Suhayb Ar-Rumi-aliefadhili dini badala ya mali
Kati kati ya karne ya
tano milaadiya na kabla ya kuja utume, mji wa Al-Uballah ulioko kwenye kingo za
mto Euphrates ulitawaliwa na Mwarabu anaeitwa Sinan Ibn Malik. Alipewa jukumu
hilo na mtawala wa kiajemi. Alikuwa na watoto wengi na kwa bahati nzuri
alipendezwa sana na mmoja wa watoto wake ambaye wakati huo alikuwa umri wake
hata hajatimia miaka mitano. Jina lake ni Suhayb na alikuwa mtoto mchangamfu na
mara nyingi alikuwa akimfurahisha baba yake.
Siku moja mama yake
Suhayb alimchukua pamoja na ndugu zake wengine kwenda matembezi katika kjiji
cha Ath-thani. Ilikusudiwa iwe siku ya mapunziko na furaha lakini
yaliyotokea siku hiyo yalikuwa mambo makubwa na kubadilisha mwelekeo wa maisha
ya Suhayb.
Siku hiyo, kijiji
hicho kilivamiwa na majeshi wa kibizantini. Walinzi walioambatana na
msafara wao wote walizidiwa nguvu na kuuliwa. Vitu vyao vyote vilitekwa na
kundi la watu (kutekwa nyara) akiwemo mtoto mdogo wa miaka mitano, Suhayb.
Suhayb akachukuliwa
na kupelekwa soko la watumwa mji mkuu wa Constantinpole na kuuzwa. Hapo
tena akapita kwenye mikono tofauti ya wafanyabiashara ya utumwa. Khatma yake
haikuwa tofauti na maelfu ya watumwa waliojaa kwenye nyumba za kasri na mavilla
ya wabizantini.
Utoto na ujana wake
wote aliupitisha akiwa mtumwa na kwa muda wa miaka ishirini alikuwa
kwenye ardhi ya wabizantini. Hii ilimsaidia kuweza kufahamu na
kuelewa mfumo mzima wa maisha na jamii ya wabizantini. Aliona ndani ya makasri
vipi udhalimu na ubadhirifu ulivyotawala na kuichukia sana hali hii huku
akijisemea, “jamii kama hii itaweza kusafishwa na gharika”
Alikulia na kuongea
kigiriki lugha ya kibizantini na kusahau kabisa kiarabu. Hata hivyo,
hakusahau asili yake mtoto wa jangwani. Alikuwa akiota na kutamani siku ambayo
ataachiwa huru na kuungana na watu wake.
Ilipojitokeza nafasi
tu alitoroka na kukimbilia moja kwa moja Makka, unzi hizo ilikuwa ndio makaazi
ya wakimbizi. Alipewa jina la Arrumi kutokana na lugha na umbile lake.
Mmoja katika waheshimiwa wa Makka enzi hizo Abdullah ibn Judan akamchukua
na kukaa naye. Suhayb akajiingiza katika biashara na kupata mafanikio
sana mpaka kuwa tajiri.
Siku moja aliporudi
Makka kutoka katika safari zake za kibiashara akapata habari kwamba Muhammad
ibn Abdulla anawalingania watu kumuamini Mwenyezi Mungu na kuwaamrisha kufanya
mambo mema na kuwakataza kufanya mambo mabaya. Akauliza kuhusu mtu huyu (Muhammad)
ni nani hasa na wapi anakaa, akafahamishwa.
“Yupo kwa Al-Arqam
ibn Al-Arqam, jihadhari na maquraysh wasikuone. Wakikuona watakufanyia na
wewe ni mgeni mji huu na wala huna uhusiano wowote wa kikabila wa kukutetea
wala ukoo wa kukusaidia”
Suhayb akaenda kwa
kujifichaficha mpaka nyumba ya Al-Arqam. Mlangoni akakutana na Ammar bin
Yassir ambaye baba yake anajuana naye. Alisita kwanza kisha akasogea na kusema,
“Umekuja kufuata nini
(hapa) Ammar?”
“Nikuulize wewe, nini
umefuata?, akajibu Ammar.
