Abdullah ibn 'Umar-mwambata wa Mtume (SAW)

Abdullah ibn 'Umar-mwambata wa Mtume (SAW)
 
Katika mji wa Shaykhan, uliopo baina ya Madina na mlima Uhud, jeshi la waislam wapatao elfu moja likiongozwa na Mtume Muhammad (SAW) lilisimama huku jua likitua. Mtume (SAW) akateremka kutoka kwenye farasi wake, Sakb. Alivaa vazi la kivita, kilemba kilichomzunguka kofia yake ya chuma, nguo ya chuma kifuani na juu yake koti kubwa huku ala ya upanga wake ikining’inia.
 
Magharibi, Bilal akaadhini na wakasali. Baada ya sala Mtume (SAW) akalipitia jeshi lake na hapo kuwaona watoto wanane ambao licha ya umri wao kuwa mdogo walikuwa tayari kushiriki katika vita.  Miongoni mwao Usamah ibn Zaid na Abdullah ibn Umar.   Zaid alikuwa mtoto wa kumlea Mtume . Abdullah,baba yake  ni Umar Ibn Khattab. Wote walikuwa na miaka kumi na mitatu.
 
Mtume (SAW) akatoa amri kwa watoto wote kurudi nyumbani kwao haraka ila wawili ambao walionesha uwezo wa kupigana na hivyo kuruhusiwa kujumuika na jeshi.
 
Tokea utotoni kwake, Abdullah alionesha hamu yake ya kujishughulisha na Mtume (SAW).  Alisilimu hata kabla ya kutimia miaka kumi na kufanya hijra pamoja na baba yake Umar ibn Khattab na dada yake Hafsah. Alitaka kupigana vita vya Badr kabla yake ila alirudishwa nyumbani.
 
 Walipotimia umri wa miaka kumi na mitano, yeye na Usamah waliruhusiwa kujiunga na jeshi katika vita vya Khandak na si kwa ajili ya kuchimba Khandak bali hata kupigana.
 
Tokea kufanya Hijra mpaka kufariki miaka sabiini baadaye, Abdullah alipata mafanikio katika kuutumikia  uislamu na alisifika zaidi kwa kuwa na elimu, uvumilivu na ukarimu, ucha mungu, uadilifu na kuwa imara katika kufanya ibada.
 
Alijifunza mengi kutoka kwa baba yake na wote walibahatika kwa kuwa karibu na Mtume Muhammad (SAW) na hivyo kufaidika kielimu kutoka kwa mwalimu wa walimu. Huziangalia kauli za Mtume (SAW) kwa vizuri na kuyatizama matendo yake kwa kituo katika hali tofauti na yeye mwenyewe kuyatekeleza kwa moyo na kwa mujibu wa alivyomuona Mtume Muhammad (SAW).
Kwa mfano akimuona Mtume (SAW) amesali katika sehemu fulani, basi na yeye atasali katika sehemu hiyo hiyo. Akimuona anaomba dua huku kasimama na yeye atafanya hivyo hivyo.  Akiwa safarini akimuona Mtume (SAW) ameshuka kwenye ngamia wake sehemu na kusali rakaa mbili na yeye akibahatika kupita njia hiyo atasimama sehemu hiyo na kusali.
 
Ilitokea siku moja Makka, ngamia wa Mtume (SAW) alizunguka mizunguko miwili kabla Mtume (SAW) hajashuka na kusali rakaa mbili. Inawezekana ngamia yule alifanya tu kitendo kile bila ya kukusudia lakini  kwa Abdullah alipobahatika kupita sehemu ile naye pia alimfanya ngamia wake azunguke mizunguko miwili kabla ya kumuinamisha na kushuka na kisha kusali rakaa mbili kama alivyofanya Mtume (SAW).
 
Bibi Aisha (RA) alimuona Abdullah akimfuatilia sana Mtume Muhammad (SAW) nyendo zake na kusema,“Hakuna mtu mwengine yoyote aliyekuwa akifuata nyendo za Mtume (SAW) kwa kila sehemu anazoteremka (kipando chake) kama Ibn Umar.
 
Licha ya kuwa karibu sana na Mtume (SAW), Abdullah alichukua tahadhari sana kufika kuogopa, kusimulia hadithi au maneno ya Mtume (SAW).  Husimulia tu pale ambapo ana uhakika wa kukumbuka kila neno alilolitamka.  Hali kadhalika alikuwa akichunga na kusita kutoa fatwa.
Aliwahi kuulizwa hukumu ya jambo fulani na kujibu, “sijui hilo unalouliza” .Yule mtu alipoondoka Abdullah akapiga viganja vyake na kujisemea, “Mtoto wa Umar ameulizwa kwa jambo asilolijua na kusema sijui!”
 
