Abdullah ibn Umm Maktoum- kipofu alieithamini jihadi



Abdullah ibn Umm Maktoum- kipofu alieithamini jihadi
 
Abdullah ni bint ami wa Bi Khadija bint Khuwaylid, mama wa waislam.  Baba yake ni Qays ibn Zayd na mama yake Bi Aatikah bint Abdullah. Mama yake aliitwa Umm Maktoum (mama wa aliefichwa) kwa sababu ya kuzaa mtoto kipofu.
 
Abdullah alishuhudia jinsi uislam ulivyoaanza na kukua Makka kwani ni miongoni mwa watu wa mwanzoni kusilimu.  Alishuhudia mateso na madhila waliyoyapata waislam Makka na yeye mwenyewe kuteswa kama ilivyokuwa kwa masahaba wa Mtume (SAW).  Msimamo wake wa dhati na kujitolea muhanga kuilinda dini ya Mwenyezi Mungu (SW) ni silaha pekee ya imani iliyowasaidia na mateso ya maquraysh na kuzidi kuziongeza nguvu imani zao.
 
Abdullah alikuwa na hamu sana kuihifadhi Quran na hivyo kila nafasi anayoipata aliitumia kwa kazi hii.  Bila ya shaka, pupa na wingi wa msisitizo kutoka kwake ulifikia wakati mwengine kuwa maudhi, kwani bila ya kukusudia alikuwa akimshughulisha sana Mtume (SAW).
 
Katika kupindi hiki Mtume (SAW) alikuwa akikutana na wakubwa wa kiquraysh na alitamani kusilimu kwao.  Katika siku hii alikuwa na mkutano na Utbah ibn Rabiah na kaka yake Shaybah, Amr ibn Hisham (Abu Jahl), Umayyah ibn Khalaf na Walid ibn Mughirah ambaye ni baba wa Khalid ibn Walid.
 
Alianza kwa kuwasimulia kuhusu uislam na kuwasihi wakubaliane naye na kuachana na ibada ya masanamu. Alizidi kuwanasihi kuingia uislam au kwa uchache basi kutowatesa waislam.  Wakati akishughulika nao, Abdullah akaja na kumuomba Mtume (SAW) amsomee aya:
 
“Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu nifundishe yale aliyokufundisha Mwenyezi Mungu.”
 
Mtume hakupendezwa na kitendo kile na kusonya na wala hakumshughulikia huku akiendelea kujadiliana na wakubwa wa kiquraysh akitaraji kusilimu kwao kutasaidia sana, risala yake na kuzidi kuihuisha dini.  Baada ya kumaliza tu na kwenda zake akaanza kujihisi kutetemeka na kama anataka kupoteza fahamu wakati aya zifuatazo zilikuwa zikiteremka kwa njia ya wahy:
Abasa 1-16
 “Alikunja kipaji na akageuka.Kwa sababu alimjia kipofu.Na nini kitajuulisha pengine yeye atatakasika?.Au atawaidhika na mawaidha yamfae? Ama ajionaye hana haja.Wewe ndie unamshughulikia? Na si juu yako kama hakutakasika. Ama anaekujia kwa juhudi.Naye anaogopa.Ndio wewe unampuuza?. Sivyo hivyo! huku ni kukumbushana. Basi anayependa akumbuke. Yamo katika kurasa zilizoheshimiwa. Zilizoinuliwa, zilizotakaswa. Zimo mikononi mwa Malaika waandishi.Watukufu,wema” 
Ni aya kumi na sita ambazo ziliteremshwa kwa Mtume (SAW) kuhusu Abdullah ibn Umm Maktum. Ni aya ambazo zinaendelea na kuendelea kusomwa mpaka siku ya mwisho.
 

Toke siku hiyo, Mtume (SAW) akawa mkarimu sana kwa Abdullah na kumpa rukhsa kuuliza lolote atakalo na kumtimizia haja zake na pia kumchukua kwenye majlis yake.  Na hili si geni kwani karipio alilolipata kutoka kwa Mwenyezi Mungu tena kwa njia ya wahy lilikuwa fundisho kwake.
 
Baadaye akikutana na Abdullah alikuwa akimsalimia kwa maamkizi haya ya unyenyekevu.
“Tunamkaribisha kwa yule ambaye kwa tukio lake Mwenyezi Mungu amenikaripia”  
Pale mateso ya maquraysh dhidi ya Mtume (SAW) na waislam yalipokithiri, Mwenyezi Mungu alitoa rukhsa ya Hijrah.  Abdullah hakuchelewa yeye na Musab ibn Umayr walikuwa masahaba wa kwanza kufika Madina.
 

