Al-Qamar (54)


سُورَةُ الْقَمَر
Al-Qamar (54)

(Imeteremka Makka)


Imekuja Aya ya kwanza katika Sura hii kuzindua kuwa watu wasikilize kwamba Kiyama kinakaribia, na watu wanahadharishwa na tukio hilo. Kisha zimekuja Aya nyengine baada yake kuweka wazi msimamo wa makafiri kwa mintarafu ya miujiza, na kushikilia kwao kukadhibisha. Na anatakiwa Mtume s.a.w. awapuuze na awangojee mpaka siku watakapo toka makaburini kama nzige walio tapanyika.
Tena baada ya hapo Aya zikawa zinafuatana, zikieleza hali namna mbali mbali za mataifa yaliyo tangulia kwa mnasaba na Mitume wao, na adhabu iliyo washukia. Na baina ya kila kisa na kingine inazindua mawazo ya kwamba Qur'ani tukufu imefanywa nyepesi kwa mwenye kutaka kuwaidhika na kuzingatia.
Mwishoe inabainisha kwamba hao makafiri wa Makka si watu wenye nguvu zaidi au wakali zaidi kushinda mataifa yaliyo kwisha tangulia, na kwamba wao si wenye kuiepuka adhabu. Tena Sura ikakhitimisha kwa kuwahadharisha wanao kadhibisha wenye inda kuwa mwisho wao watakuja tumbukizwa Motoni kifudifudi, na wataambiwa: Onjeni mguso wa Jahannamu mliyo kuwa mkiikadhibisha. Na inawatuza wachamngu katika maskani zao za Mabustanini na mito, katika makao mazuri kwa Mfalme Mwenye uweza.

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ


اقْتَرَبَتِ السَّاعَةُ وَانشَقَّ الْقَمَرُ ﴿١﴾

1.      Saa (Qiyaamah) imekaribia na mwezi umekatika.

وَإِن يَرَوْا آيَةً يُعْرِضُوا وَيَقُولُوا سِحْرٌ مُّسْتَمِرٌّ ﴿٢﴾

2. Na wanapoona Aayah (ishara, dalili) hukengeuka, na husema: “Sihiri inayoendelea”


وَكَذَّبُوا وَاتَّبَعُوا أَهْوَاءَهُمْ ۚ وَكُلُّ أَمْرٍ مُّسْتَقِرٌّ ﴿٣﴾

3. Na wakakadhibisha (haki), na wakafuata matamanio yao, na kila amri (ina muda wa) kuthibitika (kwake).

وَلَقَدْ جَاءَهُم مِّنَ الْأَنبَاءِ مَا فِيهِ مُزْدَجَرٌ ﴿٤﴾

4. Na kwa yakini imekwishawajia katika habari (visa vya Ummati zilizokadhibisha Mitume) ambazo ndani yake kuna makemeo (makali kabisa).

حِكْمَةٌ بَالِغَةٌ ۖ فَمَا تُغْنِ النُّذُرُ ﴿٥﴾

5. Ni hikmah kamilifu lakini hayafai kitu maonyo.

فَتَوَلَّ عَنْهُمْ ۘ يَوْمَ يَدْعُ الدَّاعِ إِلَىٰ شَيْءٍ نُّكُرٍ ﴿٦﴾

6. Basi jiepushe nao (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Siku atakayoita muitaji kuliendea jambo la kuchukiza.

خُشَّعًا أَبْصَارُهُمْ يَخْرُجُونَ مِنَ الْأَجْدَاثِ كَأَنَّهُمْ جَرَادٌ مُّنتَشِرٌ ﴿٧﴾
7. Macho yao yatanyenyekea, watatoka katika makaburi (yao) kama kwamba nzige waliotawanyika.

مُّهْطِعِينَ إِلَى الدَّاعِ ۖ يَقُولُ الْكَافِرُونَ هَـٰذَا يَوْمٌ عَسِرٌ ﴿٨﴾

8. (Watakuwa) Wenye kukimbia mbio vichwa vyao juu (na huku macho yamedokoka) wakielekea kwa muitaji; makafiri watasema: “Hii ni siku ngumu!”

كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ فَكَذَّبُوا عَبْدَنَا وَقَالُوا مَجْنُونٌ وَازْدُجِرَ ﴿٩﴾

9. Walikadhibisha kabla yao watu wa Nuwh, walimkadhibisha mja Wetu, wakasema: “Majnuni.” Na akakaripiwa (kuwekewa vitisho).

فَدَعَا رَبَّهُ أَنِّي مَغْلُوبٌ فَانتَصِرْ ﴿١٠﴾

10. Basi akamwita Rabb (Mola) wake kwamba: “Hakika mimi nimeshindwa, basi Nusuru.”

فَفَتَحْنَا أَبْوَابَ السَّمَاءِ بِمَاءٍ مُّنْهَمِرٍ ﴿١١﴾

11. Tukafungua milango ya mbingu kwa maji yamiminikayo kwa nguvu.

وَفَجَّرْنَا الْأَرْضَ عُيُونًا فَالْتَقَى الْمَاءُ عَلَىٰ أَمْرٍ قَدْ قُدِرَ ﴿١٢﴾

12. Na Tukachimbua (na kububujua kwenye) ardhi chemchemu; basi yakakutana maji (ya mbinguni na ardhini) kwa amri iliyokwisha kadiriwa.

وَحَمَلْنَاهُ عَلَىٰ ذَاتِ أَلْوَاحٍ وَدُسُرٍ ﴿١٣﴾

13. Na Tukambeba kwenye ile (jahazi) iliyo (tengenezwa) kwa mbao na misumari.

تَجْرِي بِأَعْيُنِنَا جَزَاءً لِّمَن كَانَ كُفِرَ ﴿١٤﴾

14. Inatembea kwa Macho Yetu, ni jazaa kwa yule aliyekuwa amekanushwa.

وَلَقَد تَّرَكْنَاهَا آيَةً فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿١٥﴾

15. Na kwa yakini Tumeiacha iwe ni Aayah (ishara, dalili)  je, basi yuko anayekumbuka (na kuwaidhika)?

فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿١٦﴾

16. Basi vipi ilikuwa (kali) adhabu Yangu na maonyo Yangu?

وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿١٧﴾

17. Na kwa yakini Tumeiwepesisha Qur-aan kwa kuikumbuka, basi je, yuko yeyote (yule) anayekumbuka?

كَذَّبَتْ عَادٌ فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿١٨﴾

18. Kina ‘Aad walikadhibisha, basi vipi ilikuwa (kali) adhabu Yangu na maonyo Yangu?

إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا صَرْصَرًا فِي يَوْمِ نَحْسٍ مُّسْتَمِرٍّ ﴿١٩﴾

19. Hakika Sisi Tumewapelekea kimbunga (tsunanmi) katika siku ya nuksi inayoendelea.

تَنزِعُ النَّاسَ كَأَنَّهُمْ أَعْجَازُ نَخْلٍ مُّنقَعِرٍ ﴿٢٠﴾

20. Unawang’oa watu kama kwamba vigogo vya mtende vilivyochopolewa.

فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿٢١﴾

21. Basi vipi ilikuwa (kali) adhabu Yangu na maonyo Yangu?

وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿٢٢﴾

22. Na kwa yakini Tumeiwepesisha Qur-aan kwa kuikumbuka, basi je, yuko yeyote (yule) anayekumbuka?

كَذَّبَتْ ثَمُودُ بِالنُّذُرِ ﴿٢٣﴾

23. Kina Thamuwd waliwakadhibisha Waonyaji.

فَقَالُوا أَبَشَرًا مِّنَّا وَاحِدًا نَّتَّبِعُهُ إِنَّا إِذًا لَّفِي ضَلَالٍ وَسُعُرٍ ﴿٢٤﴾

24. Wakasema: “Ah! Tumfuate mtu mmoja miongoni mwetu? Hakika hapo sisi tutakuwa katika upotofu na wazimu.

أَأُلْقِيَ الذِّكْرُ عَلَيْهِ مِن بَيْنِنَا بَلْ هُوَ كَذَّابٌ أَشِرٌ ﴿٢٥﴾

25. “Ah! Ameteremshiwa dhikri (mawaidha, ukumbusho) baina yetu (sote)? Bali yeye ni muongo fedhuli mkubwa.”

