبَّارُونَ وَالْمُتَكَبِّرُونَ.  وَقَالَتْ الْجَنَّةُ: فِيَّ ضُعَفَاءُ النَّاسِ وَمَسَاكِينُهُمْ: فَقَضَى الله بَيْنَهُمَا: إِنَّكِ الْجَنَّةُ رَحْمَتِي أَرْحَمُ بِكِ مَنْ أَشَاءُ.  وَإِنَّكِ النَّارُ عَذَابِي أُعَذِّبُ بِكِ مَنْ أَشَاءُ.  وَلِكِلَيْكُمَا عَلَيَّ مِلْؤُهَا)) رواه مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy(رضي الله عنه)  amesema: Mtume wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Pepo na moto zilihojiana [zilikhasimikiana]. Moto ukasema: Kwangu kunapatikana watu majabari na wenye kiburi.  Pepo ikasema: Kwangu kunapatikana watu madhaifu na masikini wao.  Allaah Akahukumu baina yao (Akisema): Wewe Pepo ni Rahma Yangu, Nitamrehemu kwa sababu yako Nimtakaye. Na wewe moto ni adhabu Yangu, Nitamwadhibu Nimtakaye kwa sababu yako, na nyote Nitawajaza)).[1]
 
 
Mafunzo Na Hidaaya:
 
  1. Allaah (سبحانه وتعالى) Anawaacha watu wawe huru kutenda wayatakayo baada ya kuwaonyesha njia ya haki na ya ubatilifu [Al-Balad 90: 8-10].
 
إِنَّا خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن نُّطْفَةٍ أَمْشَاجٍ نَّبْتَلِيهِ فَجَعَلْنَاهُ سَمِيعًا بَصِيرًا ﴿٢﴾ إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا ﴿٣﴾
 
Hakika Sisi Tumemuumba bin-Aadam kutokana na tone la manii iliyochanganyika ili Tumjaribu; Tukamjaalia mwenye kusikia na kuona. Hakika Sisi Tumemuongoza njia; ima awe mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru [2]
 
  1. Hikma ya Allaah (سبحانه وتعالى) kuwajaalia baadhi ya watu kuwa ni masikini, wanyonge na wengineo kuwa ni matajiri wenye nguvu [An-Nahl 16: 71].  Hata Mitume wamefadhilishwa wengine juu ya wengine [Al-Baqarah 2: 253].
 
  1. Ujuzi wa Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba baadhi ya waja Wake watakuwa ni wema japokuwa wao ni dhaifu, maskini na wanyonge, na hivyo hatima yao itakuwa ni Pepo. Na wengineo watakuwa wenye kutakabari na majabari juu ya kuwa ni matajiri, hivyo hatima yao itakuwa ni moto.   [Hadiyth: ((Wataingia Peponi Waislamu masikini kabla ya matajiri wao kwa nusu siku ambayo ni miaka 500)).[3]   
 
  1. Bishara njema ya Pepo kwa walio wanyonge duniani, na tisho la moto kwa wenye kutakabari na majabari. [Rejea Hadiyth namba 55].
 
  1. Hii inatufunza kuwa kufaulu Aakhirah hakutegemei uwezo wa kifedha hapa duniani.
 
 
 



[1]  Muslim.
[2]  Al-Insaan (67: 2-3).
[3]  Swahiyh At-Tirmidhiy ya Al-Albaaniy.