Al-Waaqi’ah (56)


سُورَةُ  الْوَاقِعَة
Al-Waaqi’ah (56)

(Imeteremka Makka)


Sura hii imeanzia kwa kusimulia Tukio la Kiyama, na matokeo yatayo ambatana na Tukio hilo. Kisha ikasimulia kuwa viumbe Siku hiyo watakuwa namna tatu. Ikafuatia hayo kwa kufafanua kwa kutosha walio andaliwa kila fungu katika hao, ikiwa ni neema zinazo wafikiana na cheo chao, au ni adhabu inayo nasibiana na ukafiri wao na uasi wao.
Kisha Aya zikaweka wazi baada ya hayo yanayo onekana katika neema za Mwenyezi Mungu Mtukufu, na athari za uweza wake katika viumbe, na makulima, na maji, na moto; na yanayo hitajika kutokana na athari hizi kumsabihi Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumtakasa.

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

إِذَا وَقَعَتِ الْوَاقِعَةُ ﴿١﴾

1. Litakapotokea (hilo) Tukio (Qiyaamah)

لَيْسَ لِوَقْعَتِهَا كَاذِبَةٌ ﴿٢﴾

2. Hakuna cha kukanusha kutokea kwake.

خَافِضَةٌ رَّافِعَةٌ ﴿٣﴾

3. Literemshalo (watu kuwa baadhi kuwa duni na dhalilifu; na) linyanyualo (baadhi daraja na taadhima).

إِذَا رُجَّتِ الْأَرْضُ رَجًّا ﴿٤﴾

4. Itakapotikishwa ardhi mtikiso mkubwa.

وَبُسَّتِ الْجِبَالُ بَسًّا ﴿٥﴾

5. Na yatapondwapondwa majabali.

فَكَانَتْ هَبَاءً مُّنبَثًّا ﴿٦﴾
6. Yatakuwa (chembe za) vumbi zinazoelea hewani.

وَكُنتُمْ أَزْوَاجًا ثَلَاثَةً ﴿٧﴾

7. Na (nyinyi) mtakuwa namna tatu.

فَأَصْحَابُ الْمَيْمَنَةِ مَا أَصْحَابُ الْمَيْمَنَةِ ﴿٨﴾

8. Basi watu wa kuliani; je, ni nani (hao) watu wa kuliani?

وَأَصْحَابُ الْمَشْأَمَةِ مَا أَصْحَابُ الْمَشْأَمَةِ ﴿٩﴾

9. Na watu wa kushotoni; je, ni nani (hao) watu wa kushotoni.

وَالسَّابِقُونَ السَّابِقُونَ ﴿١٠﴾

10. Na waliotangulia mbele, (hao ndio) watakaotangulia mbele.

أُولَـٰئِكَ الْمُقَرَّبُونَ ﴿١١﴾

11. Hao ndio watakaokurubishwa.

فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ ﴿١٢﴾

12. Katika Jannaat za Na’iym.

ثُلَّةٌ مِّنَ الْأَوَّلِينَ ﴿١٣﴾

13. Kundi kubwa kutoka kwa (karne) za awali.

وَقَلِيلٌ مِّنَ الْآخِرِينَ ﴿١٤﴾

14. Na wachache kutoka kwa (karne) za mwishoni.

عَلَىٰ سُرُرٍ مَّوْضُونَةٍ ﴿١٥﴾

15. (Watakuwa) Juu ya makochi ya fakhari yaliyotonewa vito (vya thamani vya mapambo).

