027 - Hadiyth Ya 27: Kila Mtu Ana Jukumu La Kuchunga Atakaloulizwa



عَنْ ابْنِ عُمَرَ (رضي الله عنهما) عَنْ النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قَالَ:  ((كُلُّكُمْ رَاعٍ وَكُلُّكُمْ مَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ,  وَالأمِيرُ رَاعٍ,  وَالرَّجُلُ رَاعٍ عَلَى أَهْلِ بَيْتِهِ, وَالْمَرْأَةُ رَاعِيَةٌ عَلَى بَيْتِ زَوْجِهَا وَوَلَدِهِ, فَكُلُّكُمْ رَاعٍ وَكُلُّكُمْ مَسْئُولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ)) متفق  عليه
 
Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar(رضي الله  عنهما)   kwamba Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Nyote ni wachunga na kila mmoja wenu ataulizwa kuhusu alichokichunga. Kiongozi ni mchunga, na mume ni mchunga juu ya mkewe na mke ni mchunga juu ya nyumba ya mumewe na watoto wake. Kwa hivyo nyote ni wachunga na kila mmoja wenu ataulizwa kuhusu alichokichunga)).[1]
 
Mafunzo Na Hidaaya:
 
  1. Kila Muislamu analo jukumu lake katika jamii [Al-Ahzaab 33: 72].
إِنَّا عَرَضْنَا الْأَمَانَةَ عَلَى السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَالْجِبَالِ فَأَبَيْنَ أَن يَحْمِلْنَهَا وَأَشْفَقْنَ مِنْهَا وَحَمَلَهَا الْإِنسَانُ ۖ إِنَّهُ كَانَ ظَلُومًا جَهُولًا ﴿٧٢﴾
 
Hakika Sisi Tulidhihirisha amana (amri, makatazo, majukumu) kwa mbingu na ardhi na majabali (Tukazitaka kuibeba hiyo amana); vikakataa kuibeba na vikaiogopa; lakini bin-Aadam akaibeba. Hakika yeye (bin-Aadam) amekuwa dhalimu mno, jahili mno (kwa kutokuitimiza amana)[2]
 
 
  1. Jukumu ni amana na kila mmoja ataulizwa kuhusu kutimiza kwake jukumu.
 
  1. Kutimiza amana ni miongoni mwa sifa zitakazompatia Muislamu Pepo ya Firdaws [Al-Muuminuun 23: 8].
 
  1. Mume na mke washirikiane katika malezi ya watoto ili wakuwe katika maadili mazuri ya Kiislamu.
 
  1. Mwanamke wa Kiislamu ana cheo kikubwa katika nyumba kwa kuwa ana jukumu kubwa la ulezi wa nyumba yake.

  1. Kutimizia amana au jukumu ni jambo mojawapo la kumwezesha mtu kuvuka As-Swiraatw Siku ya Qiyaamah [Hadiyth: ((...na zitatumwa amana na ar-rahm [fuko la uzazi; uungaji udugu], navyo vitasimama pembeni ya Swiraatw kuliani na kushotoni…..))].[3]
 

 



[1]  Al-Bukhaariy na Muslim.
[2]  Al-Ahzaab (33: 72).
[3]  Muslim.