Rumaysah bint Milhan-mahari yake ilikuwa Qur'aan
Hata kabla kufika Uislam Yathrib, Bi Rumaysa
alifahamika kwa uzuri wa tabia, akili na mwanamke mwenye msimamo. Alijulikana
kwa majina tofauti yakiwemo Rumaysa na Ghumaysah. Yote haya inasemekana
hayakuwa majina yake halisi. Jina lake lilikuwa Sahlah na baadaye kuwa maarufu
kwa jina la Umm Sulaym.
Aliolewa chuo cha kwanza na Malik ibn an Nadr
na kujaaliwa mtoto Anas ibn Malik, sahaba maarufu enzi za Mtume Muhammad (SAW).
Bi Umm Sulaym alikuwa miongoni mwa wanawake wa
mwanzo kusilimu Yathrib. Daawa iliyotolewa na Mus-ab ibn Umayr alietumwa maalum
na Mtume (SAW) kwa kazi hiyo ilimuingia vyema. Ilikuwa ni baada ya kiapo
cha utii ambapo watu kumi na mbili kutoka Yathrib walikwenda Aqaba kando kando
ya mji wa Makka kwa ajili ya kiapo cha utii kwa Mtume (SAW).
Kitendo cha kusilimu Umm Sulaym kilifanyika
bila ya ridhaa ya mumewe Malik. Alikuwa nje ya Yathrib kipindi hicho na
aliporudi aliona mabadiliko kwenye nyumba na kumuuliza mkewe:
“Vipi umepata mwamko nini?”
Akajibu Umm Sulaym, “hapana ila nimemuamini
huyu mtu (akikusudia Mtume (SAW).”
Malik hakufurahishwa kabisa na kitendo cha
mkewe kusilimu na alizidi kukasirika pale mkewe alipokwenda kuitangaza imani
yake hadharani na pia kumfundisha mwanawe Anas mafunzo na mafundisho ya dini
mpya:
Alimfundisha
kutamka, “Laa ilaha illa Llahu Muhammadun Rasuulu Llah.”
Anas alikuwa akipenda kulirudia ‘kalima’ kila
mara nyumbani kwao tena kwa ufasaha kabisa. Malik akajawa na ghadhabu na
kumkanya, “Usiniharibie mwanangu.”
Umm Sulaym akajibu, “Wala sijamuharibu.”
Mumewe aliamua kuondoka kwenye nyumba na
inasemekana baadhi ya maadui zake walimfanyia njama na kumuua. Habari
hizi zilimshitusha Umm Sulaym lakini hazikumhuzunisha. Aliendelea
kumlea mwanawe na kuhakikisha anapata malezi ya uhakika na aliwahi kusema
kwamba hatokuwa tayari kuolewa tena mpaka mwanawe Anas akubali.
Taarifa za ujane wa Umm Sulaym zilipozagaa,
mtu mmoja Zayd ibn Sahl maarufu Abu Talha aliazimia kwenda kumposa kabla ya
watu wengine. Alikuwa na uhakika wa kutokataliwa, kwani alikuwa tajiri na
kuwa na jumba la fahari. Alikuwa askari farasi na mrusha mishale
stadi. Juu ya yote hayo walikuwa wanatoka kabila moja, Banu Najjar.
Abu Talha akaelekea nyumbani kwa Umm
Sulaym. Alikumbuka njiani kwamba Daawa ya Mus-ab ibn Umayr ndio
iliyomfanya asilimu.
Akajisemea, “kwani kitu gani, mbona mumewe
mpaka kufa kwake alikufa katika dini yake na alikuwa akimpinga Muhammad na
ujumbe wake?”
Alifika nyumbani na kugonga, akafunguliwa na
Anas naye alikuwepo. Abu Talhah akajieleza lengo na madhumuni ya ujio ule
ni kutaka kumwoa.
“Mtu kama wewe Abu Talha, si rahisi
kukataliwa. Lakini sitokubali kamwe kuolewa na wewe ukiwa kafiri.”Alijibu
Umm Salaym.
Abu Talha akadhani labda ni tabia tu za
mwanamke kutotoa jibu hapo hapo na kutaka kumzungusha au labda keshapata mtu
tajiri zaidi kuliko yeye.
Hivyo akamwambia, “Nini hasa kinakuzuia
kunikubali, Umm Salaym? Ni chuma cha manjano na cheupe? (dhahabu na fedha).
Dhahabu na fedha! Umm Sulaym alishtushwa
kidogo. Abu Talha akamwambia kwa sauti iliyojaa upole, “Naam”
Umm Sulaym akasema, “Nnakuapia, Abu Talha na
nnaapa kwa Allah (SW) ukikubali kuingia Uislam, nitakuwa radhi kukubali
kama mume wangu bila ya hata dhahabu wala fedha. Uislam wako ndio mahari
yangu.”
Abu Talha alifahamu vyema athari za maneno
yale, na ikawa nafasi muafaka kwa Umm Sulaym kufanya Daawa na kuonesha upofu wa
kuabudu masanamu na kusema:
“Kwani huyu, Mungu unayemuabudu asiyekuwa
Allah (SW) ametoka kwenye udongo, Abu Talha?”
