015 - Hadiyth Ya 15: Kitendo Cha Bid’ah Hakikubaliwi Katika Dini Yetu

015 - Hadiyth Ya 15: Kitendo Cha Bid’ah Hakikubaliwi Katika Dini Yetu


عَنْ عَائِشَة (رضي الله عنها)  قَالَتْ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم:  ((مَنْ أَحْدَثَ فِي أَمْرِنَا هَذَا مَا لَيْسَ مِنْهُ فَهُوَ رَدّ)) رواه  مسلم
 Imepokelewa kutoka kwa ‘Aaishah(رضي الله عنها)  amesema: Mtume wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mwenye kuzua katika hili jambo [Dini] letu lisilokuwemo humo, litakataliwa)).[1]
Mafunzo Na Hidaaya
  1. Hadiyth hii ni asili ya Dini na nguzo kati ya nguzo kama alivyosema Imaam An-Nawawiy (رحمه الله). Hivyo basi, kuna umuhimu mkubwa wa kumtii Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), kwani hivyo ni kumtii Allaah (سبحانه وتعالى). [An-Nisaa 4: 80].
  1. Dini ya Kiislamu ni Dini ya kufuata maamrisho na si ya kuongeza mambo na kuzusha. [Al-Hashr 59: 7].
  وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ                  
Na lolote (lile) analokupeni Mtume (Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) basi lichukueni, na (lolote lile) analokukatazeni, basi acheni. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Shadiydul-‘Iqaab (Mkali wa kuadhibu)[2]
  1. Jambo lolote linalotendwa kama ni ‘Ibaadah ya kujikurubisha kwa Allaah (سبحانه وتعالى) ambalo halimo katika Qur-aan na  Sunnah ni bid’ah (uzushi) litakataliwa, na mzushi au mtendaji uzushi hatopata thawabu yoyote, hata ikiwa kwa niyyah safi, na itakuwa ni kupoteza juhudi zake na mali yake kwa jambo lisilo na thamani mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى). [Al-Furqaan 25: 23, Al-Kahf 18: 103-104].
  1. Dini ya Kiislamu hairuhusu bid’ah yoyote bali inatilia nguvu kushikamana na Qur-aan na Sunnah, na hiyo ndio njia iliyonyooka ipasayo kufuatwa: [Yuwsuf 12: 108, Al-An’aam 6: 153].
  1. Hili ni onyo kwa Muislamu kutozua jambo lolote katika Dini kwani tayari Dini imekamilika [Al-Maa’idah 5: 2].



[1] Al-Bukhaariy na Muslim.
[2] Al-Hashr (59: 7).