'Amr ibn Jam'uh - Hekima Ilimsilimisha



'Amr ibn Jam'uh- hekima ilimsilimisha

 
Amr ni mmoja katika viongozi wa Yathrib enzi za ujahiliya.  Alikuwa mkuu wa Banu Salamah na alifahamika sana kwa ukarimu.
 
Kila kiongozi wa mji alipewa hadhi ya kuwa na sanamu nyumbani kwake.  Siku hizo waliamini kwamba sanamu hilo litamsaidia kwa kila atakakalolifanya.  Kiongozi alitarajiwa kulitolea kafara sanamu lake kwa siku maalumu na kuliomba msaada hasa wakati wa shida. Sanamu la Amr liliitwa Manat.  Alilichonga kwa ubao wa thamani na alitumia muda wake mwingi, fedha na hadhari ya hali ya juu kulitunza na kulijaza manukato ya gharama aina kwa aina.
 
Amr alikuwa na miaka sitini pale uislam ulipoanza kuingia Yathrib. Nyumba hadi nyumba zilitambulishwa dini hii mpya chini ya Mus-ab ibn Umayr alietumwa rasmi na Mtume (SAW) kabla ya Hijra. Kupitia kwake Mus-ab, watoto watatu wa Amr, Muawadh, Muadh na Khallad wakaingia uislam, mkewe Amr; Hindi naye pia akaingia uislam pamoja na wanawe na yote haya yalitokea ndani ya nyumba yake bila ya Amr kujua nini kinaendelea.
 
Hindi aliona jinsi uislam ulivyokuwa ukienea Yathrib na karibu viongozi wote walikwishasilimu isipokuwa mumewe na baadhi ya watu wachache.  Alimpenda mumewe na kuona fahari kubahatika kuwa naye lakini aliingiwa na wasi wasi asije kufa katika ukafiri na hivyo kuingia motoni Jahannam.
 
Na katika kipindi hicho hata Amr mwenyewe hakuwa akijisikia. Aliogopa kuona wanawe wanatoka katika dini ya baba na babu zao na kufuata mafundisho ya Musab ibn Umayr ambaye kwa muda mchache tu ameweza kuwabadilisha watu kutoka kuabudu masanamu na kuingia katika dini ya kiislam.
 
Siku hiyo Amr akamwambia mkewe:
 
“Jihadhari sana wanao wasikutane na huyu mtu (akiamanisha Mus-ab) kabla hatujatangaza maoni yetu (kuhusu yeye).”
 
“Kusikia ni kutii, lakini hutaki kumsikia mwano Muadh atakayoyasema kutoka kwa mtu huyu?” akajibu mkewe.
 
“Adhabu iwe juu yako! Huyu Muadh tayari amekwisha badilika bila ya mimi kujua!”
 
Hindi alimuonea huruma mumewe ambaye tayari ni mzee na kumwambia:
“Hata bado, lakini amewahi kuhudhuria baadhi ya mikutano yake na amehifadhi baadhi ya alivyofundisha.” Alijibu mkewe.
 
“Mwite aje hapa” Muadh akaja.
 
“Hebu nipe mfano wa anayolingania huyu mtu”
 
Muadh akamsomea Suratul Fatiha. Alipomaliza akasema Amr, “Ni maneno yaliyotimia na mazuri!”  Akaendelea, “Kila kitu anachosema ni kama hivi?”
 
Akajibiwa, “ndio baba sasa unasemaje unataka kwenda kusilimu? Kwani watu wako wote tayari wameshafanya hivyo.
Alikaa kimya kwanza kwa muda, kisha akasema;
 
“Sitofanya hivyo mpaka nimshauri Manat na kumsikiliza akasemaje”
 
“Nini manat atasema baba? Ni kipande cha mbao tu hicho.  Hakiwezi kufikiri wala kusema.”
Baba akasema kwa hasira, “Nimeshakuambia sitofanya chochote bila ya yeye!”
 
Baadaye, Amr akaenda kwa manat.  Ilikuwa ni ada ya wanaoabudu masanamu enzi hizo kumweka bibi kizee nyuma ya sanamu wanapotaka kusema nalo.  Bibi huyu kizee, walivyokuwa wakiamini, atajibu kwa mujibu wa alivyoagizwa na sanamu hilo.  Amr akasimama kwa heshima na taadhima na kuanza kusema nalo kwa sauti ya chini ya unyenyekevu huku akilijaza kila sifa.
 
“Ewe manat! bila ya shaka unamjua huyu mpiga porojo alietumwa kwetu kutoka Makka ambaye anakutakia yote mabaya wewe. Amekuja kutuzuia tusikuabudu. Mimi sitaki kwenda kwake na kula kiapo cha utii licha ya maneno mazuri nilivyoyasikia kutoka kwake.  Hivyo, nimekuja kwako kwa ushauri.  Tafadhali nisaidie.”
 