سَيَعْلَمُونَ غَدًا مَّنِ الْكَذَّابُ الْأَشِرُ ﴿٢٦﴾

26. Watakuja kujua kesho nani muongo fedhuli mkubwa.

إِنَّا مُرْسِلُو النَّاقَةِ فِتْنَةً لَّهُمْ فَارْتَقِبْهُمْ وَاصْطَبِرْ ﴿٢٧﴾

27. (Tukamwambia Rasuli Wetu Nabii Swaalih): “Hakika Sisi Tutawapelekea ngamia jike (kama walivyotaka) awe jaribio kwao, basi watazame na vuta subira.”

وَنَبِّئْهُمْ أَنَّ الْمَاءَ قِسْمَةٌ بَيْنَهُمْ ۖ كُلُّ شِرْبٍ مُّحْتَضَرٌ ﴿٢٨﴾

28. Na wajulishe kwamba maji yatagawanywa baina yao (baina ya huyo ngamia na wao), kila (siku ya) kinywaji itahudhuriwa (na mwenye zamu yake).

فَنَادَوْا صَاحِبَهُمْ فَتَعَاطَىٰ فَعَقَرَ ﴿٢٩﴾

29. Wakamwita swahibu wao, akaazimia (kuchukua silaha), akamkata ukano wa mvungu wa goti (akamchinja).

فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿٣٠﴾

30. Basi vipi ilikuwa (kali) adhabu Yangu na maonyo Yangu?

إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ صَيْحَةً وَاحِدَةً فَكَانُوا كَهَشِيمِ الْمُحْتَظِرِ ﴿٣١﴾

31. Hakika Sisi Tumewapelekea Swayhatan (ukelele angamizi) mmoja tu, basi wakawa kama mabuwa (ya mtengenezaji kitalu) yaliyokatika-katika.


وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿٣٢﴾

32. Na kwa yakini Tumeiwepesisha Qur-aan kwa kuikumbuka, basi je, yuko yeyote (yule) anayekumbuka?

كَذَّبَتْ قَوْمُ لُوطٍ بِالنُّذُرِ ﴿٣٣﴾

33. Watu wa Luutw waliwakadhibisha waonyaji.

إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ حَاصِبًا إِلَّا آلَ لُوطٍ ۖ نَّجَّيْنَاهُم بِسَحَرٍ ﴿٣٤﴾

34. Hakika Sisi Tuliwapelekea tufani ya mawe (ikawaangamiza) isipokuwa watu wa Luutw, Tukawaokoa (karibu na) Alfajiri.


نِّعْمَةً مِّنْ عِندِنَا ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِي مَن شَكَرَ ﴿٣٥﴾

35. Neema kutoka Kwetu, hivyo ndivyo Tunavyomlipa yule anayeshukuru.

وَلَقَدْ أَنذَرَهُم بَطْشَتَنَا فَتَمَارَوْا بِالنُّذُرِ ﴿٣٦﴾

36. Na kwa yakini aliwaonya unyakuaji Wetu (wa adhabu), lakini wakayatilia shaka maonyo (Yangu).

وَلَقَدْ رَاوَدُوهُ عَن ضَيْفِهِ فَطَمَسْنَا أَعْيُنَهُمْ فَذُوقُوا عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿٣٧﴾

37. Na kwa yakini walimshawishi (awape) wageni wake, basi Tukawapofoa macho yao (na Tukawaambia): “Onjeni adhabu Yangu na maonyo Yangu.”


