019 - Hadiyth Ya 19: Dhulma Irudishwe Duniani Kabla Ya Malipo Ya Aakhirah


عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قَالَ:  ((مَنْ كَانَتْ عِنْدَهُ مَظْلَمَةٌ مِنْ أَخِيهِ مِنْ عِرْضِهِ أَوْ  مِنْ شَيْءٍ  فَلْيَتَحَلَّلْهُ مِنْهُ الْيَوْمَ قَبْلَ أَنْ لاَ يَكُونُ دِينَارٌ وَلاَ دِرْهَمٌ, َإِنْ كَانَ لَهُ عَمَلٌ صَالِحٌ أُخِذَ مِنْهُ بِقَدْرِ مَظْلَمَتِهِ. وَإِنْ لَمْ يَكُنْ لَهُ أُخِذَ مِنْ سَيِّئَاتِ صَاحِبِهِ فَحُمِل عَلَيْهِ))  رواه البخاري
Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Aliyekuwa na kitu cha dhulma cha nduguye kutokana na kumvunjia heshima au kitu chochote, basi amuombe amhalalishie leo kabla haijafika siku ambayo hakutakuwa na dinari wala dirham. Ikiwa ana ‘amali njema, basi zitachukuliwa kwa kadiri ya alichodhulumiwa. Na ikiwa hana, basi zitachukuliwa dhambi za aliyemdhulumu abebeshwe)).[1]
 
Mafunzo Na Hidaaya:
 
  1. Tahadharisho la kumtendea mtu dhulma, kwani dhulma ni viza (giza) Siku ya Qiyaamah. [Hadiyth: ((Ogopeni dhuluma, kwani dhuluma ni viza Siku ya Qiyaamah)).[2] Na dhalimu ana adhabu kali Aakhirah. [Al-‘Araaf 7: 41, Maryam 19: 72, Ghaafir 40: 52].
 
  1. Allaah Ameharamisha dhulma na kutahadharisha. [Hadiyth: ((Enyi waja Wangu! Mimi Nimejiharamishia dhuluma juu ya Nafsi Yangu na Nikaifanya ni haramu baina yenu, basi msidhulumiane)).[3]
 
  1. Kuwekeana heshima ni katika mambo makuu yanayohimizwa katika Uislamu.
 
  1. Kutahadhari kuchuma ya haramu kwa kudhulumu watu kula mali zao bila ya haki. [Al-Baqarah 2: 188, An-Nisaa 4: 29,161].
 
  وَلَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَكُم بَيْنَكُم بِالْبَاطِلِ وَتُدْلُوا بِهَا إِلَى الْحُكَّامِ لِتَأْكُلُوا فَرِيقًا مِّنْ أَمْوَالِ النَّاسِ بِالْإِثْمِ وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ
Na wala msiliane mali zenu kwa ubatilifu na kuzipeleka kwa mahakimu ili mle sehemu katika mali ya watu kwa dhambi nanyi mnajua (kwamba ni haraam)[4]
 
  1. Dhulma inaharibu ‘amali njema, kwani tajiri anayedhulumu atakuwa masikini Siku ya Qiyaamah, na masikini aliyedhulumiwa atakuwa tajiri Siku ya Qiyaamah. [Hadiyth: ((Je, mnamjua muflis?)) Wakasema [watu]: “Muflis kwetu sisi ni yule miongoni mwetu asiyekuwa na dirhamu [pesa] wala vyenye kumnufaisha yeye hapa duniani.” Akasema (صلى الله عليه وآله وسلم) ((Hakika muflis katika Ummah wangu ni yule atakayekuja Siku ya Qiyaamah na Swalaah, Swawm na Zakaah, lakini amemtusi huyu, amemsingizia huyu mwingine kuwa amezini, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya mwingine na kumpiga mwengine. Thawabu zake zitapatiwa huyu na yule mpaka zimalizike. Na zinapokwisha basi madhambi ya hao [aliowadhulumu] atabandikwa nayo, kisha aingizwe Motoni)).[5]
 
  1. Kuharakiza kulipa dhulma duniani wakati fursa bado ipo kabla ya kufikia mauti.
 
  1. Anayedhulumiwa avute subira kwa kutegemea malipo mema ya aliyemdhulumu na kuondoshewa madhambi yake.
 
 



[1]  Al-Bukhaariy.
[2]  Muslim.
[3]  Muslim.
[4]  Al-Baqarah (2: 188).
[5]  Muslim.