Abdullah ibn Salaam - Mkitaka Kumuona Mtu wa Peponi Basi Mtizame Huyu



Kutoka katika kitabu
MAISHA YA MASAHABA
 صور من حياة الصحابة
cha Mwandishi Dr. Abdurrahman Raafat Al-basha
Kimefasiriwa na Ustaadh Talib Juma
Alikuwa Al Hussein ibn Salaam mmoja wa wanazuoni wakubwa wa kiyahudi katika Madina. Licha ya khitilafu za mila na dini mbali mbali, alikuwa ni mwenye kutukuzwa na kuheshimiwa.
Alijulikana baina ya watu kwa uchamungu wake na akisifikana kwa msimamo madhubuti na ukweli. Alikuwa ni mwenye kuishi maisha ya utulivu na wakati huo huo ni mwenye msimamo na mwenye manufaa kwa wengine.
Aliugawa wakati wake sehemu tatu. Sehemu moja ndani ya sinagogi[i] kwa ajili ya mawaidha na ibada. Sehemu ya pili kwenye shamba lake akishughulikia mitende, kupalilia na kupandishia. Sehemu ya tatu ni mutalaa (kuipitia) kwenye Tauraat kwa kujiongezea elimu.
Kila anaposoma Tauraat, husimama muda mrefu kwenye habari ambazo zinabashiria kudhihiri Nabii katika  mji wa Makka, atakaekuja kukamilisha risala za Manabii waliopita na kuwa ni Nabii wa mwisho na risala ya mwisho. Alitafuta wasifu wa Nabii huyu mtarajiwa na alama zake na akazidi furaha kwani alijua kwamba atahama mji atakaoteremshwa na kuhamia Madina akiwa ni Muhajiri na kubakia hapa.
Kila anaposoma habari hizi, hisia kumpitia moyoni hutamani kwa Allah Subhaanahu Wata’ala amzidishie umri mpaka adiriki kuja kwa Nabii  mtarajiwa na afurahie kukutana nae na awe wa mwanzo kumfuata.
Allah Subhaanahu Wata’ala aliijibu du’aa yake na akamcheleweshea ajali (kifo) yake mpaka kuja kwa Mtume huyu wa uongofu na rehema.  Na akaandikiwa hadhi ya kukutana nae na kuwa pamoja nae na akaamini haki ambayo ameteremshwa nayo.
Hebu na tumuachie Al Hussein mazungumzo atusimulie kisa cha kusilimu kwake. Hakika yeye ni mbora wa kukisimulia.  Anasema:
“Niliposikia kudhihiri Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) nikatoka kutafuta jina na nasaba yake na sifa zake na wakati na mahala alipoteremshwa na kulinganisha na yale yaliyoandikwa katika vitabu vyetu. Mpaka pale nilipothibitisha ukweli wa da’awah yake, nikazificha habari hizo kuwaambia mayahudi na nikaufunga ulimi wangu na kutokusema lolote lile.
Alipofika Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) Qubaa. watu walitujia na kututangazia kuja kwake, na wakati huo nilikuwa kileleni mwa mtende nikiutengeneza.
Wakati huo shangazi yangu,  Khalida bint Al Haarith amekaa chini ya mti. Niliposikia habari nilisema kwa kelele; “Allahu Akbar!” Akasema; ‘Hasara yako, wallahi ungelisikia kuja kwa Mussa ibn ‘Imraan usingelifanya hivyo.’
Nikamwambia; ‘ Ewe shangazi! hakika huyu ni ndugu wa Mussa ibn ‘Imraan yuko katika dini yake na ameletwa na lile aliloletewa yeye!’ Akanyamaza na kisha akasema; ‘Je huyu ni yule Mtume ambae mliyekuwa mkituambia kuwa atakuja kusadikisha na kukamilisha risala ya waliopita?.’Nikamwambia;  ‘Ndiyo’ Akasema; ‘Kwa hivyo nini cha kufanya?’
Nikatoka hapo hapo kwenda kwa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) nikakuta watu wamezongea mlangoni pake. Nikajaribu kujisogeza mpaka nikawa karibu nae. Na la mwanzo kulisikia kutoka kwake ni kauli yake: ‘Enyi watu salimianeni na mpeane chakula na msali usiku watu wakiwa wamelala, mtaingia peponi kwa salama’. (Hadithi)
Nikawa najaribu kumjaza machoni mwangu na kumsoma mpaka nikawa na hakika kwamba si mtu muongo. Nikasogea na kutoa shahada.
Akaniangalia na kuniuliza; ‘Jina lako nani?’
Nikamwambia  ‘Al Hussein ibn Salaam’
Akasema; ‘Bali ni Abdullah ibn Salaam.’
Nikasema; ‘Naam Abdullah ibn Salaam. Hakika yule aliyekuleta kwa haki, sitopenda mimi kuwa na jina zaidi ya hili ulilonipa baada ya leo’.
Halafu nikaondoka na kurudi nyumbani na kuwalingania watoto wangu, mke wangu na jamaa zangu katika Uislamu na wote wakasilimu pamoja na shangazi yangu Khalida na alikuwa ni kikongwe mtu mzima.
Halafu nikawaambia; ‘Ficheni kwanza kusilimu kwenu dhidi ya mayahudi mpaka nikupeni idhini…’ Wakasema; ‘Sawa’ Kisha nikarudi tena kwa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) na kumwambia; ‘Ewe mjumbe wa Allah! Hakika mayahudi ni watu waovu na waongo, nami napenda uwaite viongozi wao mbele yako, na unifiche wasinione nyumbani mwako halafu uwaulize kuhusiana na hadhi na cheo changu kwao, kabla hawajajua uislam wangu. Halafu uwalinganie Uislamu. Kwani wakijua kusilimu kwangu, watanitia dosari na ila na kila upungufu na hata kunipiga vita’.
Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) akanificha ndani ya moja ya nyumba zake. Halafu akawaita na kuwalingania Uislamu na kuwapendekezeshea imani na akawakumbusha kwa yale wanayoyajua kuhusiana nae kama ilivyo ndani ya vitabu vyao. Wakawa wanajadiliana nae kwa kupinga na kubatilisha haki, nami nasikia.
Mtume alipoona hawataki kusilimu akawauliza ‘Al-Hussein ibn Salaam ni mwenye hadhi gani kwenu?’ Wakasema; “Ni bwana wetu, mtoto wa mabwana zetu. Mwanachuoni wetu na mtoto wa wanachuoni wetu’.
Akasema; ‘Je mnaonaje, ikiwa atasilimu nanyi mtasilimu?’ Wakasema ‘Mwenyezi Mungu amuepushe na hilo na hawezi kusilimu’. Hapo nikawachomozea na kuwaambia; ‘Enyi mayahudi muogopeni Allah na fuateni aliyokuja nayo Muhammad’
‘Wallahi hakika mnatambua kwamba yeye ni Mtume wa Allah na mnamkuta ameandikwa ndani ya vitabu vyenu ndani ya Tauraat kwa majina na sifa zake nami nashudhudia kwamba hakika yeye ni Mtume wa Allah na namuamini na kumsadikisha na namtambua (rasmi)’.
Wakasema; ‘Umuongo wewe. Wallahi wewe umuovu wetu na mtoto wa watu waovu kabisa na jahili wewe ni mtoto wa majahili wetu’. Hawakuacha aibu ila walimnasibisha nayo!
Nikamwambia Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) ‘Je sikukwambia hayo hakika mayahudi ni watu waongo na waovu? Na ni watu wa khiyana na uchafu?’.”
Abdallah ibn Salaam aliupokea vyema Uislamu kama vile mwenye kiu ya maji aonapo chemchem. Akajawa na Quraan na ulimi wake ukawa daima umajamaji kwa aya zake zilizo bayana na wazi.
Daima akawa pembeni mwa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) mithili ya ya mtu na kivuli chake. Na akanadhiria kuipata pepo mpaka Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) akambashiria. Na habari za bishara hiyo zikaenea baina ya masahaba. Katika bishara hiyo kuna kisa alichokisimulia alichokipokea Qays ibn ‘Ubaadah na wengineo.
Anasema mpokezi: “Nilikuwa nimekaa katika majlis za elimu ndani ya msikiti wa Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) Madina. Na mlikuwa na mtu mzima ambae nafsi zinapenda kuwa nae na nyoyo zinafurahiwa nae. Akawa anazungumza na watu maneno matamu yenye athari aliposimama watu wakasema; ‘Mkitaka kumuona mtu wa peponi basi mtizame huyu’
Nikauliza; ‘Nani’? Wakasema; ‘Abdullah ibn Salaam’ Nikasema ndani ya nafsi yangu  wallahi nitamfuata. Akatoka hadi  kufikia nje ya Madina halafu akaingia nyumbani mwake. Nikaomba ruhusa akaniruhusu akasema; ‘Unashida gani ndugu yangu?’ Nikamwambia; ‘Nimesikia watu wanakuzungumza wakati ulipotoka msikitini wakisema; Anaependa kumuona mtu wa peponi basi na wamtazame huyu hapa’
Nikakufuata ili nipate habari zako nipate kujua  vipi watu wamejua kwamba wewe ni miongoni mwa watu wa peponi. Akasema; ‘Allah ndie mjuzi wa watu wa peponi ewe kijana wangu’ Nikamwambia; ‘Ndio. Lakini lazima kwa waliyoyasema kuna sababu’ Akasema; ‘Basi nitakusimulia sababu zake.’
Nikasema; ‘Nisimulie Allah akulipe kheri’ Akasema; ‘Wakati nilikuwa nimelala usiku mmoja enzi za Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam), alinijia mtu na kuniambia, amka nikaamka, akanishika mkono nikajikuta nipo njiani ninaelekea kushoto nikataka kufuata akaniambia, iache siyo njia yako hiyo’.
Nikatazama tena nikaona kuna njia safi kuliani akaniambia; ‘Sasa hiyo ifuate’ Nikaifuata mpaka nikafika kwenye bustani iliyo pana na mandhari nzuri ya kupendeza na ujani uliokolea. Katikati yake palikuwa na nguzo ya chuma refu iliyochomekwa ardhini na kumalizika mbinguni. Na mwisho (juu) kuna duara ya dhahabu, Akaniambia; ‘kweya (panda)’ Nikamwambia; ‘Siwezi’
Akaja mtumishi akanisaidia na nikaanza kukweya hadi kufikia kwenye kiduara cha dhahabu na kukishika kwa mikono yote miwili nikabakia nimekishikilia hadi asubuhi.
Mchana wake nikamwendea Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) na kumsimulia ndoto yangu  na Mtume (Sallallahu ‘Alayhi Wasallam) akasema: ‘Ama njia ya kushoto uliyoiona hiyo ni njia ya watu wa kushoto, watu wa motoni, Ama njia ya kulia uliyoiona ni njia ya watu wa kulia, watu wa peponi. Ama bustani ambayo ilikushughulisha kwa mandhari yake nzuri ya kupendeza huo ni Uislamu. Ama nguzo ambayo imo katikati ni kamba madhubuti (‘Urwatul  Wuthqaa) nawe utabaki umeshikamana nayo mpaka kufa.    




[i] Ni nyumba ya ibada ya kiyahudi