Safiyyah Bint Abdulmuttalib
Mwanamke wa Mwanzo Kumuua Mshirikina
Ni nani huyu mama mtukufu mwenye hadhi aliyetamaniwa na
kutarajiwa na maelfu ya wanaume. Ni nani Sahaba huyu shujaa aliyekuwa wa
mwanzo katika wanawake kumuua mshirikina katika uislam?
Ni nani mwanamke huyu mwenye ushujaa na ushupavu alietoa
shujaa wa mwanzo kunyanyua upanga katika njia ya Allah. Hakika si mwengine
ila ni Safiyyah bint Abdulmuttalib al-Hashimiya Al Qurayshiya, shangazi yake Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam)
unatosheleza utukufu wake kwa kila upande
Baba
yake, Abdulmuttalib ibn Hashim ni babu wa
Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) na kiongozi wa makureshi na
bwana mwenye kutiiwa. Mama yake Haalab bint Wahab
ni dada wa bibi Amina bint Wahab mama yake
Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam).
Mumewe
wa mwanzo ni Alharith ibn Harb, ndugu wa Abu Sufiyan ibn Harb kiongozi wa Bani Umaiyyah.
Na alimkalia kizuka mumewe wa pili ambae ni Al-Awwaam
ibn Khuwaylid ndugu wa Bibi Khadija bint
Khuwaylid mama mtukufu wa waarabu kabla uislam na ni mama wa waislam
wa mwanzo. Na mtoto wake Zubeir ibn Al-Awwaam
ni mlinzi wa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam). Je baada ya haya kuna zaidi
ya utukufu ambao nafsi zingeliutamani zaidi ya utukufu wa imani?!.
Alifariki
mumewe Al-Awwaam ibn Khuwaylid, akiwa
amemwachia mtoto mmoja mdogo nae ni Zubeir, mtoto aliemlea katika maisha ya
kishujaa na ukakamavu na akamlea kuwa ni mpanda farasi na mpiganaji
shujaa. Ikawa mchezo wake daima ni kutunga shabaha na kutengeneza pinde
na akitamani atumie ushujaa huu kwa kila lenye kumtisha na kumzonga na
kumhatarisha. Na alikuwa akimuona anazembea au kuogopa humpiga sana. Ikafika
hadi ami zake wakamgomba na kumwambia; "Sivyo hivi mtoto anavyolelewa na
kupigwa wewe unampiga na kumuumiza. -sivyo hivyo- mama anatakiwa kumpenda
mwanawe". Akawajibu kwa kusema; “Ama anaesema kwamba namchukia basi
amesema uongo bali nampiga apate akili na ashinde na aje na ngawira"
Mwenyezi
Mungu alipomtuma Mtume wake na dini ya uongofu na haki na akamtuma kuwa ni
muhadharishaji na mtoa bishara njema kwa watu, akamuamrisha aanze kulingania
watu wake wa karibu akakusanya Bani Abdulmuttalib wakike kwa kiume,
wakubwa kwa wadogo akawahutubia na kusema:
“Ewe
Fatma bint Muhammad, ewe Safiyyah bint Abdulmuttalib enyi ukoo wa Bani
Abdulmuttalib hakika mimi similiki chochote kwenu mbele ya Allah".
Akawalingania
imani kuwasisitiza kuiamini risala yake wakaikubali nuru ya imani
waliyoikubali na wakaitakataa nuru wale waliyoikataa. Akawa Safiyyah bint
Abdulmuttalib miongoni mwa kizazi cha mwanzo miongoni mwa waislamu waumini
hapo ndipo alipozidi kujikusanyia utukufu wa nasaba na utukufu mkuu wa
Uislamu.
Akaingia
Safiyyah katika msafara wa nuru ya (kiimani) yeye na mwanawe, na akapata
shida mithili ya zile zilizowakaribia waislamu wa mwanzo kutokana na vishindo
na mateso ya makureshi.
Mwenyezi
Mungu alipomuamrisha Mtume kuhajiri kwenda Madina, aliacha Bibi huyu Mtukufu
nyuma yake Makka kila kumbukumbu njema na njia zote za fakhari, na akaelekea
Madina akiwa ni mwenye kuhajiri na dini yake kwa ajili ya Allah na Mtume
wake.
Licha
ya kwamba mama huyu mtukufu alikuwa anaingia miaka
sitini ya umri wake, alikuwa na nafasi kubwa katika medani za jihadi.
Tarekhe (historia) ingali inaitaja nafasi huyu kwa ulimi wa mshangao na
shukrani. Inatosheleza hapa kutaja matukio mawili. La mwanzo (wake?) ni
katika vita vya Uhud na la pili ni siku
ya vita vya Handaki.
Ama
yanayomuhusu kutokana na vita vya Uhud ni kwamba alitoka pamoja na jeshi la
waislamu akiwa na kundi la wanawake wa kiislamu akawa ni mwenye kuchota maji
kunywesheza wenye kiu, na kukusanya na kuweka sawa pinde na mishale. Huku
akiwa na lengo lake kuu nalo ni kushuhudia vita kwa kila hisia zake.
Hakuna
ajabu kwa hilo kwa ndugu yake Hamza, Simba wa Mwenyezi Mungu na mwanawe Zubeir,
mlinzi wa Mtume wamo (vitani). Vile vile juu ya yote haya vita hivi ni muhimu
kwake kwani Uislamu alijiunga nao kwa mapenzi na akahajiri kwa ajili ya Allah
akitarajia malipo. Na kupitia dini hiyo, ndiyo pepo ataipata.