Hakupata jibu lolote kutoka kwa manat.  Amr akaendelea.
 
“Labda umekasirika lakini mpaka sasa sijawahi kufanya jambo lolote kukudhuru……….. Basi usijali, nitakuacha mpaka hasira zako zipungue.”
 
Wanawe walifahamu fika jinsi baba yao alivyokuwa akimtegemea manat.  Wakaona vipi imani yake ya kuabudu masanamu ilivyoanza kuyumba, na kuona haja ya kumsaidia kuachana naye kabisa.
 
Usiku mmoja watoto wake wakiwa pamoja na rafiki yao Muadh ibn Jabal walikwenda kwa manat.  Walipofika wakamchukua na kumtumbukiza shimoni. Wakarudi majumbani kwao bila ya mtu mwengine kuelewa walichokifanya. Amr alipoamka asubuhi yake, kama kawaida alikwenda kwa unyenyekevu kwa manat kutoa heshima zake: hakumkuta.
 
“Adhabu kali kwenu, nani aliemshambulia mungu wetu jana usiku?” akauliza kwa hasira.
Hakuna aliyejibu.  Akaanza kulitafuta sanamu huku akiwa na hasira na ghadhabu kumjaa na kuapa kwa wale waliotenda uovu huu.  Akaja kuliona kichwa chini miguu juu ndani ya shimo.  Akaliosha na kulitia manukato na kulirudisha sehemu yake huku akisema, “nikimjua aliyekufanya haya nitamuadhibu”
 
Siku iliyofuata wale vijana wakafanya tena vile vile.  Mzee wao nao akarudi kuliokota, kuliosha na kulitia manukato. Mchezo huu ukaendelea kwa siku kadhaa mpaka siku moja Amr akaamua kuweka upanga shingoni mwa sanamu na kuliambia:
 
“Ewe manat, sijui ni nani anayekufanya hivi.  Kama una nguvu zozote basi jikinge nafsi yako na uovu huu, huu upanga ni wako.”
 
Wale vijana wakamsubiri mpaka Amr amelala wakauondoa upanga shingoni na kulitupa kule kule shimoni.
 
Amr akaliona sanamu kichwa chini ila upanga haukuonekana.  Mwishowe akaamini kwamba sanamu halina nguvu yoyote na wala halistahili kuabudiwa haukupita muda akasilimu.  Akaonja utamu wa imani kwa kuamini Mungu mmoja na kuingia na simanzi na huzuni kila anapokumbuka muda wake alioupoteza kwenye shirk.  Kuamini kwake hakukuwa na shaka yoyote ndani na kujitoa yeye mwenyewe, utajiri wake na watoto wake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume (SAW).
 
Upeo wa kujitolea kwake ulionekana kwenye vita vya Uhud.  Aliwaona wanawe watatu wakijiandaa wa ajili ya vita.  Akawatazama jinsi walivyojaa ari ya ima kufa wakiwa mashahidi au kupata ushindi na radhi za Mwenyezi Mungu ikamuingia hamu ya kushiriki.  Akaazimia kutoka na kupigana jihadi chini ya bendera ya Mwenyezi Mungu (SW) na Mtume (SAW) na  vijana wake wakamwambia hapana.  Tayari alikuwa mzee sana na dhaifu.
 
“Baba, hakika Mwenyezi Mungu ameshaondoa wajibu (huu wa jihadi) kwako, kwa nini uchukue jukumu tena,” wakamwambia.
Mzee Amr akakasirika na akaenda moja kwa moja mpaka kwa Mtume (SAW) kulalamika.
 
“Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu, wanangu wanataka kunikosesha huu msingi wa kheri wakidai mimi ni kizee na sina nguvu tena, Wallahi ninataka kuipata pepo kwa njia hii hata kama ni mzee sana na nguvu sinazo tena”
 “Mwachieni, labda Mwenyezi Mungu atamjaalia kuwa shahidi,” Mtume alisema. 
Ilipofika wakati wa kwenda vitani, Amr akamuaga mkewe kisha akaelekea kibla na kuomba.”
 
“Ewe Mola, nijaalie kuwa shahidi na usinirudishe kwenye familia yangu bila ya kupata nililokuwa nikitaraji.”
 
Akatoka akiongozana na wanawe watatu, pamoja na kundi kubwa la watu wa kabila lake, Banu Salamah.
 
Vita viliposhamiri, Amr alionekana akienda huku na huko mstari wa mbele vitani, akiruka ruka kwa nguvu kwa mguu wake mzima, mwengine alikuwa kiguru huku akisema kwa sauti kubwa:
“Nnatamani pepo, nnatamani pepo.”
 
Mwanawe Khallad alikuwa karibu naye na wote wakapigana kwa ushujaa na ari wakimlinda Mtume (SAW) wakati wengine walimtenga na kukimbilia ngawira.  Baba na mwana walianguka na kufariki wakipishana kwa muda mchache baina yao.