“Ninataka kwenda kwa
huyu mtu (Muhammad) na kumsikiliza mimi mwenyewe nini anasema”
“Na mimi hivyo
hivyo,” basi na tuingie, wakaambizana.
Wakaingia na
kusikiliza kwa kituo. Nuru ya imani ikawaingia nyoyoni mwao na siku hiyo
hiyo wakasilimu. Wakaitumia siku hiyo nzima wakiwa pamoja na Mtume (SAW)
na ilipofika usiku wakaondoka kwa kujificha, nyuso zao zimejaa tabasamu .
Kama yale
yaliyowasibu waislam waliopo Makka, yakampata na Suhayb pia. Aliteswa na
kuteswa kama walivyoshughulikiwa Bilal, Ammar na mama yake Sumayyah, Khabab na
wengineo. Yalikuwa ni mafundisho ya Mtume (SAW) na kupewa moyo na masahaba ndio
vitu pekee vilivyomsaidia kutoterereka katika imani yake.
Rukhsa ya kufanya
hijra, kwenda Madina ilipotoka Suhayb aliazimia kuandamana na Mtume Muhammad (SAW)
pamoja na Abubakar. Hata hivyo, maquraysh wakagundua mpango wake huu na
kuamua kumwekea ulinzi wa hali ya juu ili asiweze kuondoka yeye mwenyewe pamoja
na mali zake alizozipata alipokuwa akifanya biashara Makka .
Baada ya Mtume na
Abubakar kuondoka, Suhayb aliendelea kubaki Makka na kuvuta muda huku akisubiri
wakati muafaka wa kufanya hijra. Alijitahidi kutafuta mbinu za kuwakwepa
walinzi bila ya mafanikio mpaka ikambidi atumie hila.
Usiku mmoja ilikuwa
baridi kali na Suhayb akadai kuwa maumivu ya tumbo na alitoka kila mara kwenda
nje akijidai ‘anajisaidia’. Walinzi walipomuona katika hali ile
wakaambizana, “tusiwe na wasi wasi Lata na Uzza wanamshughulikia tumbo lake”.
Hawakushtushwa sana
na wakaendelea na lindo lao hadi usingizi ukawachukua. Suhayb akatoka
tena kama kwenda msalani na alipowaona wamelala akawavuka na kupanda ngamia
akielekea Madina.Walinzi waliposhtuka na kugundua kwamba Suhayb tayari
ametoroka, wakapanda farasi wao mbio kumfuata wakijua wapi alikoelekea na
hatimaye kumkaribia.
Suhayb alipowaona
akapanda kwenye mlima na kujiandaa kwa kuelekeza mshale wake kwa maquraysh huku
akitoa sauti kubwa na ya kutisha, “enyi maquraysh, nnakuahidini mimi ni mmoja
katika mastadi wa mishale na nikitunga sikosei, na yoyote atakayenikaribia kila
mshale nilionao nitampiga nao na kisha nitapambana nanyi kwa upanga wangu.”
Msemaji wa kiquraysh
akasema, “ na sisi tutahakikisha kwamba hatutokuruhusu ukimbie na mali.
Ulipokuja Makka ulikuwa maskini hohehahe, na ukapata ulichokipata.”
Suhayb akawauliza,
“Nikikupeni mali zangu mtafanya nini?, mtaniachia niendelee na safari yangu?.
Akajibiwa, “ndiyo”.
Suhayb akawafahamisha
wapi alipoficha mali zake Makka na maquraysh wakamruhusu.
Akaendelea na safari
yake huku akiwa na furaha kwamba baada ya muda atakuwa karibu na Mtume (SAW) na
kupata uhuru wa kuabudu. Alipofika Quba nje kidogo ya Madina ambapo Mtume
Muhammad (SAW) alipumzika wakati wa safari yake, Mtume (SAW) alimuona Suhayb
anakuja na alijawa na furaha na kumpokea.
“Biashara yako imezaa
ewe Abu Yahya, biashara yako imezaa,” alisema Mtume (SAW) mara tatu. Suhayb
alifurahi sana kusikia kauli ya Mtume Muhammad (SAW) ingawa alishangaa kidogo
na kusema, “Wallahi, hajawahi kuja mtu yoyote (kukuhadithia) kabla yangu.
