Jina lake halisi ni Abdullah ibn
Qays bin Salim na umaarufu wake tokea enzi na enzi alikuwa akijulikana kama Abu
Musa. Jina la Ash’ariy ni la kabila lake la Yemen.
Alitokea Yemen na kuhamia Makkah na
kusilimu baada ya kusikia kuletwa kwa Mtume ambae alikuwa akiwalingania watu
kumuabudu Mungu mmoja.Tetesi hizi zilizidi kuzagaa Yemen za huyu mtu anaedai
kuwa ni Mtume katika mji wa Makkah mpaka kumfanya Abu Musa kufanya safari
kwenda kuhakikisha kama ni kweli.Hakuhakikisha tu bali aliingia moja kwa moja
katika dini ya Allah Subhaanahu Wata’ala.
Muda mwingi alikuwa pamoja na Mtume
Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam akijifunza dini pamoja na kupata mafundisho ya
Daawah.Baadae aliagizwa na Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kurudi Yemen
kuwalingania watu wake dini kwani wakati huo bado uislamu ulikuwa ukipigwa vita
Makkah.
Baada ya kusikia kwamba Waislamu
wamehamia Madina na kuanzisha Dola ya kiislamu Abu Musa alikusanya watu wake na
waliosilimu wote wakaongoza njia kuelekea Madina kwa njia ya bahari na kwa
bahati mbaya upepo ukawavumia vibaya na wakaangukia Habashah. Huko walikutana
na masahaba wengine ambao walikuwa wakijiandaa kuelekea Madina akiwemo Jaafar
ibn Abi Talib .
Imam Ahmad bin Hanbal anasimulia
kwenye Musnad wake kwamba kabla ya kundi hili kuwasili Madina, Mtume Salla
Allahu ‘Alayhi Wasallam aliwasimulia masahaba juu ya ujio wa ugeni huu adhimu
kama alivyoteremshiwa wahy na Jibriyl ‘Alayhi Ssalaam.
Abu Musa alitokea kuwa msomaji
mahiri wa Quraan tokea enzi za Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam. Inasemekana
kitu alichokuwa akikipenda kukifanya katika wakati wake wa mapumziko ikiwa
mchana au usiku basi ni kuisoma Quraan. Masahaba walikuwa wakisimulia hata
wakiwa safarini na kuwa na machofu bado humsikia Abu Musa akisoma Quraan kwa
sauti nzuri akiwaliwaza. Imethibitika kutoka kwa Hadithi sahihi ya Mtume Salla
Allahu ‘Alayhi Wasallam kwamba aliwahi kusema kuhusu Qiraa (kisomo) cha Abu
Musa kwamba:
: لو رأيتني وأنا أستمع
قراءتك البارحة لقد أوتيت مزمارًا من مزامير آل
داود
Laiti ungeliniona
ninavyokisikiliza kisomo chako kizuri hakika umepewa (sauti ya) zumari kama
waliyopewa watu wa Daaud (Alayhi Ssalaam)
Muda wake mwingi hakupenda utumike
ovyo kwani hata wakiwa safarini na masahaba kuanza kuzungumzia mambo ya kidunia
basi huwatanabahisha na kuwausia kuzungumzia imani, aqidah, pepo au moto na
mambo mengine ya dini. Mara nyengine huonekana akisoma Quraan kama ilivyo
kawaida yake. Na alikuwa mwalimu mzuri wa kuisomesha kwani hata baada ya
kufariki kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam alikuwa akienda Msikitini huku
akiwaita waislamu kwa kusema:
“Ndugu zangu subirini na bakieni
nikusomesheni Quraan kama nilivyojifunza kutoka kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi
Wasallam”
Maisha yake yalikuwa Quraan na
Quraan ilikuwa ndiyo maisha yake si kwa kuisoma tu bali hata kwa matendo mpaka
kufikia kuwahi kuwausia waliohifadhi Quraan kwa kusema:
إن هذا القرآن كائن لكم أجرًا وكائن عليكم وزرًا فاتبعوا القرآن ولا يتبعنكم
القرآن، فإنه من اتبع القرآن هبط به على رياض الجنة، ومن تبعه القرآن زج في قفاه
فقذفه في
النار
Hakika hii Quraan ina
sehemu ambayo mtapata ujira na pia ina sehemu ambayo mtapata dhambi basi
ifuateni Quraan na wala Quraan isiwafuate (kuwakimbilia huku nyinyi mnaikimbia)
kwani mwenye kuifuata Quraan basi atateremka nayo ndani ya bustani za peponi.