مُّتَّكِئِينَ عَلَيْهَا مُتَقَابِلِينَ ﴿١٦﴾

16. Wakiegemea juu yake wakikabiliana.

يَطُوفُ عَلَيْهِمْ وِلْدَانٌ مُّخَلَّدُونَ ﴿١٧﴾

17. Watazungukiwa na auladi wa (ujana wa) wenye kudumu.


بِأَكْوَابٍ وَأَبَارِيقَ وَكَأْسٍ مِّن مَّعِينٍ ﴿١٨﴾

18. Kwa vikombe na mabirika na gilasi za (mvinyo kutoka kwenye) chemchemu.

لَّا يُصَدَّعُونَ عَنْهَا وَلَا يُنزِفُونَ ﴿١٩﴾

19. Hawatoumizwa vichwa kwavyo (vinywaji hivyo), na wala hawatoleweshwa.

وَفَاكِهَةٍ مِّمَّا يَتَخَيَّرُونَ ﴿٢٠﴾

20. Na matunda watakayopendelea.

وَلَحْمِ طَيْرٍ مِّمَّا يَشْتَهُونَ ﴿٢١﴾

21. Na nyama za ndege watakazozitamani.

وَحُورٌ عِينٌ ﴿٢٢﴾

22. Na huwrun-’iyn (wanawake wazuri wa Jannah wenye macho makubwa ya kupendeza).

كَأَمْثَالِ اللُّؤْلُؤِ الْمَكْنُونِ ﴿٢٣﴾

23. Kama (mfano wa) lulu zilizohifadhiwa.

جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٢٤﴾

24. Jazaa kwa yale waliyokuwa wakitenda.

لَا يَسْمَعُونَ فِيهَا لَغْوًا وَلَا تَأْثِيمًا ﴿٢٥﴾

25. Hawatosikia humo upuuzi na wala (maneno au kauli za) dhambi.

إِلَّا قِيلًا سَلَامًا سَلَامًا ﴿٢٦﴾

26. Isipokuwa itasemwa: “Salama, salama!” 

وَأَصْحَابُ الْيَمِينِ مَا أَصْحَابُ الْيَمِينِ ﴿٢٧﴾

27. Na watu wa kuliani, je, ni nani (hao) watu wa kuliani?

فِي سِدْرٍ مَّخْضُودٍ ﴿٢٨﴾

28. (Watakuwa) Kwenye (vivuli vya) mikunazi isiyo na miba.

وَطَلْحٍ مَّنضُودٍ ﴿٢٩﴾

29. Na migomba ya ndizi iliyopangwa matabaki.

وَظِلٍّ مَّمْدُودٍ ﴿٣٠﴾

30. Na kivuli (kirefu) kilichotanda.

وَمَاءٍ مَّسْكُوبٍ ﴿٣١﴾

31. Na maji yamiminikayo.

وَفَاكِهَةٍ كَثِيرَةٍ ﴿٣٢﴾

32. Na matunda mengi (ya kila aina).

لَّا مَقْطُوعَةٍ وَلَا مَمْنُوعَةٍ ﴿٣٣﴾

33. Hayana kikomo na wala hayakatazwi.

وَفُرُشٍ مَّرْفُوعَةٍ ﴿٣٤﴾

34. Na matandiko yaliyoinuliwa.

إِنَّا أَنشَأْنَاهُنَّ إِنشَاءً ﴿٣٥﴾

35. Hakika Sisi Tunawaanzisha (huwrun-’iyn) uanzishaji.

فَجَعَلْنَاهُنَّ أَبْكَارًا ﴿٣٦﴾

36. Tunawafanya mabikra.

عُرُبًا أَتْرَابًا ﴿٣٧﴾

37. Wenye mahaba kwa waume zao, hirimu moja.

لِّأَصْحَابِ الْيَمِينِ ﴿٣٨﴾

38. Kwa ajili ya watu wa kuliani.

ثُلَّةٌ مِّنَ الْأَوَّلِينَ ﴿٣٩﴾

39. Kundi kubwa kutoka kwa (karne) za mwanzoni.

وَثُلَّةٌ مِّنَ الْآخِرِينَ ﴿٤٠﴾
40. Na Kundi kubwa (pia) kutoka kwa (karne) za mwishoni.