Ni Jibril peke yake ndio aliyekwambia, na kuyathibitisha hayo. Aya 207
Surati Baqarah ikateremka.
“Na katika watu yupo
ambae huiuza nafsi kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu;na Mwenyezi Muingu na
mpole kwa waja wake”
Nini fedha, nini mali
ni dhahabu na dunia yote mbele ya imani sahihi? Suhayb akapendwa sana na
Mtume (SAW) na kumbashiria kuwa atakuwa ufunguo wa kuifungua Byzantin kuingia
uislam.
Suhayb pia
alikuwa mtu wa kupenda utani, siku moja Mtume (SAW) alimuona akila tende,
akamuona Suhayb ana uvimbe kwenye jicho lake moja na kumwambia huku akicheka,
“unakula tende mbivu wakati jicho lako moja lina uvimbe?”
Suhayb akajibu,
“Kwani kuna ubaya gani?”
“nnakula na jicho
jengine”.
Suhayb alikuwa
mkarimu kwani ruzuku aliyokuwa akipata kutoka Baytul Mal alikuwa anaitoa kuwapa
maskini na wanaohitaji, alikuwa mfano wa Aya ya Quran, “ Na kuwalisha chakula
juu ya kukipenda kwake,maskini ,mayatima na wafungwa” Al –insaan /8
Ukarimu wake
ulisifiwa na Umar ibn Khattab pale aliposema:
“Nimekuona ukitoa
chakula kwa wingi mpaka inaonekana unafanya israaf (katika kutoa).
Suhayb akajibu,
“Nilimsikia mjumbe wa Mwenyezi Mungu akisema “Mbora wenu ni yule anaelisha
(chakula)”
Uchamungu wa Suhayb
ulikuwa wa kupigiwa mfano kwani hata Umar ibn Khattab alimteua kuwaongoza
waislam katika kile kipindi alichokufa mpaka pale kuchaguliwa Khalifa mwengine.
Umar aliwaita
masahaba sita, Uthman, Ali, Talha, Zubeir, Abdulrahaman ibn Awl na Saad ibn Abi
Waqas. Hakumchagua yoyote miongoni mwao, kwani kama angelifanya hivyo,
kwa mujibu wa riwaya “kungelikuwa na muda ambao makhalifa wawili
wangelitazamana”
Aliwaagiza hawa sita
washauriane pamoja na waislam kumchagua mrithi na kusema, “Waliyusalli binnas
Suhayb, Suhayb asalishe watu”
Alikuwa imamu kwa
kipindi chote alichoteuliwa na Umar mpaka alipofariki na hadi kuchaguliwa
Khalifa mwengine.
Uteuzi wa Suhayb
umeonesha pia jinsi uislam ulivyowathamini watu mbali mbali, miongoni mwa
waarabu na hata wasiokuwa waaarabu, waliokuwa watumwa na hata mabwana na
kudhalika.
Enzi za Mtume (SAW)
mnafiki mmoja, Qaysib Mutatiyah aliwatukana baadhi ya waislam aliowakuta kwenye
‘halaqah’ wakisoma. Walikuwapo kina Salman Alfarsi, Suhayb Arrumi na Bilal Al
habashi na wengineo na akasema,
“Ni Aws na Khazraj
ndio waliomlinda huyu mtu (Muhammad) na nyinyi mnafanya nini hapa pamoja naye?”
Muadhi ibn Jabal
aliposikia dharau hii alikasirika na kumtaarifu Mtume (SW) yote
aliyoyasema Qays. Mtume (SW) naye akajawa na hasira na hapa hapo akaingia
msikitini na kuamrisha kuadhiniwe.
Hii ndio ilikuwa njia
ya kuitana waislam kama jambo kubwa limetokea, akasimama na kumshukuru Allah
(SW) na kusema:
“Mola wenu ni mmoja, Baba yenu ni mmoja, dini yenu ni moja, chukueni
mwongozo. Hamjaupata uarabu kupitia baba na mama, ni kwa kupitia ndimi,
hivyo yoyote anayezungumza kiarabu basi ni mwarabu”