008 - Hadiyth Ya 8: Kukimbilia Kutoa Sadaka Kabla Ya Mauti

008 - Hadiyth Ya 8: Kukimbilia Kutoa Sadaka Kabla Ya Mauti


عن أبي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  قَالَ: جَاءَ رَجُلٌ إِلَى النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم) فَقَالَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ, أَيُّ الصَّدَقَةِ أَعْظَمُ أَجْرًا؟ قَالَ: ((أَنْ تَصَدَّقَ وَأَنْتَ صَحِيحٌ شَحِيحٌ تَخْشَى الْفَقْرَ وَتَأْمُلُ الْغِنَى وَلاَ تُمْهِلُ حَتَّى إِذَا بَلَغَتْ الْحُلْقُومَ قُلْتَ لِفُلاَنٍ كَذَا وَلِفلاَنٍ كَذَا وَقَدْ كَانَ لِفُلاَنٍ)) متفق عليه
 
Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah(رضي الله عنه)  amesema: “Mtu mmoja alikuja kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwuliza: Ee Mjumbe wa Allaah! Ni sadaka ipi yenye ujira mkubwa zaidi?  Akasema: ((Ni utoe sadaka nawe umzima, unataka mali bado, unakhofia ufukara na unatarajia utajiri. Wala usichelewe mpaka roho ikafika kwenye koo, ukaanza kusema: fulani ana haki kadhaa na fulani ana haki kadhaa na fulani alikuwa ana haki kadhaa)).[1]
 
Mafunzo Na Hidaaya:
 
  1. Sadaka ya aliye mzima ni bora kuliko ya mgonjwa kwa sababu aghlabu binaadamu anakuwa mchoyo na bakhili anapokuwa katika afya kamili. Hivyo, atakapotoa wakati yu mzima itakuwa ni sadaka ya niyyah safi na mapenzi ya kutoa kwa ajili ya Allaah (سبحانه وتعالى).
 
  1. Kukimbilia kutenda mema wakati una umri na siha kabla ya kufikwa na mtihani wa magonjwa na ufukara [Al-Baqarah 2: 148]. Na amrisho la kutoa sadaka kabla ya kufika siku ambayo halitomfaa mtu lolote [Al-Baqarah 2: 254].
 
  1. Kukimbilia kutoa sadaka kabla ya kufikwa na mauti kama Anavyoonya Allaah (سبحانه وتعالى).
 
 وَأَنفِقُوا مِن مَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ فَيَقُولَ رَبِّ لَوْلَا أَخَّرْتَنِي إِلَىٰ أَجَلٍ قَرِيبٍ فَأَصَّدَّقَ وَأَكُن مِّنَ الصَّالِحِينَ. وَلَن يُؤَخِّرَ اللَّـهُ نَفْسًا إِذَا جَاءَ أَجَلُهَا ۚ وَاللَّـهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ
Na toeni katika yale Tuliyokuruzukuni kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti akasema: “Mola wangu! Lau Ungeliniakhirisha mpaka muda wa karibu hivi, basi ningenitoa swadaqah  na ningelikuwa miongoni mwa (watu) wema.” Lakini Allaah Haiakhirishi (kamwe) nafsi yeyote inapokuja ajali yake (ya kufa) na Allaah ni Khabiyr kwa mnayoyatenda. (Mjuzi wa  vilivyodhahiri na vilivyofichikana)[2]
 
  1. Mali ya kudumu khasa ni ile anayoitoa Muislamu kabla ya kufariki kwake, ama baada ya hapo ni mali ya warithi. [An-Nahl 16: 96]. [Rejea Hadiyth namba 54, 63, 72, 78].  Pia, Imepokelewa kutoka kwa Mutwarrif: ((Binaadamu husema: Mali yangu, mali yangu!  Ee mwanadamu! Je, una mali yoyote isipokuwa uliyoimaliza, uliyoitumia, uliyoivaa kisha ikachafuka, au [bora mali] uliyoitolea sadaka ikatangulizwa?)).[3]
 
  1. Kukumbuka mauti na kuyakhofia kila mara khasa unapotaka kufanya jambo jema au kutenda ovu.
 
  1. Kutoa wakati unaaga dunia hakuruhusiwi kishari’ah, na chochote utakachotoa wakati huo kuwapatia ahli yako na jamaa, hakitahesabiwa, kwani Allaah (سبحانه وتعالى) tayari Ashampatia kila mmoja haki yake kutoka kwa marehemu.
 
  1. Inafaa mja atumie vyema neema ya afya, uzima na mali, kwani hivi ni vitu ambavyo havidumu. Na ikiwa hatoweza kuvitumia kwa maslahi yake na kujikurubisha kwa Allaah (سبحانه وتعالى), basi atakuwa amekhasirika. [Rejea Hadiyth namba 9].
 
 
 



[1] Al-Bukhaariy na Muslim.
[2] Al-Munaafiquwn (63: 10-11).
[3] Muslim.