وَلَقَدْ صَبَّحَهُم بُكْرَةً عَذَابٌ مُّسْتَقِرٌّ ﴿٣٨﴾

38. Na kwa yakini iliwajia asubuhi (mapema) adhabu ya kudumu.

فَذُوقُوا عَذَابِي وَنُذُرِ ﴿٣٩﴾

39. Basi onjeni adhabu Yangu na maonyo Yangu.

وَلَقَدْ يَسَّرْنَا الْقُرْآنَ لِلذِّكْرِ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿٤٠﴾

40. Na kwa yakini Tumeiwepesisha Qur-aan kwa kuikumbuka, basi je, yuko yeyote (yule) anayekumbuka?

وَلَقَدْ جَاءَ آلَ فِرْعَوْنَ النُّذُرُ ﴿٤١﴾

41. Na kwa yakini watu wa Fir’awn walifikiwa (na) waonyaji.

كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا كُلِّهَا فَأَخَذْنَاهُمْ أَخْذَ عَزِيزٍ مُّقْتَدِرٍ ﴿٤٢﴾

42. (Lakini) Walikadhibisha Aayaat (ishara, dalili) Zetu zote Tukawachukuwa mchukuo wa ‘Aziyzin-Muqtadir (Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika daima - Mwenye uwezo wa yote daima).

أَكُفَّارُكُمْ خَيْرٌ مِّنْ أُولَـٰئِكُمْ أَمْ لَكُم بَرَاءَةٌ فِي الزُّبُرِ ﴿٤٣﴾

43. Je, makafiri wenu (enyi Maquraysh) ni bora kuliko hao (ummah wa awali)? Au yameandikwa katika Maandiko (kuwa) mmetolewa hatia (dhidi ya adhabu Yangu?).

أَمْ يَقُولُونَ نَحْنُ جَمِيعٌ مُّنتَصِرٌ ﴿٤٤﴾

44. Au wanasema: “Sisi ni wengi tutashinda (tu).”

سَيُهْزَمُ الْجَمْعُ وَيُوَلُّونَ الدُّبُرَ ﴿٤٥﴾

45. Wingi wao utashindwa, na watageuka nyuma (kukimbia).

بَلِ السَّاعَةُ مَوْعِدُهُمْ وَالسَّاعَةُ أَدْهَىٰ وَأَمَرُّ ﴿٤٦﴾

46. Bali Saa (Qiyaamah) ndio miadi yao, na Saa ni jangaa kubwa na chungu zaidi.

إِنَّ الْمُجْرِمِينَ فِي ضَلَالٍ وَسُعُرٍ ﴿٤٧﴾

47. Hakika wahalifu wamo katika upotofu na wazimu.

يَوْمَ يُسْحَبُونَ فِي النَّارِ عَلَىٰ وُجُوهِهِمْ ذُوقُوا مَسَّ سَقَرَ ﴿٤٨﴾

48. Siku watakayoburutwa Motoni kifudifudi (waambiwe): “Onjeni mguso wa (Moto wa) Saqar.”

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ ﴿٤٩﴾

49. Hakika sisi Tumekiumba kila kitu kwa makadirio.

وَمَا أَمْرُنَا إِلَّا وَاحِدَةٌ كَلَمْحٍ بِالْبَصَرِ ﴿٥٠﴾

50. Na Amri Yetu (kwa kitu chochote kile Tukitakacho) haiwi isipokuwa kama upepeso wa jicho.

وَلَقَدْ أَهْلَكْنَا أَشْيَاعَكُمْ فَهَلْ مِن مُّدَّكِرٍ ﴿٥١﴾

51. Na kwa yakini Tumewaangamiza wenzenu, je, basi yuko yeyote (yule) mwenye kukumbuka (na kuwaidhika)?

وَكُلُّ شَيْءٍ فَعَلُوهُ فِي الزُّبُرِ ﴿٥٢﴾

52. Na kila kitu wakifanyacho kimo katika maandiko (madaftarini yanayorekodi ‘amali).

وَكُلُّ صَغِيرٍ وَكَبِيرٍ مُّسْتَطَرٌ ﴿٥٣﴾

53. Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa.

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَنَهَرٍ ﴿٥٤﴾

54. Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na mito.  

فِي مَقْعَدِ صِدْقٍ عِندَ مَلِيكٍ مُّقْتَدِرٍ ﴿٥٥﴾

55. Katika makao ya kweli kwa Maliykin-Muqtadir (Mfalme - Mwenye uwezo daima).




Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejeauliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii falhaqqiy@gmail.com