Na mwenye kufuatwa na Quraan ndiyo itakayombeba na kumvurumisha katika moto”
Abu Musa ni miongoni mwa
masahaba waliokuwa wakiheshimika na kufikia kupewa heshima ya kuwa Kadhi.
Masahaba walikuwa wakisema “Makadhi katika umma huu ni ‘Umar (bin Khattaab),
‘Ali (bin Abi Talib) Abu Musa (Al Ash ‘ariy) na Zaid ibn Thabit”
Alikuwa pia ni miongoni mwa wapokezi
wa Hadithi kutoka kwa Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam na mjuzi katika elimu
ya dini. Na inasemekana aliwahi kukusanya msahafu mzima hata kabla ya amri ya
kukusanywa Quraan ilipotolewa baada ya wengi wa waliohifadhi kufariki.
Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam
alimteua pamoja na Mu’aadh bin Jabal kwenda Yemen kuwalingania watu na alikuwa
akimuusia kuendelea kuwafundisha na kuwaelimisha watu Quraan.
Pia enzi za ukhalifa wa ‘Umar ibnul
Khattaab, Allah amuwie radhi, aliteuliwa kuwa Amiri wa mji wa Basra. Khalifa
‘Umar katika uteuzi wake aliagiza katika wasia akifariki, maamiri wote
aliowateua wabaki kwa mwaka mmoja tu kisha wabadilishwe isipokuwa Abu Musa
pekee aliagiza kuendelea kuwa Amiri kwa miaka mine zaidi! Hii si sudfa bali ni
ile thiqa aliyekuwa nayo Khalifa kwa Amiri wake huyu ambae alisifika kwa ukweli
na uadilifu.Kwani khalifa hakutaka kubeba jukumu wakati amekwishaondoka duniani
lakini alikuwa tayari kwa Abu Musa Al Ash’Ariy. Ni khalifa huyu huyu alikuwa
kila akimuona Abu Musa humwambia:
: ذكرنا ربنا تعالى، فيقرأ (أي القرآن).
“Tukumbushe mola wetu
mtukufu” na (Abu Musa) alikuwa akiwasomea (Quraan)
Moja katika riwaya zilizopokewa kutoka kwa Abu Musa zikiwa
na ujumbe mzito ni kama alivyowahi kuhutubia waislamu na kusema :
أيها الناس، ابكوا فإن
لم تبكوا فتباكوا، فإن أهل النار يبكون الدموع حتى تنقطع، ثم يبكون الدماء حتى لو
أرسلت فيه السفن لجرت.
رواه الإمام أحمد رحمه الله.
Enyi watu lieni machozi na kama hamlii basi
lizaneni ili mtokwe na machozi kwani watu wa motoni watatokwa na machozi mpaka
yatakatika kisha wataanza kutokwa na machozi ya damu mpaka ingeliletwa meli
basi ingelielea (kwa wingi
wake) Ahmad.
Abu Musa alikuwa mwana jihadi shujaa na kupigana katika
vingi na aliwahi kupewa sifa ya mpanda farasi mahiri vitani . Aliwahi
kuteuliwa kuwa kiongozi na amiri jeshi wa jeshi la waislamu waliopigana katika
vita vya Sasania katika mji wa Tutsar huko Isfahan(Iran) Jeshi hili pia
lilikuwa na masahaba maarufu kama ‘Ammaar bin Yaasir, Al Barraa bin Maalik
pamoja na ndugu yake Anas na wengineo.
Na wakati ilipokuja fitna kubwa kati ya waislamu
kupigana wenyewe kwa wenyewe kwa ajili ya ukhalifa, msimamo wa Abu Musa
ulikuwa kutojifunga na kundi lolote na ni wazo lake la hekima alilolitoa
kujaribu kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe pale alipotoa rai kwamba wote
waliokuwa wakidai ukhalifa waache kwanza na jambo la kuchagua khalifa mwengine
liachiwe kwa waislamu wenyewe.
Licha ya busara zake kutofanyiwa kazi ipasavyo
aliendelea na msimamo wake wa kutojifunga na upande wowote huku akiomba du’aa
maarufu akisema: “Allahumma anta Ssalaam waminka Ssalaam”.
Mwishoni mwa uhai wake inasemekana alihamia Makkah ambapo
aliishi na kufariki katika mwaka 42 au 52 Hijriyah.