Walipofika tu, walianza kujadiliana na watu wa Madina juu ya uislam, kuwasomea Quran na kuwafundisha dini ya Mwenyezi Mungu. Na Mtume (SAW) alipowasili Madina akamteua Abdullah pamoja na Bilal ibn Ribah kuwa waadhini.
 
Bilal akiadhini, Abdullah huqimu.  Abdullah akiadhini Bilal anaqimu. Katika mfungo wa Ramadhani wakajiwekea utaratibu maalum mmoja wao ataadhini kuamsha watu kwa ajili ya kula daku mwengine ataadhini kuwataarifu kuingia alfajiri.  Bilal aliwaamsha na Abdullah kutangaza kuingia alfajiri.
 
Moja katika majukumu aliyopewa Abdullah ibn Umm Maktum na Mtume (SAW) ni kumkaimu wakati akiwa hayupo.  Karibu mara kumi Mtume (SAW) alimwachia jukumu hili wakati hayupo.
 
Muda mfupi baada ya vita vya Badri, Mtume (SAW) alipata wahy kuonesha kupanda daraja kwa wale wanajihadi kuliko wale “Al-qaaidiin” waliobaki  nyumbani.  Hii ni kwa kuwatia moyo zaidi wapiganaji jihadi na kumtia mori huyu aliebaki naye kujihimu katika kupata fadhila adhimu za jihadi. Aya hii ilimuathiri sana Ibn Umm Maktum.  Ilimuuma sana kujiona hayupo kwenye hadhi na daraja ya juu na akasema kumwambia Mtume (SAW).
 
“Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu, kama ningeweza kwenda jihadi basi ningelifanya”
 
Kisha akamuomba Mwenyezi Mungu ateremshe wahy kwa watu walio na udhuru kama yeye na wengine ambao hawakubaki majumbani kwa kutaka.
 
Ombi lake hili likakubaliwa na aya nyingine ikateremka kuwaruhusu wenye vilema kubaki majumbani: An Nisaa/95
 Hawawi sawa waumini waliokaa tu wala hawana dharura na wale wanaopigana katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao. Mwenyezi Mungu amewatukuza cheo wale wanaopigana kwa mali yao na nafsi zao kuliko wale wanaokaa tu.ingawa Mwenyezi Mungu amewaahidi mashukio mema. Lakini Mwenyezi Mungu amewafadhili wanaopigana,kwa ujira mkubwa kuliko wanaokaa. 
Ijapokuwa aliruhusiwa kutokwenda jihadi, nafsi ya Ibn Umm Maktum ilikataa kata kata kukaa bure tu  huku vita vikiendelea.  Nafsi zilizoadhimu haziwezi kuwa na furaha zikiwa mbali na matukio makubwa.  Akajipangia kazi vitani.
“Niwekeni kati kati ya safu mbili na mnipe bendera.  Nitaibeba na kuilinda na kwa kuwa mimi ni kipofu sitoweza kukimbia.”
 
Mwaka wa 14 hijriya, Umar aliamua kuandaa mkakati rasmi wa kupata njia ya kutangaza uislam ulimwenguni. Ilihitajika kupambana na waajemi na kuwashinda ili kupata njia ya kupita.  Hivyo akawaandikia barua ma Amiri wa tawala za kiislam.
 
“Nawaagiza mleteni yoyote mwenye silaha au farasi au yoyote atakayeweza kusaidia.  Na mfanye haraka”
 
Makundi ya waislam kutoka kila kona yakaitikia wito wa Amirul Muuminiin na kukusanyika Madina miongoni mwao alikuwepo mpiganaji jihadi kipofu ibn Umm Maktum.
 
Saad ibn Abi Waqqas akachaguliwa kuliongoza jeshi la waislam na Umar ibnul Khattab.  Walipofika Qadissiyyah wakamkuta ibn Umm Maktum yupo tayari keshavaa nguo za kivita.  Aliahidi kuibeba bendera ya waislam au kuuwawa kwa hilo.
 
Majeshi yalikutana na kupigana kwa siku tatu.  Vita hivi vinahesabika kwa vita vikali na vikubwa katika historia nzima ya kiislam ya kuikomboa miji na nchi. Siku ya tatu yake waislam wakapata ushindi ambao ulikuwa mkubwa na wa kihistoria kuweza kuiangusha moja katika tawala zilozokuwa zikitawala duniani. 
 
Aqeedah na Tauhid zikasimama kwenye nchi iliyokuwa ikiabudu masanamu. Gharama ya ushindi huu mkubwa ilikuwa ni maelfu ya mashahidi waliouwawa.  Miongoni Ibn Umm Maktum, alionekana tayari amekata roho huku kaishikilia bendera.