وَأَصْحَابُ الشِّمَالِ مَا أَصْحَابُ الشِّمَالِ ﴿٤١﴾

41. Na watu wa kushotoni, je, ni nani (hao) watu wa kushotoni?

فِي سَمُومٍ وَحَمِيمٍ ﴿٤٢﴾

42. (Watakuwa) Kwenye Moto ubabuao na maji yachemkayo.


وَظِلٍّ مِّن يَحْمُومٍ ﴿٤٣﴾

43. Na kivuli cha moshi mweusi mno.

لَّا بَارِدٍ وَلَا كَرِيمٍ ﴿٤٤﴾

44. Si baridi na wala si kustarehe.


إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَٰلِكَ مُتْرَفِينَ ﴿٤٥﴾

45. Hakika wao walikuwa kabla ya hayo mutrafiyn (wanaostareheshwa kwa anasa za dunia).

وَكَانُوا يُصِرُّونَ عَلَى الْحِنثِ الْعَظِيمِ ﴿٤٦﴾

46. Na walikuwa wakishikilia kwenye (ufanyaji wa) dhambi kubwa.

وَكَانُوا يَقُولُونَ أَئِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ ﴿٤٧﴾

47. Na walikuwa wakisema: “Je, hivi (kweli sisi) tukifa na tukawa mchanga na mifupa, hivi (ndio kweli) tutafufuliwa?”

أَوَآبَاؤُنَا الْأَوَّلُونَ ﴿٤٨﴾

48. “Au, baba zetu wa awali (pia)?”

قُلْ إِنَّ الْأَوَّلِينَ وَالْآخِرِينَ ﴿٤٩﴾

49. Sema: (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika wa awali na wa mwishoni.

لَمَجْمُوعُونَ إِلَىٰ مِيقَاتِ يَوْمٍ مَّعْلُومٍ ﴿٥٠﴾

50. “Bila shaka watajumuishwa katika mahali siku maalumu.

ثُمَّ إِنَّكُمْ أَيُّهَا الضَّالُّونَ الْمُكَذِّبُونَ ﴿٥١﴾

51. “Kisha enyi wapotofu mnaokadhibisha (kufufuliwa).

لَآكِلُونَ مِن شَجَرٍ مِّن زَقُّومٍ ﴿٥٢﴾

52. “Bila shaka mtakula katika mti wa zaqquwm.

فَمَالِئُونَ مِنْهَا الْبُطُونَ ﴿٥٣﴾

53. “Na kwa huo mtajaza matumbo (yenu).

فَشَارِبُونَ عَلَيْهِ مِنَ الْحَمِيمِ ﴿٥٤﴾

54. “Na mtakunywa juu yake maji ya moto yachemkayo.

فَشَارِبُونَ شُرْبَ الْهِيمِ ﴿٥٥﴾

55. “Tena mtakunywa kama wanywavyo ngamia wenye kiu mno!”

هَـٰذَا نُزُلُهُمْ يَوْمَ الدِّينِ ﴿٥٦﴾

56. Haya ndio mapokezi yao Siku ya Malipo!

نَحْنُ خَلَقْنَاكُمْ فَلَوْلَا تُصَدِّقُونَ ﴿٥٧﴾

57. Sisi Tumekuumbeni, basi kwa nini hamsadiki?

أَفَرَأَيْتُم مَّا تُمْنُونَ ﴿٥٨﴾

58. Je, mnaona (mbegu ya uzazi) mnayoitoneza?

أَأَنتُمْ تَخْلُقُونَهُ أَمْ نَحْنُ الْخَالِقُونَ ﴿٥٩﴾

59. Je, nyinyi ndio mliyoiumba (ikawa kiumbe), au Sisi ndio Waumbaji?


نَحْنُ قَدَّرْنَا بَيْنَكُمُ الْمَوْتَ وَمَا نَحْنُ بِمَسْبُوقِينَ ﴿٦٠﴾

60. Sisi Tumekadiria (majaaliwa) baina yenu mauti, na wala Sisi   Hatushindwi.


عَلَىٰ أَن نُّبَدِّلَ أَمْثَالَكُمْ وَنُنشِئَكُمْ فِي مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٦١﴾