Abu Talha akajibu, “ni kweli”
“Hujioni kama mpumbavu kuabudu sehemu ya mti
halafu sehemu hiyo hiyo iliyobaki kuitumia kuoka mikate na kujipashia moto?
(ikiwa utaachana na itikadi hizo potofu) na ingia uislam, nitakuwa radhi
kukubali kama mume wangu na wala sitodai sadaka (mahari) kutoka kwako mbali na
uislam wako.”
“Nani ataniongoza (kuingia) katika uislam?
“mimi”
“vipi”
“Tamka tamko la haki na ushuhudie kwamba
hapana mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah (SW) na Muhammad
(SAW) na mjumbe wa Allah (SW)
Ukimaliza nenda zako nyumbani na uvunje
masanamu yote na uyatupilie mbali.”
Umm Sulaym na Abu Talha wakaoana. Anas,
mwanawe alikuwa radhi na waislam walikuwa wakisema:
“Hatujawahi kusikia mahari yenye thamani na
hadhi kubwa kuliko mahari Umm Sulaym kwani uislam ndio ulikuwa mahari yake.”
Umm Sulaym aliishi kwa furaha na mumewe na
alizidi kupendezwa kwani zile fani zake zote sasa alizitumia kwa ajili ya
uislam. Abu Talha ni miongoni mwa watu sabini na tatu walioapa kiapo cha pili
cha utii kwa Mtume (SAW) hapo Aqaba.
Abu Talha alipendezwa sana na Mtume
(SAW). Alipenda kukaa na kumuangalia jinsi anavyoongea na jinsi maneno
matamu yanavyotoka kinywani kwa Mtume (SAW). Alishiriki vita vyote
vikubwa na kujulikana zaidi kwa saumu kwani muda mwingi huwa yupo katika
funga. Inasemekana alikuwa na kikataa kimoja maridadi sana Madina kikiwa
kimejaa mitende, mizabibu na kuzungukwa na chemchem za maji.
Siku moja alikuwa akisali chini ya mti na
ndege mmoja mwenye rangi nzuri za kupendeza akaruka mbele yake.
Alishughulishwa na ndege yule mzuri mpaka kusahau rakaa ngapi amesali, mbili?
au tatu?. Alipomaliza akaenda moja kwa moja kwa Mtume (SAW) na kumweleza
jinsi alivyoshughulishwa. Mwisho akasema:
“Shuhudia ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu tokea
leo nimekitoa sadaka kikataa hiki kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mtukufu”
Ilionekana kwamba Mtume (SAW) alikuwa na
huruma sana kwa Umm Sulaym na alipoulizwa akajibu, “Kaka yake aliuwawa pembeni
mwangu.”
Umm Sulaym alikuwa na dada yake maarufu – Umm
Haram,mke wa ubaadah ibn Samit. Alikufa kwenye jahazi akiwa safarini na
kuzikwa Cyprus, mumewe Abu Talha alikufa kwenye jahazi enzi za Ukhalifa wa
Uthman na kuzikwa baharini.
Umm
Sulaym alikuwa mwanamke shujaa, alikuwa akificha silaha kwenye mikunjo yake ya
nguo zake vitani huku akiwashughulikia majeruhi. Alijaribu pia kumhami
Mtume (SAW) pale vita vya Uhud vilipowageukia waislam. Na katika vita vya
Khandaq, Mtume (SAW) alimuona Umm Sulaym kabeba silaha na kumuuliza ni ya
nini. Umm Sulaym akasema, “ni kwa ajili ya kupigana na hawa walioasi”
Mtume (SAW) akamwambia, Mwenyezi Mungu akukinaishe kwa hilo.”
Wakati wa majanga na mitihani, alikuwa mtu wa
subira na uvumilivu wa hali ya juu. Mmoja kati ya watoto wake (Umayr) aliugua
hadi kufa wakati mumewe yupo kwenye kikataa. Alimuosha na kumkafini na
kuwaambia waliokuwepo wasimpe habari mumewe kwani alitaka yeye mwenyewe
kumtaarifu licha ya kuwa na huzuni na msiba wa mwanawe.
Alikuwa
na mtoto mwengine Abdullah, siku chache baada ya kuzaliwa alimpeleka kwa Mtume
(SAW) pamoja na Anas. Mtume (SAW) akamchukua Abdullah na kumuweka
mapajani kwake kasha akasaga tende mdomoni mwake na kumrambisha kidogo Abdullah
akawa anajiramba na Mtume (SAW) kusema, “Waansaar wao wanapenda tende
tu.”
Abdullah alipokuwa mkubwa alijaaliwa watoto
saba na wote walihifadhi Quran.
Umm Sulaym alikuwa muislam, mke na mama wa
kupigiwa mfano. Imani yake ilikuwa ya dhati na hakuwa tayari kuhatarisha
imani yake na malezi ya watoto wake kwa ajili ya fedha na utajiri hata kama
unavutia kiasi gani!
Mapenzi yake kwa Mtume (SAW) yalikuwa makubwa
mpaka kumpatia kijana wake Anas awe mwambata wake. Alichukua jukumu la
kuwafundisha watoto wake na kushiriki kikamilifu katika shida na raha
walizozipata waislam katika kujenga taifa la kiislam na kuishi maisha yake kwa
kutaraji radhi za Mwenyezi Mungu.