Kutokana na msimamo wake huu hakuwa tayari kuwa kadhi licha ya kuwa na sifa zote.  Alipewa nafasi hii na Uthman ibn Affan na kukataa. Sababu haikuwa kuidharau bali ni hofu yake katika kukosea mambo yanayohusu uislam. Uthman alikubaliana na Abdullah asitangaze hadharani msimamo wake huu isije masahaba wengine nao pia ambao tayari wanaifanya amali hii nao kukataa.
 Abdullah aliwahi kutajwa kama “ndugu wa usiku” kwani alikuwa akikesha usiku akisali akiomba dua huku akilia na kusoma Quran kutafuta msamaha na maghfira kutoka kwa Mwenyezi Mungu (SW).  Siku moja Mtume (SAW) alimwambia dada yake Hafsa, “Mtazame mtu alierehemewa, Abdullah, akiendelea kusimama usiku basi atarehemewa zaidi.” 
Tokea siku hiyo Abdullah aliendelea kusimama usiku kwa ajili ya ibada bila ya kuacha iwe safarini au nyumbani. Ubayd ibn Umayr anasimulia siku moja ziliposomwa aya za Quran Suraatu Nnisaa/ 41-42 kwa Abdullah :
 
“Basi itakuaje  pindi tukiwaletea kutoka kila umma shahidi. Na tukakuleta wewe kuwa shahidi wa hawa? Siku hiyo waliokufuru na wakamuasi Mtume watatamani ardhi isawazishwe juu yao. Wala hawataweza kumficha M/Mungu neno lolote”
 
Abdullah alitokwa na machozi baada ya kuzisikiliza, mpaka ndevu zake zikawa chapa chapa kwa machozi. Na siku moja alikuwa amekaa na wenzake na akasoma suratul Mutafiffin /1-3:
 
“Ole wao hao wapunjao. Ambao wanapojipimia kwa watu hudai watimiziwe. Na wao wanapowapimia watu kwa kipimo au mizani hupunguza…..
 
Alipofika hapa akawa anarudia na kuirudia huku akilia mpaka kufikia kupoteza fahamu.
 
Ucha mungu, ukarimu na kuwa mtu wa kawaida asiye na makubwa ni sifa  ambazo zilimfanya aheshimike mbele ya masahaba na wale waliokuja baada yao Tabiin.  Alitoa alichonacho bila ya kinyongo wala kuwa na khiana hata kwamba yeye mwenyewe angekuwa  muhitaji.
 
Alikuwa mfanyabiashara aliyefanikiwa sana katika biashara zake na muaminifu katika maisha yake yote.  Pamoja na haya pia alikuwa akipata ruzuku kutoka Baytul Maal ambayo pia alikuwa akiitumia kwa maskini na wasiokuwa na uwezo.  Ayyub ibn Wail ar-Rasi anatukumbusha tukio moja la ukarimu wa Abdullah.
 
Siku moja alipewa Abdullah ruzuku yake ya Dirham elfu nne pamoja na blanketi la mahameli. Siku iliyofuata Ayyub alimuona Abdullah sokoni anakopa chakula cha ngamia wake. Alikwenda kwa familia yake na kuuliza, “ kwani Abu Abdul-Rahmman (yaani Abdullah) hakupata Dirham elfu nne na Blanket la mahameli jana? Akajibiwa, “kweli kapata”
 
“Mbona leo nimemuona sokoni ananunua chakula cha ngamia wake wala hana pesa za kulipa? Aliendelea kuuliza Ayyub.
 
Akajibiwa, “kabla hata usiku wa jana haujaingia amezitoa zote halafu akatoka na kujitanda blanketi mabegani, aliporudi hata hilo hakuwa nalo. Tulipomuuliza akasema amempa mtu mmoja masikini”.
 
Abdullah, licha kuwa mkarimu pia alikuwa akihimiza waislam kuwasaidia mayatima, masikini na wanaohitaji. Mara nyingi akila hula pamoja na mayatima na masikini.  Alikuwa akiwakaripia watoto wake kwa kuwadharau masikini na kuwapapatikia matajiri. Aliwahi kuwaasa,
 
“Mnawaalika matajiri na kuwatelekeza masikini.”
 
Kwa Abdullah, utajiri ulikuwa kama utumwa na wala si ubwana. Ni njia tu ya kujipatia mahitaji muhimu na wal si kujifaharisha. Kuishi maisha ya kama mtu wa kawaida asiyependa makuu kulimsaidia katika msimamo wake huu na alipoletewa zawadi ya kanzu ya fahari na rafiki yake kutoka Khurasan na kumwambia, “Nimekuletea hii kanzu toka Khurasan, nnaamini itakuletea utulivu machoni mwako na ningelikushauri uvue hizo nguo zilizochoka na uvae hii kanzu nzuri”
 
“Hebu nioneshe!, alipoona na kuigusa akauliza, “si hariri hii?”
 
Akajibiwa, “Hapana”

Abdullah kidogo alionekana kufurahishwa lakini ghafla aliisukuma huko ile kanzu na kusema,
 
“Hapana nnaichelea nafsi yangu, nina khofu isije ikanitia kiburi na majivuno na Mwenyezi Mungu (SW) hapendi watu wenye kujivuna na jeuri.”
 
Maymun ibn Mahram anasimulia kisa hiki:
 
“Nilingia nyumbani kwa ibn Umar na nikajaribu kuvitia thamani vilivyomo ndani ya nyumba yake, ikiwa ni pamoja na kitanda, shuka, zulia na kila kilichomo nikavikisia havifikii hata Dirham mia moja.”
 
Na hii sio kwamba Abdullah ibn Umar alikuwa masikini , bila ya shaka alikuwa tajiri na si kwa kuwa alikuwa muhitaji kwani bila shaka alikuwa mkarimu laysal Qiyaas!