61. Kwamba Tuwabadilishe wengine mifano yenu, na Tukuumbeni katika (umbo) msilolijua.

وَلَقَدْ عَلِمْتُمُ النَّشْأَةَ الْأُولَىٰ فَلَوْلَا تَذَكَّرُونَ ﴿٦٢﴾

62. Na bila shaka mmejua umbo la awali, basi kwanini hamkumbuki?

أَفَرَأَيْتُم مَّا تَحْرُثُونَ ﴿٦٣﴾

63. Je, mnaona (mimea) mnayopanda?

أَأَنتُمْ تَزْرَعُونَهُ أَمْ نَحْنُ الزَّارِعُونَ ﴿٦٤﴾

64. Je, ni nyinyi ndio mlioiotesha, au Sisi ndio Tulioiotesha?

لَوْ نَشَاءُ لَجَعَلْنَاهُ حُطَامًا فَظَلْتُمْ تَفَكَّهُونَ ﴿٦٥﴾

65. Lau Tungelitaka, Tungeliifanya mapepe (haizai), mkabakia   mnanung’unika (mnajuta).

إِنَّا لَمُغْرَمُونَ ﴿٦٦﴾

66. (Mkisema): “Hakika sisi tumegharimika.

بَلْ نَحْنُ مَحْرُومُونَ ﴿٦٧﴾

67. “Bali sisi tumenyimwa.”

أَفَرَأَيْتُمُ الْمَاءَ الَّذِي تَشْرَبُونَ ﴿٦٨﴾
68. Je, mnaona maji ambayo mnakunywa?

أَأَنتُمْ أَنزَلْتُمُوهُ مِنَ الْمُزْنِ أَمْ نَحْنُ الْمُنزِلُونَ ﴿٦٩﴾

69. Je, ni nyinyi ndio mliyoyateremsha mawinguni, au Sisi ndio Wateremshaji?

لَوْ نَشَاءُ جَعَلْنَاهُ أُجَاجًا فَلَوْلَا تَشْكُرُونَ ﴿٧٠﴾

70. Lau Tungelitaka, Tungeliyafanya machungu basi kwa nini hamshukuru?

أَفَرَأَيْتُمُ النَّارَ الَّتِي تُورُونَ ﴿٧١﴾

71. Je, mnaona moto ambao mnauwasha?

أَأَنتُمْ أَنشَأْتُمْ شَجَرَتَهَا أَمْ نَحْنُ الْمُنشِئُونَ ﴿٧٢﴾

72. Je, ni nyinyi ndio mliouanzisha mti wake, au Sisi ndio Waanzilishaji?

نَحْنُ جَعَلْنَاهَا تَذْكِرَةً وَمَتَاعًا لِّلْمُقْوِينَ ﴿٧٣﴾

73. Sisi Tumeufanya (huu moto) kuwa ni tadhkiratan (ukumbusho) na manufaa kwa wasafiri (na wengineo duniani).

فَسَبِّحْ بِاسْمِ رَبِّكَ الْعَظِيمِ ﴿٧٤﴾

74. Basi sabbih kwa Jina la Rabb (Mola) wako Mtukufu.


فَلَا أُقْسِمُ بِمَوَاقِعِ النُّجُومِ ﴿٧٥﴾

75. Basi Naapa kwa maanguko ya nyota.

وَإِنَّهُ لَقَسَمٌ لَّوْ تَعْلَمُونَ عَظِيمٌ ﴿٧٦﴾

76. Na hakika hicho ni kiapo kikubwa mno lau mngelielewa.

إِنَّهُ لَقُرْآنٌ كَرِيمٌ ﴿٧٧﴾

77. Hakika hii (mnayosomewa) bila shaka ni Qur-aan Karimu.

فِي كِتَابٍ مَّكْنُونٍ ﴿٧٨﴾
78. Katika Kitabu kilichohifadhiwa. (Lawhum-Mahfuudhw).