Pale
alipoona waislamu wanamkimbia Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) ila
wachache na wakawa washirikina wamemkaribia Mtume (Sallallahu ‘Alayhi
Wasallam) na kutaka kumuua; akatupa mtungi chini na kuchupa mithili ya
simba jike ambae watoto wake walioshambuliwa. Akachomoa mkuki kwa mmoja
aliyekufa, akawa anakata safu akishambulia nyuso za (washirikina) huku akipaza
sauti yake kuwaambia waislamu:
“Acheni
nyie! mnashindwa mbele ya Mtume wa Allah?” Mtume alipomuona anamsogelea
alichelea asije akamuona ndugu yake amekufa na kukatwakatwa vibaya vibaya na
akamuashiria mwanawe Al-Zubeir akasema Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam).
kumwambia:
“Zubeir!,
mwanamke! Mwanamke!"
Zubeir
akageuka kumwangalia na kumwambia;
"Ewe
mama yangu rudi! rudi!"
Akamwambia:
"Huna mama leo hapa!"
Akasema
Zubeir; “Mtume amekuamrisha kurudi".
Akasema
“kwa nini?, Wakati nimesikia ndugu yangu amepasuliwa?”
Mtume
(Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) akamwambia Zubeir; “Mwachilie aende zake"
Baada
ya vita kumalizika, Safiyyah alisimama mbele ya ndugu yake Hamza, akamkuta
amepasuliwa tumbo na ini kutolewa na pua imekatwa na masikio pia. Uso
umechorwachorwa kwa kuchinjwa, akamtakia msamaha kwa Allah na akasema;
"hakika nimeridhia qadhaa ya Allah .Wallahi nitasubiri na kutarajia
ujira Inshaallah.”
Hivi
ndivyo ilivyokuwa hali yake siku ya Uhud.
Ama
hali yake siku ya Handaki, ni kisa hichi cha ajabu chenye kushangaza hata
wale wenye akili. Pokea habari hizi kama zinavyosimuliwa na vitabu vya
kihistoria.
Ilikuwa
ni kawaida ya Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) anapoazimia vita, kuwaweka
wanawake pamoja na watoto kwenye ngome ili kuwalinda dhidi ya mashambulizi ya
ghafla dhidi ya mji wa Madina wakati wapiganaji waislamu hawapo.
Hivyo
ndivyo ilivyokuwa siku ya Handaki akawaweka wakeze na shangazi yake na kundi
la wanawake wa kiislamu kwenye ngome ya Hassan ibn Thabit ambayo aliirithi
toka kwa wazee wake. Ilikuwa ni ngome imara na haikuwa rahisi kufikiwa.
Wakati
waislamu walipokuwa ulinzini pembeni mwa Handaki kukabiliana na Makureshi na
washirika wao, wakawa wameacha wanawake na watoto na kumshughulikia adui,
Ghafla, Safiyyahh bint Abdulmuttalib, alikiona kivuli kinakwenda kwenye kiza
cha alfajiri. Akatega sikio kusikiliza na kukitolea jicho na kukifuatilia.
Kumbe alikuwa ni myahudi akijisogeza kwenye ngome huku akijaribu kutafuta
habari na kupeleleza kiliomo ndani ya ngome ile.
Safiyyah
alitambua kuwa yule alikuwa ni jasusi alietumwa kutafuta habari. Je baina ya
kuta zake kuna wanaume ndani ya ngome au hamna zaidi ya wanawake na
watoto?. Akasema Safiyyah ndani ya nafsi yake; Mayahudi wa Banu Quraidha
wamevunja ahadi yao na Mtume na wamewaunga mkono makureshi na washirika wao
dhidi ya waislamu. Wala hapana baina yetu na (mayahudi) wa kutuhami na Mtume
(Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) na masahaba wapo mstari wa mbele dhidi ya adui.
Akiweza
kuchukua habari za uhakika wa kilichomo ndani ya ngome hii atateka wanawake
na kuwafanya watumwa watoto na huo utakuwa ni mkosi mkubwa. Hapo hapo
alichukua ushungi wake (khimar) na kufunika kichwa na akajizonga nguo zake
vizuri kiunoni na akachukua kipande cha kigongo akaweka begani mwake na
akatoka mpaka kwenye mlango wa ngome. Akafungua kwa hadhari na kumuangalia
adui wa Allah kwa hadhari kubwa. Alipohisi yupo kwenye shabaha nzuri na
kumpata akamwachia kigongo kizuri cha kichwa na papo hapo akaanguka chini na
kumuongeza cha pili na cha tatu, mpaka akahakikisha amekwisha kufa.
Akamwendea
tena na kisu chake na kukitenga kichwa cha adui huyo na mwili wake, baada ya
hapo akakirusha nje ya ngome, kikibiringika mpaka walipo mayahudi. Mayahudi
walipokiona kichwa cha mwenzao kikibiringita walisema; “Tunajua wazi kwamba
Muhammad asingeweza kuwaacha wanawake na watoto pasina ulinzi”
Wakarudi
nyuma kwenda zao.
Mwenyezi
Mungu awe radhi na Safiyyah bint Abdulmuttalib. Hakika alikuwa ni mfano wa
pekee wa wanawake wa kiislamu.
Amemlea
mtoto wake na akakamilisha vyema malezi. Mitihani ikamjaribu ikamkuta ni shujaa
na mwenye akili. Tarekhe ikamuandika katika kurasa zake safi: “Hakika
Safiyyah bint Abdulmuttalib ni mwanamke wa mwanzo kumuuwa mshirikina katika
Uislamu.