لَّا يَمَسُّهُ إِلَّا الْمُطَهَّرُونَ ﴿٧٩﴾

79. Hakuna akigusaye isipokuwa waliotakaswa.


تَنزِيلٌ مِّن رَّبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٨٠﴾

80. Ni uteremsho kutoka kwa Rabb (Mola) wa walimwengu.

أَفَبِهَـٰذَا الْحَدِيثِ أَنتُم مُّدْهِنُونَ ﴿٨١﴾

81. Je, kwa al-hadiyth hii nyinyi ni wenye kuibeza?

وَتَجْعَلُونَ رِزْقَكُمْ أَنَّكُمْ تُكَذِّبُونَ ﴿٨٢﴾

82. Na mnafanya (shukurani) za riziki yenu kuwa nyinyi mnakadhibisha.

فَلَوْلَا إِذَا بَلَغَتِ الْحُلْقُومَ ﴿٨٣﴾

83. Basi mbona (hamuizuii roho kutolewa) ifikapo kooni.

وَأَنتُمْ حِينَئِذٍ تَنظُرُونَ ﴿٨٤﴾

84. Nanyi wakati huo mnatazama.

وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنكُمْ وَلَـٰكِن لَّا تُبْصِرُونَ ﴿٨٥﴾

85. Nasi Tuko karibu naye zaidi (anayefariki) kuliko nyinyi, lakini hamuoni.


فَلَوْلَا إِن كُنتُمْ غَيْرَ مَدِينِينَ ﴿٨٦﴾

86. Basi kwa nini ikiwa (mnadhani kuwa) hamuwajibiki malipo?

تَرْجِعُونَهَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٨٧﴾

87. Muirudishe (hiyo roho mwilini mwake), mkiwa ni wakweli?

فَأَمَّا إِن كَانَ مِنَ الْمُقَرَّبِينَ ﴿٨٨﴾

88. Basi (anayefariki) ikiwa atakuwa miongoni mwa waliokurubishwa.

فَرَوْحٌ وَرَيْحَانٌ وَجَنَّتُ نَعِيمٍ ﴿٨٩﴾

89. Basi Rawh (mapumziko ya raha), na rayhaan (manukato), na Jannah ya Na’iym.

وَأَمَّا إِن كَانَ مِنْ أَصْحَابِ الْيَمِينِ ﴿٩٠﴾

90. Na kama (anayefariki) atakuwa miongoni mwa watu wa kuliani.

فَسَلَامٌ لَّكَ مِنْ أَصْحَابِ الْيَمِينِ ﴿٩١﴾

91. Basi (ataambiwa): “Salaam (amani) juu yako (wewe ni) kutoka kwa watu kuliani.”

وَأَمَّا إِن كَانَ مِنَ الْمُكَذِّبِينَ الضَّالِّينَ ﴿٩٢﴾

92. Na kama (anayefariki) atakuwa miongoni mwa wakadhibishaji wapotofu.

فَنُزُلٌ مِّنْ حَمِيمٍ ﴿٩٣﴾

93. Basi mapokezi (yake yatakuwa) maji ya moto yachemkayo.

وَتَصْلِيَةُ جَحِيمٍ ﴿٩٤﴾

94. Na kuunguzwa na (Moto wa) Jahiym.


إِنَّ هَـٰذَا لَهُوَ حَقُّ الْيَقِينِ ﴿٩٥﴾

95. Hakika hii bila shaka ni haki yenye yakini.

فَسَبِّحْ بِاسْمِ رَبِّكَ الْعَظِيمِ ﴿٩٦﴾

96. Basi sabbih kwa Jina la Rabb (Mola) wako Mtukufu.




Ukitaka kusoma Sura nyengine Rejeauliko toka
Ukiwa una shauri au maelezo juu ya tarjuma hii, andika kwa anwani hii falhaqqiy@gmail.com